MAADHIMISHO YA MAUAJI YA JANUARI 26 NA 27, 2001 YA CUF YATOKANAYO NA MAANDAMANO YA KUDAI HAKI
Siku ya leo siyo siku ya furaha hata kidogo na wala si siku ya
kujifaharisha, ni siku ya kihistoria kwa chama chetu, ni siku ya
kukumbukwa sana, miaka kumi na nne iliyopita tarehe kama ya leo tarehe
27 Januari, 2001 na tarehe kama ya jana tarehe 26 Januari 2001,
Wanachama wenzetu waliojitoa muhanga, leo hii hawapo wamekwenda mbele ya
haki katika siku kama hii, mama zetu na dada zetu wanaikumbuka kwa
huzuni kubwa siku kama hii ya leo, kwani si vyema kuwakumbusha lakini
inatubidi tuyakumbuke yaliyowakuta siku kama hii ya leo, mama zetu na
dada zetu walibakwa na kunajisiwa na askari wa kidhalimu wa Serikali ya
Chama cha Mapinduzi, na wengine wakaachwa mayatima kwa waume zao kuuwawa
na askari hao hao wa kidhalimu, na kutuachia mayatima na wengine hadi
leo wanaishi na ulemavu.
Kwa mara ya kwanza nchi yetu ilizalisha wakimbizi kwa ndugu zetu na
wanachama wenzetu ilibidi wakimbilie Mombasa nchini Kenya katika
kunusuru maisha yao, wapo wengine waliyakimbia makazi yao na kuishi
maporini na wengine walifia baharini wakati wakijaribu kujinusuru.
Tukizikumbuka nasaha nzuri alizozitoa Mwenyekiti wetu Prof. Ibrahim
Haruna Lipumba mwezi Oktoba 2001 pale Bwawani Hotel Zanzibar wakati wa
kutiliana saini mkataba wa Muafaka alisema kwamba “Ni vyema tukaendelea
kuyakumbuka yaliyotokea ili ibaki kuwa kovu itakayotufanya tusiweze
kuyarudia tena yale yaliyosababisha maafa kama yale kutokea”.
Tukiikumbuka siku kama ya leo inatubidi pia kuzikumbuka siku mbili kabla
ya leo, yaani Januri 25, 2001 wakati Mwenyekiti Prof. Ibrahim Haruna
Lipumba alipopigwa na wenzake na kuvunjwa mkono na askari wa Serikali ya
Chama cha Mapinduzi na kumkamata pamoja na Viongozi wengine waandamizi
na wanachama wenzetu na kuwafungulia kesi ya uchochezi.
Mwenyekiti alikuwa akitekeleza misingi ya Demokrasia kwa mujibu wa
katiba ya nchi ya kukusanyika na kutoa mawazo yako hadharani, jambo
ambalo aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Wiliam Benjamin Mkapa alishatoa
amri kwenyae hotuba yake ya kuuaga mwaka 2000 na kuingia mwaka mpya wa
2001 kwa kukataza mikutano ya hadhara pamoja na maandamano akidai kwamba
uchaguzi umemalizika na washindi wameshajulikana hivyo ni vyema
tukaungana katika kuijenga nchi kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba katika hotuba yake pale Mbagala Zakiem kabla ya kukamatwa kwake, pamoja na kusisitiza nchi kuendeshwa kwa kufuata misingi ya utawala bora, demokrasia na utawala wa sheria, lakini pia aliahidi kuwa kwa vile nchi yetu imepoteza sifa na dira ya kuitwa nchi yenye misingi hiyo, suluhisho pekee ni kufanya maandamano nchi nzima na yeye ndie atakae yaongoza maandamano hayo ambayo aliyatangaza kufanyika siku ya tatu yake yaani tarehe 27, Januari 2001.
Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba katika hotuba yake pale Mbagala Zakiem kabla ya kukamatwa kwake, pamoja na kusisitiza nchi kuendeshwa kwa kufuata misingi ya utawala bora, demokrasia na utawala wa sheria, lakini pia aliahidi kuwa kwa vile nchi yetu imepoteza sifa na dira ya kuitwa nchi yenye misingi hiyo, suluhisho pekee ni kufanya maandamano nchi nzima na yeye ndie atakae yaongoza maandamano hayo ambayo aliyatangaza kufanyika siku ya tatu yake yaani tarehe 27, Januari 2001.
Katika maandamano hayo tulikuwa na madai manne;
- Kutomtambua Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume na kutaka uchaguzi urudiwe
- Kudai Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
- Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
- Katiba Mpya
Pamoja na Mwenyekiti wetu kumkamata wakidhani kwamba watakuwa
wamefanikiwa kutuzuia tusiandamane, halikadhalika watu wawili waliuliwa
siku moja kabla, yaani tarehe 26 Januari pale Zanzibar, kwa agizo la
aliekuwa Makamo wa Rais Marehemu Dk. Omari Alli Juma wakiamini watakuwa
wametutisha kiasi cha kutosha, lakini wapi, tuliandamana na wenzetu
wengine wakawa muhanga. MWENYEZI MUNGU ZILAZE ROHO ZA MAREHEMU WOTE WALIOJITOA MUHANGA MAHALI PEMA PEPONI – AMINY!!
Narudia tena kwa msisitizo; ni hali ya kusikitisha kila inapofika siku kama ya leo, inatukumbusha madhila tuliofanyiwa ndani ya nchi yetu kwa kudai haki, inatukumbusha damu ya ndugu zetu iliyomwagika kwa sababu ya kudai haki, inatukumbusha ulemavu walioupata ndugu zetu kwa sababu ya kudai haki, inatukumbusha dada zetu na mama zetu walioachwa vizuka kwa waume zao waliuwawa kwa sababu ya kudai haki, inatukumbusha binti, dada zetu na mama zetu walibakwa kwa sababu ya kudai haki, inatukumbusha watoto walioachwa yatima kwa sababu yakudai haki, inatukumbusha watu walisamehe Ubunge wao na Uwakilishi wao katika baraza la wawakilishi kwa sababu ya kudai haki.
Muhanga huu waliojiotoa ndugu zetu, ndio matokeo na mafanikio
yaliyojitokeza sasa hivi hadi kufikia wengine kujidai na kujifaragua na
kufikia hata kutoa kejeli na maneno ya kifedhuli na kebehi, wakati ndugu
zetu wanapoteza maisha yao kwa kuandamana wao waliona tunaigiza.
Mafanikio katika madai yetu yale manne;
- Kuhusu kutomtambua aliekuwa Rais wa Zanzibar Amani Karume na kudai uchaguzi kurudiwa; kulipelekea kufikiwa kwa muafaka kati yake na Katibu Mkuu wetu Maalim Seif Sharif Hamad, ndio uliopelekea kupatikana kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ambapo chama chetu kipo varandani Ikulu kwa Maalim Seif kuwa Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, na tunatarajia mwishoni mwaka huu Oktoba 2015 tunaichukua wenyewe Ikulu ya Zanzibar.
- Kuhusu madai ya Tume Huru ya Uchaguzi, kwa upande wa Zanzibar Tume hiyo iliundwa pamoja na kugubikwa na wingi wa makada wa Chama cha Mapinduzi kutokana na mfumo mbovu wa uteuzi, lakini tunaamini huu ni mwanzo tu, kilichobakia ni kupigania maboresho ya Tume hiyo kuwa Huru Kwelikweli na si kama ilivyo sasa. Tunaiasa CCM na Serikali yake Bila Uchaguzi huru na wa Haki Oktoba 2015 Taifa linaweza likarudia historia ya mwaka 2001.
- Kuhusu Daftari la Kudumu la Wapiga kura tulifanikiwa kulipata, nalo huwa linachafuliwa na wajanja wa Chama cha Mapinduzi kwa kulitia mikono, lakini nalo tutalipigania kuhakikisha linatumika ipasavyo na kama tulivyokusudia wakati wakulidai, na kwa vile kuna maboresho ya mfumo mpya wa daftari, tunawaomba wanachama wetu tuhamasishane tujitokeze wote kwenda kujiandikisha kwa Dar es Salaam uandikishaji unaanza Februari 15 mwezi ujao.
- Kuhusu kupatikana kwa Katiba Mpya, ambapo ndani yake kungekuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na mengineyo yaliyomuhimu kwetu sisi katika kuleta haki na usawa kwa wote, CCM na Serikali yake wameuteka mchakato huo hatua za Mwisho za Bunge la Katiba na kuyatupilia mabali mambo yote muhimu yatokanayo na michango ya wananchi wenyewe yaliyokusanywa na Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba na kuingiza mambo yao yenye maslahi ya kifisadi kwa Taifa. CUF – Chama Wananchi tunatoa AGIZO ni marufuku kwa wanachama na wapenzi wetu wote nchi nzima kujitokeza kwenda kupiga kura ya maoni, kwani kushiriki kwa aina yoyote hata kupiga kura ya hapana ni kubariki mchakato haramu uliofanywa na Mafisadi wa Chama cha Mapinduzi.
Waheshimiwa wanachama wenzetu, tunawaomba na tunawasihi sana tuyatumie
maadhimisho haya katika kushauriana namna bora ya kuboresha chama chetu,
na hasa katika kuongeza wanachama watakao kipatia chama chetu ushindi,
na tunaendelea kusisitiza kimbilio letu kubwa liwe ni kwa vijana wetu
tulionao, ni aibu kubwa sana kama utakuwa na kijana mwenye umri wa
kupiga kura na asikuunge mkono wewe kama mzazi wake au mlezi wake,
tukumbuke wosia wa Muasisi wetuMarehemu Shaaban Khamis Mloo, kuwa
tuhamasishane kunzia katika sahani ya chakula, kitandani, ndani ya
shuka, uwani, barazani, chumba kwa chumba, mlango kwa mlango, nyumba kwa
nyumba, katika vijiwe vya kahawa, mabaraza ya bao, kinamama
wanaposukana, vilabu vya mipira, maofisini na kila penye mkusanyiko wa
watu na tujiwekee ahadi kila mwanachama mmoja imalizikapo miezi mitatu
angalau awe ameingiza ndani ya chama sio chini ya wanachama wapya
watatu.
MWISHO;
Tunawaomba radhi na tunawapa pole Wanachama wenzetu wote wa CUF – Chama
cha Wananchi, kwa kuwakumbusha siku hii nzito kwetu na ya majonzi
makubwa TUNAJUA MMEGUSWA, lakini tujifute machozi yetu kwa kuenzi moyo
wa kujitoa kwa ajili ya chama ili kuhakikisha haki inapatikana na chama
chetu kinapata ushindi katika uchaguzi huu ujao, hii ndio namna bora ya
kuwaenzi WAHANGA wetu, tukumbuke “WOGA NI ADUI WA HAKI”
HAKI SAWA KWA WOTE
Prof.Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti CUF Taifa
Mwenyekiti CUF Taifa
Post a Comment