Alhaji Jumbe afarijika kutembelewa na viongozi wa CCM

Rais mstaafu wa Zanzibar, Alhaji  Aboud Jumbe Mwinyi (pichani)  amefarijika kwa namna ya kipekee baada ya kukutana na viongozi wa CCM wa  mkoa wa Dar es Salaam waliomtembelea nyumbani kwake, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mafanikio ya miaka 38 ya chama hicho.
Mzee Jumbe ambaye sasa ametimiza miaka 95, anaishi Kigamboni Mjimwema na alitumia fursa hiyo kutafakaria mambo ya kijamii na kisiasa pamoja na wana CCM ambao leo mkoani Dar es Salaam wanasherehekea mafanikio hayo yatakayofikia kilele Februari 5, 1977.

Msafara wa viongozi uliomtembelea uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, uliwajumuisha pia  wenyeviti wa CCM wa wilaya za   Ilala,  Kinondoni na Katibu wa Siasa na Uenezi wa Dar es Salaam  na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wa mkoa.

Jumbe aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Pili wa Rais wa Tanzania mwaka 1984, alijiuzulu katika Mkutano Mkuu wa CCM, Dodoma kwa madai ya kuvunja Muungano na kushinikiza uwapo wa Serikali ya Zanzibar.

Pamoja na kuwa Rais alishika wadhifa wa Mwenyekiti wa chama cha Afro Shiraz (ASP) ambacho baadaye kiliungana na  Tanganyika African Union (TANU) kuunda CCM mwaka 1977.

Kutokana na uzee, ugonjwa wa macho, kichwa na miguu viongozi hao walizungumza naye akiwa kitandani wakimsalimia na kujitambulisha  na pia wanahabari waliokuwa kwenye safari hiyo walipata fursa ya kumsalimia.

Akiwa kitandani  hapo huku akilitaja jina  la Mungu pamoja na kumsifu wakati wa mazungumzo na viongozi hao, alisema anaiombea Tanzania amani na upendo.

Hata hivyo, alikuwa anazungumza  kwa shida akisaidiwa na wasaidizi wake wawili walimsikiliza na kuwaeleza wageni kuwa  aliwashukuru kwa  kumtembelea.

“Mwenyezi Mungu awatangulie  ninawatakiwa kila la kheri, hali yangu kama mnavyoniona nina miaka 95  sioni hata  kusikia ni vigumu na pia sauti inanikimbia,” alisema na kuongeza:

“Mungu akujalieni nyinyi na wenzenu wote Watanzania amani, sauti inazidi kukimbia lakini Mungu ndiye anayejua zaidi,” alisema.

Awali, kabla ya Jumbe kuzungumza maneno hayo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, alimweleza kuwa, ujio huo kwake ni kwa sababu chama kinatambua mchango wake kuasisi na kuendeleza chama.

“Kama siyo mapenzi yako kwa CCM kisingeweza kuasisiwa, kwa sababu ya uzalendo uliona kuna haja ya Afro Shiraz na TANU vilivyokuwa na lengo kuungana na kuzaa CCM,”alisema.

 Alisema CCM itaendelea kumtambua, kumuenzi na kumdhamini hasa mchango wake alioutoa katika nchi. Mke wa tatu wa Jumbe, Zehaya Rashidi Mohamed,  alisema hali ya mume wao si mbaya na kwamba anasumbuliwa na tatizo la kichwa na uzee ambao kila baada ya miezi mitatu amekuwa akienda nchini India kwa uchunguzi wa afya.

Mke wa nne wa kiongozi huyo mstaafu, Fatma Mohamed Hassan, amewaomba Watanzania kumuombea dua na kwenda kumuona kwa kuwa hilo huwafariji, aliwashukuru  Rais Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Jaji mkuu mstaafu, Agustino Ramadhani.

Msaidizi Mkuu wa kiongozi huyo, Abuu Mbande, alisema kuwa licha ya Jumbe kusumbuliwa na magonjwa ya uzeeni, lakini akili inafanyakazi na ameandika vitabu mbali mbali vya dini.

Alimsifu kwa kuwashirikisha  mara kwa mara na kuwafundisha  historia ya CCM, ASP na uongozi wa marehemu Rais Aman Abeid Karume na Mwalimu Julius Nyerere.

“Sasa hivi alikuwa na hamu kubwa ya kuongea na viongozi wa chama kwa hiyo leo amefarijika sana kukutana nao,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post