Wabunge
wameelezea kuchoshwa na wizi, matumizi mabaya ya fedha na mikataba
mibovu iliyobainishwa katika taarifa za baadhi ya kamati
zilizowasilishwa bungeni, na kushauri maazimio yapitishwe ili wahusika
wa ufisadi huo wabanwe.
Katika
kuchangia taarifa za Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Kamati ya Bajeti
zilizowasilishwa bungeni, wabunge wengi wameeleza kuchoshwa na mijadala
ya kila mara bungeni inayohusu wizi na ufisadi, badala ya kujadili
maendeleo ya wananchi.
Kwa
mujibu wa wabunge hao, katika taarifa zote zilizowasilishwa, suala la
wizi na matumizi mabaya ya fedha za Serikali limejitokeza kwa wingi,
jambo ambalo wabunge wametaka hatua za makusudi zichukuliwe haraka,
kuliko wabunge kuendelea kulalamika bila kupata suluhu la kudumu.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF)
alitoa mfano wa suala Kampuni ya Ndege (ATCL) lililoainishwa kwenye
taarifa ya PAC juu ya hali ya kifedha na madeni makubwa iliyo nayo.
Madeni
hayo ni pamoja mabilioni ya fedha yanayoendelea kulipwa kwa Kampuni ya
Wallis, kwa huduma ya ndege iliyofanya kazi nchini kwa miezi sita pekee,
na kisha ndege kupelekwa Ufaransa kwa matengenezo.
Alisema chanzo cha tatizo ni mikataba mibovu. “Tulidai
mikataba iletwe bungeni tuipitie. Ikiwa tutaendelea kulalama kwamba
tunaibiwa… wizi kila mahali, ikiwa hatutasaidia Takukuru (Taasisi ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa) kama Bunge kwa kuona kwamba wote waliohusika
na mikataba wanafikishwa mahakamani, itakuwa Bunge hatujatenda haki.
“Kwa
kamati ambazo zimewasilisha taarifa, tupitishe maazimio kwa mikataba
yote yenye utata na walioipitisha, wafikishwe mahakamani. Tulione Bunge
likiwa na meno yake, wote waliohusika wachukuliwe hatua kwa kupelekwa
mahakamani,“ alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM),
alizungumzia suala la Mamlaka ya Bandari (TPA) kutumia Sh bilioni tisa
kulipana posho bila kuidhinishwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina; taarifa
iliyotolewa na PAC.
Bulaya
alihoji majibu ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, ambaye juzi katika
kujibu, alisema TPA walijieleza kwamba walifanya hivyo kutokana na
kutokuwa na uelewa wa sheria.
“Eti
jibu jepesi, hawakuwa na uelewa wa kisheria!. Tunaomba watu wote hao
washughulikiwe. Haiwezekani makosa yawe yale yale na majibu yale yale,” alisema Bulaya.
Kuhusu madeni ambayo mifuko ya hifadhi ya jamii inadai Serikali, Bulaya alisema; “Kila
siku zinapigwa kelele juu ya hali mbaya ya mifuko ya jamii, halafu
Waziri anasema kinaundwa kikosi kazi…hiki ni kikosi kazi cha kumi, hivyo
tisa havijajua tunadaiwa kiasi gani?”
Kwa
upande wa jengo la watu mashuhuri katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu
Julius Nyerere, mbunge huyo alihoji uhalali wa kutumika Sh bilioni 12
kwa ujenzi wake.
“Dili nyingine ukipewa funga mikono, nawa mikono zinagusa maisha ya watu maskini,” alisema.
Bulaya
ambaye pia alihoji sababu za asilimia 10 ya fedha za akina mama na
vijana kutotengwa kwenye halmashauri, alishauri mawaziri kubana
watendaji iwapo hawataki kupigiwa kelele bungeni.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alisema iwapo wizi hautadhibitiwa, nchi haiwezi kubadilika hata ikikusanya matrilioni ya shilingi.
“Ni lini tutajadiliana bungeni bila kujadili wizi? Ifike hatua tujadili sera za kuendeleza Taifa,”
alisema Mbunge huyo na kuongeza kuwa CUF na Chadema haviko kwa ajili ya
kushika madaraka tu, bali ni kwa ajili ya kuwezesha taifa kwenda mbele.
Alisema
katika taarifa ya PAC mwanzo hadi mwisho, kinachosomwa zaidi ni wizi,
jambo alilotaka Serikali kushughulikia watu wanaojenga nyumba kwa
mikataba ya uongo sanjari na ulipaji mishahara hewa.
Pia Mbunge wa Nkenge, Asumpta Mshama (CCM) alihoji ni lini bunge litaelezwa kwamba matumizi ya fedha sasa yanakwenda vizuri.
Mshama
alishauri sheria ya ununuzi iletwe bungeni waibadilishe kwa kile
alichosema, inatoa mwanya mkubwa wa kufanya matumizi mabaya ya fedha.
Post a Comment