Huenda ukurasa mpya ukawa umefunguka kwa wanamuziki wa Tanzania
baada ya kampuni ya mawasiliano ya simu za mokononi ya Tigo kumwaga
zaidi ya Sh150 milioni kulipa wasanii 30 waliotumbuiza katika Tamasha la
tiGOMusic Kiboko Yao Jumamosi iliyopita.
Habari ambazo gazeti hili imezipata, msanii
aliyelipwa fedha kidogo kuliko wote, alitia kibindoni Sh5 milioni,
lakini nyota wenye mvuto walilamba Sh70 milioni.
Kwa kiwango cha chini, iwapo kila mwanamuziki
angepata Sh5 milioni tu, basi jumla ya Sh150 zilitumika kulipa wasanii
kwa onyesho moja tu.
Hata hivyo siyo Kampuni ya Tigo, wala wasanii wenyewe waliokuwa tayari kuzungumza kuhusu malipo halisi waliyopata.
Pia, tofauti na maonyesho mengine ambayo wasanii
hutumbuiza bila ya kusindikizwa na wacheza shoo au wasanii wenzao,
Jumamosi ilishuhudia waburudishaji hao wajitahidi kuhakikisha wanaenea
jukwaani.
“Jamaa wamejitahidi kutaka kuona tunatabasamu na
ndio maana ukaona kila mtu anajitahidi kufanya kitu bora kuliko vyote
alivyowahi kufanya katika huu muziki,” aliweka wazi Fid Q, ambaye jina
lake halisi ni Fareed Kubanda.
Fid Q alipanda jukwaani na wasanii wenzake watatu na kuleta ladha tofauti na anavyofanya katika matamasha mengine yaliyopita.
Young Killer, Stamina na Tifah walikuwa ni wasanii
walioshirikiana na Fid Q katika kufungua ukurasa wa Hip Hop katika
tamasha hilo lililokuwa na lengo ya kuzindua mpango wa kupakua nyimbo za
wasanii kupitia mtandao wa simu uitwao Deezer.
Msanii mwingine ambaye alipanda jukwaani tofauti
na alivyozoeleka ni Ben Pol, mshindi wa tuzo ya Kili katika miondoko ya
R&B, aliyepanda na madansa wazungu.
Hawa walikuwa wakicheza muziki wake wakati
mwenyewe akiimba, hali iliyosababisha shangwe kutoka kwa mashabiki ambao
walizoea kumuona Ben Pol akiimba peke yake jukwaani.
Mtaribu wa tamasha hilo, Alex Galinoma wa Kampuni
ya East Africa TV LTD, alikiri kuwa kulikuwa na azma ya kuhakikisha
wasanii wa nyumbani wanalipwa vizuri na walitekeleza hilo.
“Hayakuwa malipo ya kawaida waliyoyazoea... Hakuna
msanii aliyelipwa hela aliyoizoea. Tulijitahidi kwenda juu, zaidi ya
ile kawaida,” alisema Galinoma.
- Mwananchi
Post a Comment