CCM haitaki mgombea wa kusafisha kwa dodoki

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema chama hicho hakitampitisha mgombea urais asiye na sifa na kuhangaika kumsafisha kwa dodoki ili atakate.
Amesema chama hicho kimeweka mfumo mzuri wa kupata mgombea mwenye sifa, msafi na salama ambaye kazi kubwa itakayokuwapo kwa CCM ni kumwombea kura tu na si kumsafisha.
Alisema CCM ina utaratibu imara ambao utatoa mgombea bora, huku akisisitiza kuwa utawashangaza wengi pale atakapopitishwa mgombea ambaye hakutarajiwa na wengi.
“Mwaka 1995 Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema ‘msinipe mgombea ambaye nikisimama naanza kumsafisha kwanza.’ Tutatafuta mgombea wa kumuombea kura,” Nape alisema jana wakati akizungumza na wahariri wa Magazeti ya Mwananchi na The Citizen alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini.
Kauli hiyo ya Nape imekuja siku chake baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuwataka wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu huku akisema: “Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu wa kupata rais wa awamu ya tano, utakuwa wa kihistoria.”
Nape alisema chama hicho kitatumia misingi yake ya asili ambayo itatoa mgombea ambaye hatatiliwa shaka na kusisitiza kwamba hakitayumbishwa na kelele za barabarani.
Alisema hata wale wanaotabiri kwamba majina (ya wagombea), yakikatwa wataondoka na chama kitapasuka, hawatafanikiwa... “hata kama mtu ataondoka yeye, mkewe na watoto bado CCM itabaki imara.  “Utaratibu wa CCM katika uteuzi haujawahi kuwa na ushawishi wala sababu kutoka nje ya mfumo wenyewe. Kelele na ushabiki ni mambo tu ya barabarani,” alisema.
Akitolea mfano utaratibu uliotumika kupata mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995, 2000 na 2010 alisema, “Mwaka 1995 magazeti mengi, yaliandika ‘eti Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu) naye achukua fomu’. Kwenye orodha ya magazeti Mkapa aliwekwa kama mtu wa nane, lakini akawa ndiye mgombea wa CCM na akashinda.”
Alisema mwaka 2000 visiwani Zanzibar, Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal alipigiwa kura 45 huku Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume akipata kura tisa, lakini baada ya majina yao kupelekwa katika vikao vya juu vya chama, Karume alipitishwa kugombea na akashinda.
“Mwaka 2010 watu wengi waliamini kuwa Dk Bilal hana mpinzani, lakini dakika za mwisho alipitishwa Dk Ali Mohammed Shein kuwa mgombea urais wa Zanzibar na akashinda,” alisema.
Alisema mifano hiyo inaonyesha kwamba taratibu ndani ya chama hicho haziyumbi wala kuyumbishwa na matukio mengine yaliyopo nje ya mfumo ambao kimejiwekea.
“CCM ni chama imara kina katiba, sheria, kanuni, taratibu na tamaduni zake. Bado tutaweza na tunaweza kutoa mgombea mzuri, mwenye sifa, mwadilifu na anayeweza kuwa rais na Mwenyekiti wa CCM,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post