Moshi. Wananchi wa Jimbo la Vunjo mkoani
Kilimanjaro wamechanga Sh200,000 za nauli ya Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ili aweze kufika jimboni humo
kutoa somo la Katiba.
Fedha hizo zilitolewa juzi na kukabidhiwa kwa
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia wakati akihutubia mikutano ya
hadhara kwa nyakati tofauti katika miji ya Himo na Moshi Mjini kwa lengo
la kuwashukuru wananchi kwa kuwaamini wagombea wa Ukawa na kuwapa
ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya fedha hizo,
Katibu wa Umoja wa Wanawake wa NCCR-Mageuzi, Getrude Pwila alisema kama
hazitatosha kwa nauli ya Jaji Warioba, wako tayari kuchangishana
kuongeza.
“Tunataka tuelimishwe hii Katiba Inayopendekezwa
kwa sababu hatuko tayari kuipigia kura kwa sababu hatuielewi, hatujaiona
wala kuisoma na kuielewa,” alisema Pwila kwa niaba ya wananchi wa jimbo
hilo.
Katibu huyo, alimwomba Mbatia ambaye pia ni Mbunge
wa Kuteuliwa, amwombe Jaji Warioba kwenda katika jimbo hilo kuendesha
kongamano kama alivyofanya katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam na wao
wako tayari kumgharimia.
“Leo tunayo nusu ya nauli (Sh200,000) akikubali
tuko tayari kuchangia na kujazia Sh200,000 nyingine na tunakukabidhi
shati la kitenge kama alilokuwa anavaa Mandela (Nelson) ili
ukamkabidhi,” alisema.
Pwila alisema wananchi wa Vunjo wanamchukulia Jaji Warioba kama Mandela wa Tanzania, ndiyo maana wamempatia shati hilo.
Jaji Warioba alipoulizwa kuhusu maombi hayo, alisema hajayapokea na hajui lolote.
Katika mkutano huo, pia wananchi walimkabidhi
Mbatia suti mpya ambayo wanataka aivae atakapokwenda bungeni kuapishwa
akiwa mbunge wa jimbo hilo.
Mbatia awasha moto
Kwa upande wake, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti
mwenza wa Ukawa, alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza masuala
aliyokubaliana na viongozi wa vyama vya siasa kupitia Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) mwaka jana
- Mwananchi
إرسال تعليق