Dar es Salaam. Wafuasi 30 wa Chama cha Wananchi CUF
wanaokabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama na kukaidi amri
halali ya polisi na kufanya maandamano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana
waliyopewa.
Hakimu Mkazi, Emillius Mchauru jana aliwaachia
huru washtakiwa hao baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya
kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika na kila mdhamini
asaini hati ya dhamana ya maneno ya Sh 100,000.
Baada ya washtakwia hao kukamilisha masharti hayo
ya dhamana, Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 12,2015 kwa
ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Juzi, Mawakili wa Serikali, Joseph Maugo na Hellen
Mushi, katika shtaka la kwanza alidai kuwa Januari 27,2015 katika
eneo la Temeke washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kufanya
uhalifu.
Akisoma hati hiyo ya mashtaka, Maugo katika shtaka
la pili alidai kuwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa 28 kati ya 30
wanaokabiliwa na kesi hiyo, wakiwa katika ofisi ya CUF karibu na
Hospitali ya Wilaya ya Temeke bila ya kuwa na uhalali walifanya
mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano kuelekea Mbagala Zakhem.
Katika shtaka la tatu, ambalo nalo pia
linawakabili washtakiwa 28 kati ya 30 , Wakili huyo wa Serikali, Maugo
alidai kuwa siku hiyo hiyo ya tukio katika eneo la Mtoni Mtongani
waligoma na kutojali tangazo halali lililotolewa na polisi
lisilowaruhusu kuandamana na hata kufanya mkusanyiko usio halali.
Washtakiwa wanaokabiliwa katika kesi hii ni
Shabani Ngurangwa (56), Shabani Tano(29), Shabani Abdallah (40), Juma
Mattar (54), Muhamed Kirungi (40), Athuman Ngumwai (40), Shaweji
Mohamed(39), Abdul Juma(40), Hassan Said (37), Hemed Joho (46) na
Mohamed Ibrahim (31).
Pamoja na Issa Hassan (53), Allan Ally(53), Kaisi
Kaisi (51), Abdina Abdina (47), Allawi Msenga (47), Mohamed Mtutuma
(33), Salehe Ally (43), Abd Hatibu (34), Bakari Malija (43), Abdallah
Ally(32) , Said Mohamed (40), Salim Mwafisi, Salehe Rashid (25),
Abdallah Said(45),Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athuman Said
(39).
Kwa upande wa washtakiwa Dickson Leasson (37) na
Nurdin Msati (37) wao hawahusiki katika shtaka la pili na tatu ambayo
yanawakabili wenzake.
Post a Comment