Dodoma. Kamati ya Nishati na Madini, imeiagiza
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kufanya ukokotoaji upya
wa bei ya mafuta ili kupunguza bei itakayompa ahueni mwananchi.
Hayo yalisemwa jana na Juma Njwayo alipokuwa
akisoma taarifa ya kamati hiyo ya utekelezaji wa shughuli zake kwa
kipindi cha Januari mwaka 2014 hadi Januari 2015.
Alisema kwa kufanya ukokotoaji upya bei ya mafuta katika Jiji la Dar es Salaam inaweza kufika Sh1,600 kwa lita.
“Ewura kupitia utaratibu wake wa M-One wauangalie
upya kwani unaumiza mlaji, kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta duniani
bei inaweza kushuka kwa mwezi,” alisema.
Njwayo alisema bei ya bidhaa ya mafuta duniani
imeshuka kwa asilimia 60 na kwamba Dar es Salaam imekuwa ikitumia
asilimia 60 ya mafuta yanayoagizwa hapa nchini.
Alisema kampuni zinauza mafuta lita moja Sh1,520,
lakini katika vituo vya kuuza rejareja Dar es Salaam bidhaa hiyo inauzwa
kwa Sh1,955 kwa lita moja
Vilevile, kamati hiyo inaishauri Serikali kwa
kushirikiana na wawekezaji binafsi ianze ujenzi wa bomba la mafuta
kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani ili kupunguza gharama za mafuta,
usalama wa usafirishaji pamoja na usalama wa barabara za nchini.
Kamati hiyo pia imeishauri Serikali kujenga uzio kuzunguka machimbo ya Tanzanite yaliyoko Mererani.
“Pamoja na hilo tunaishauri kuhakikisha inaachana
na mitambo ya kukodi ya kampuni za Songas-Gas, IPTL na Symbion kama
ilivyofanya kwa Aggreko na kununua mitambo yake ili kuiondolea (Shirika
la Umeme) Tanesco gharama kubwa ya kulipa gharama za umeme. Gharama zake
ni kubwa mno.”
Kamati yataka sheria ya fidia ibadilishwe
Wakati huohuo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu, imeitaka Serikali kutazama upya Sheria ya Fidia kwa sababu
utaratibu unaotumika kukokotoa fidia haukidhi viwango vya sasa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba alisema
hayo bungeni jana wakati akisoma taarifa ya kazi ya kamati hiyo kuanzia
Januari 2014 hadi Januari mwaka 2015.
إرسال تعليق