Dar es Salaam. Siku tano baada ya kuzuiwa kufanya mkutano wa
hadhara kwa madai ya tishio la ugaidi, Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba jana alihutubia wananchi eneo la Manzese jijini Dar es
Salaam bila kuwapo kwa ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Mkutano wa jana wa Profesa Lipumba, ambaye
alijikuta kwenye matatizo na Jeshi la Polisi baada ya kupigwa, kutiwa
mbaroni na baadaye kufunguliwa mashtaka Jumanne iliyopita, jana
ulitawaliwa na amani na ulidumu kwa takriban saa mbili kwenye eneo hilo
la Manzese ambalo kwa kawaida huwa na utitiri wa watu.
Profesa Lipumba alikutwa na kadhia hiyo wakati
akielekea Zakhem, Mbagala ambako alidai kuwa alikuwa akienda kushawishi
wananchi watawanyike kwa amani baada ya Jeshi la Polisi kuzuia
maandamano na mkutano wa hadhara.
Katika tukio hilo, mwenyekiti huyo wa CUF
alikamatwa pamoja na wafuasi 32 na baadaye kufunguliwa mashtaka ya kula
njama, kufanya maandamano na kukusanyika bila ya kibali. Vitendo hivyo
vya polisi vilisababisha Bunge la Jamhuri ya Muungano kusitisha shughuli
zake na kuamua kujadili tukio hilo, bila ya kujali kuwa lilikuwa
likiingilia shughuli za mhimili mwingine wa nchi.
Katika mkutano wa jana, hakukuwa na polisi
waliovalia sare kama ilivyo kawaida kwenye mikutano ya hadhara ya
kisiasa, hasa ya vyama vikubwa vya upinzani, ambayo hulindwa na askari
wenye silaha na jana jukumu hilo lilifanywa na kikosi cha ulinzi cha
chama hicho cha Blue Guards.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kinondoni, Camillius Wambura alisema hafahamu kuhusu suala hilo kwa kuwa
yuko nje ya eneo lake la kazi.
“Hilo silijui kwani nipo nje ya Dar es Salaam
hivyo siwezi kulizungumzia,” alisema Kamanda Wambura, ambaye alieleza
kuwa yuko Dodoma ambako kulikuwa na mkutano wa maofisa waandamizi wa
Jeshi la Polisi uliomalizika jana.
Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya
alilieleza gazeti hili baada ya mkutano huo kuwa barua ya kuitaarifu
polisi kuhusu mkutano huo ilipelekwa Alhamisi na wakapata majibu ya
jeshi hilo siku iliyofuata, tofauti na ilivyokuwa kwenye mkutano wa
Jumanne ambao uliombewa kibali Januari 22, lakini inadaiwa majibu
yalitoka Januari 27 asubuhi.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias
Chikawe alilieleza Bunge kuwa CUF iliomba kibali Januari 26 ikitaka
kufanya maandamano na mkutano Januari 27 na kwamba walikutana na
viongozi wa mkoa wa chama hicho na kukubaliana kuyasimamisha.Akihutubia
wananchi jana, Profesa Lipumba alisema: “Kuna tatizo kubwa, kuna ombwe
la uongozi. Kama Serikali kupitia kwa Chikawe inadiriki kusema uongo
bungeni, ni hatari na mimi ninawaambia kuwa kila mwaka, tutaadhimisha
mauaji hayo yaliyotokea Zanzibar (Januari 26 na 27 mwaka 2001).”
“Chikawe kusema kwamba kama uamuzi wa polisi
haukuwa sahihi tungekata rufaa kwake, ni makosa kwani sisi tunaongozwa
na sheria ya vyama vya siasa hivyo hii ni ishara ya Serikali kuamua
kuendesha nchi kibabe jambo ambalo hatuwezi kulikubali.”
Profesa Lipumba, ambaye leo atafanya mkutano wa
hadhara Mtaa wa Kigogo-Mkwajuni jijini Dar es Salaam aliongeza kusema:
“Haya wanayoyafanya mwisho wake ni Oktoba mwaka huu kwani Ukawa
tukichukua nchi, tutahakikisha tunalifanyia marekebisho makubwa Jeshi la
Polisi ili lilinde watu na siyo kuwaua na kuwajeruhi wananchi.”
Profesa Lipumba akisema katika mkutano huo
uliokuwa na lengo la kuwahamasisha Watanzania kuipigia kura ya hapana
Katiba Inayopendekezwa, alisema mchakato ni mbovu na wananchi wajiandae
kuikataa.
- Mwananchi
Post a Comment