Dar es Salaam. Ripoti iliyotolewa na Timu ya
Wanahabari wa Kimataifa wanaoandika Habari za Uchunguzi (ICIJ), imesema
Watanzania 99 wanamiliki Dola za Marekani 114 milioni (Sh193 bilioni)
kwenye akaunti za benki nchini Uswisi.
Ripoti hiyo inayoitwa SwissLeaks iliyotolewa
Marekani jana, imesheheni taarifa za Benki ya HSBC ya Uswisi na namna
watu maarufu wakiwamo wanasiasa, wanamichezo, viongozi wa dini na
wafanyabiashara walivyoficha mamilioni ya fedha na kufanikiwa kuzikwepa
mamlaka za mapato katika nchi zao.
Katika orodha hiyo, Tanzania inashika nafasi ya
100 duniani na ya pili Afrika Mashariki ikiwa nyuma ya Kenya inayoshika
nafasi ya 58 duniani kwa kuweka zaidi ya Sh950 bilioni.
Uganda imetajwa kushika nafasi ya tatu kwa nchi za
Afrika Mashariki na 105 duniani baada ya kubainika kuwa imehifadhi
Sh151 bilioni huku Burundi ikitajwa kuwa na Sh51 bilioni.
Misri ndiyo inayoongoza Afrika ikiwa na Dola za
Marekani 3.5 bilioni, Afrika Kusini (Dola 2 bilioni), Morocco (Dola 1.6
bilioni), Eritrea (Dola 699.6 milioni), Algeria (Dola 671.1 milioni),
Tunisia (554.2 milioni), Libya (Dola 522.9 milioni), Zimbabwe
(Dola272.2 milioni) na Nigeria Dola 266.6milioni.
Ingawa taarifa hiyo haikutaja majina ya watu wote
walioweka fedha Uswisi, imemtaja mfanyabiashara Shailesh Vithlani ambaye
anadaiwa kuwa dalali wakati Tanzania iliponunua rada kutoka kwa kampuni
ya BAE System kuwa ni miongoni mwao.
Watu wengine maarufu waliotajwa katika ripoti hiyo
ni bilionea wa kwanza Afrika, Aliko Dangote, mwanasiasa kutoka Kenya,
Johnson Muthama, Alejandro Andrade, Alvaro Noboa, Fernando Alonso na
Mfalme wa Jordan, Abdullah II.
“Kuna baadhi ya wateja wa benki hiyo walikuwa
wakitoa mamilioni ya fedha kwa kutumia noti chakavu,” inasema sehemu ya
ripoti hiyo.
ICIJ inasema imefanikiwa kunasa akaunti 2,007
zinazohusishwa na zaidi ya watu 100,000 kutoka nchi 200 na taarifa hizo
tayari zilikwisha sambazwa na Serikali ya Ufaransa mwaka 2010 kwenye
nchi husika.
“Nchi ambazo zilikwishapokea taarifa hizo ni
Marekani, Hispania, Italia, Ugiriki, Ujerumani, Uingereza, Ireland,
India, Ubelgiji na Argentina.
Namna taarifa zilivyopatikana
Makabrasha kuhusu taarifa za wateja wa Benki ya
HSBC yalifichuliwa kwa mara ya kwanza na mfanyakazi wa zamani wa benki
hiyo, Hervé Falciani baada ya kuamua kuzikabidhi kwa Serikali ya
Ufaransa mwaka 2008, kisha mamlaka ya mapato nchini humo ikaanza
kuzifanyia uchunguzi.
- Mwananchi
Post a Comment