Serikali
imezuia watendaji wote wa Msajili wa Hazina, kuingia katika bodi yoyote
ya mashirika ya umma kuepuka mgongano wa maslahi.
Tafsiri
inayopendekezwa ya dhana hiyo ya Mgongano wa Maslahi katika bango
kitita hilo, imetajwa kuwa ni hali inayojitokeza wakati kiongozi au
mtumishi wa umma, ambaye anayo maslahi katika jambo fulani,
anapotekeleza majukumu yake au kufanya uamuzi, na katika kufanya hivyo
anatumia nafasi hiyo kuendeleza maslahi yake binafsi au ya ndugu zake au
marafiki zake kinyume cha taratibu za kazi yake.
Waziri
wa Fedha, Saada Mkuya (pichani) alisema bungeni, kwamba wameshaanza
kuondoa watendaji hao katika bodi mbalimbali, ili kuhakikisha
wafanyakazi wa Msajili wa Hazina, ambaye ndiye mwenye hisa katika
mashirika yote ya umma, wanakuwa wasimamizi badala ya sehemu ya
mashirika wanayoyasimamia.
Alikuwa
akizungumzia taarifa ya Kamati ya Fedha za Serikali (PAC), iliyoonesha
upungufu uliojitokeza katika ukaguzi maalumu wa matumizi ya Serikali na
mashirika ya umma, ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Katika
ukaguzi huo, ilibainika kuwa Mamlaka hiyo ilitumia Sh bilioni 9.6 kwa
ajili ya vikao vya wafanyakazi na mamilioni mengine yalilipwa kwa ajili
ya posho za safari bila kibali cha Serikali.
Waziri
Mkuya alikubaliana na taarifa ya PAC, kwamba Mamlaka hiyo iliidhinisha
na kuanza kulipa malipo na viwango vipya vya posho ya safari ya kujikimu
kwa watumishi, bila ya kupata kibali cha Msajili wa Hazina.
“Kwa
mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina, mashirika yana wajibu wa kupata
kibali cha Hazina kabla ya kulipa mishahara na posho,”
“Sisi
Wizara ya Fedha, tumeshaamua rasmi kwamba watendaji wote wa Msajili wa
Hazina hawatakuwamo katika bodi zozote za shirika lolote hapa Tanzania,” alisema Waziri Mkuya.
Alisema
wamefanya hivyo kwa sababu kuruhusu wawemo kwenye bodi za mashirika,
kutasababisha mgongano wa maslahi, kwani mfanyakazi wa Hazina anatakiwa
kusimamia mashirika hayo.
Alifafanua
kuwa kama hali hiyo ya mfanyakazi wa Hazina kuwa mjumbe wa bodi za
mashirika ya umma itaachwa, badala ya mfanyakazi huyo kuwa msimamizi wa
mashirika hayo, atakuwa sehemu ya matatizo yanayotokea kwenye mashirika.
“Tunaanza kuwatoa rasmi wafanyakazi wote katika bodi za mashirika. Tunaanza sasa hivi,” alisisitiza.
Hatua
iliyochukuliwa na Waziri Mkuya, imelishinda Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ambalo tangu mwaka Aprili 2010, aliyekuwa Mkaguzi
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alitaka
wabunge waondolewe mara moja katika bodi za wakurugenzi kwa kuwa kuwapo
kwao katika bodi hizo, kunasababisha mgongano wa kimaslahi.
“Mwenendo huu ni kinyume na taratibu nzuri na ni kinyume na kanuni za utawala bora… wenzetu wanatucheka katika hili,”
alisema Utouh alipokuwa akizungumzia ripoti yake iliyoishia Juni 30,
2009 ya ukaguzi wa mashirika ya umma na taasisi nyinginezo za Serikali.
Alisema
wakati umefika kwa Serikali kutoa waraka ambao utazuia wabunge kuwa
wajumbe wa bodi za wakurugenzi za mashirika ya umma, ili wahoji vyema
mwenendo wa mashirika hayo.
Kutokana
na hali halisi ya kutokuwepo maadili ya kutosha ya viongozi, hata
Serikali imeliona na tangu mwaka jana ilishaanza kufanyia kazi
mapendekezo ya kuundwa kwa Sheria Mpya ya Mgongano wa Maslahi Miongoni
mwa Viongozi na Watumishi wa Umma.
Katika
mapendekezo hayo yanayofanyiwa kazi chini ya Tume ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, Sheria hiyo imetakiwa itoe tafsiri ya dhana ya
Mgongano wa Maslahi.
Bango
kitita la mapendekezo hayo, limebainisha kuwa mpaka sasa hakuna Sheria
inayotoa tafsiri ya dhana ya Mgongano wa Maslahi, hivyo kusababisha
baadhi ya viongozi na watumishi wa umma kuingia katika tatizo hilo, kwa
kukosa uelewa au kutumia mwanya wa ukosefu wa tafsiri hiyo kujinufaisha.
“Kukosekana
kwa tafsiri ya Mgongano wa Maslahi ni miongoni mwa sababu
zinazosababisha baadhi ya viongozi au watumishi wa umma kutafsiri
neno hilo kwa jinsi wanavyoona inafaa na hivyo kujinufaisha binafsi,” bango kitita hilo limeeleza.
إرسال تعليق