UHAMISHAJI FEDHA: ‘Watanzania 99 wanamiliki Sh193 bil Uswisi’

Dar es Salaam. Ripoti iliyotolewa na Timu ya Wanahabari wa Kimataifa wanaoandika Habari za Uchunguzi (ICIJ), imesema Watanzania 99 wanamiliki Dola za Marekani 114 milioni (Sh193 bilioni) kwenye akaunti za benki nchini Uswisi.
Ripoti hiyo inayoitwa SwissLeaks iliyotolewa Marekani jana, imesheheni taarifa za  Benki ya HSBC ya Uswisi na namna watu maarufu wakiwamo wanasiasa, wanamichezo, viongozi wa dini na wafanyabiashara walivyoficha mamilioni ya fedha na kufanikiwa kuzikwepa mamlaka za mapato katika nchi zao.
Katika orodha hiyo, Tanzania inashika nafasi ya 100 duniani na ya pili Afrika Mashariki ikiwa nyuma ya Kenya inayoshika nafasi ya 58 duniani kwa kuweka zaidi ya Sh950 bilioni.
Uganda imetajwa kushika nafasi ya tatu kwa nchi za Afrika Mashariki na 105 duniani baada ya kubainika kuwa imehifadhi Sh151 bilioni huku Burundi ikitajwa kuwa na Sh51 bilioni.
Misri ndiyo inayoongoza Afrika ikiwa na Dola za Marekani 3.5 bilioni, Afrika Kusini (Dola 2 bilioni), Morocco (Dola 1.6 bilioni), Eritrea (Dola 699.6 milioni), Algeria (Dola 671.1 milioni), Tunisia (554.2 milioni), Libya (Dola 522.9 milioni),  Zimbabwe (Dola272.2 milioni) na Nigeria Dola 266.6milioni.
Ingawa taarifa hiyo haikutaja majina ya watu wote walioweka fedha Uswisi, imemtaja mfanyabiashara Shailesh Vithlani ambaye anadaiwa kuwa dalali wakati Tanzania iliponunua rada kutoka kwa kampuni ya BAE System kuwa ni miongoni mwao.
Watu wengine maarufu waliotajwa katika ripoti hiyo ni bilionea wa kwanza Afrika, Aliko Dangote, mwanasiasa kutoka Kenya, Johnson Muthama, Alejandro Andrade, Alvaro Noboa, Fernando Alonso na Mfalme wa Jordan, Abdullah II.
“Kuna baadhi ya wateja wa benki hiyo walikuwa wakitoa mamilioni ya fedha kwa kutumia noti chakavu,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
ICIJ inasema imefanikiwa kunasa akaunti 2,007 zinazohusishwa na zaidi ya watu 100,000 kutoka nchi 200 na taarifa hizo tayari zilikwisha sambazwa na Serikali ya Ufaransa mwaka 2010 kwenye nchi husika.
“Nchi ambazo zilikwishapokea taarifa hizo ni Marekani, Hispania, Italia, Ugiriki, Ujerumani, Uingereza, Ireland, India, Ubelgiji na Argentina.
Namna taarifa zilivyopatikana
Makabrasha kuhusu taarifa za wateja wa Benki ya HSBC yalifichuliwa kwa mara ya kwanza na mfanyakazi wa zamani wa benki hiyo, Hervé Falciani baada ya kuamua kuzikabidhi kwa Serikali ya Ufaransa mwaka 2008, kisha mamlaka ya mapato nchini humo ikaanza kuzifanyia uchunguzi.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم