Msijione wanyonge, Pengo awaambia watawa

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amelitahadhalisha kanisa hilo kwamba ni hatari endapo mapadri watawa watashindwa kutekeleza wajibu wao kwa kigezo kwamba wenzao wa jimbo wanajitosheleza.
Kardinali Pengo akizungumza jana katika ibada ya kuzindua Mwaka wa Utawa katika Kituo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam iliyoongozwa na Askofu msaidizi wa Jimbo hilo, Titus Mdoe alisema mapadre watawa hawatakiwi kujiona wanyonge na watimize wajibu wao ipasavyo.
“Ni jambo ambalo kwa kipindi cha miaka 24 ya uaskofu wangu nimeona ni moja ya hatari kubwa...Mapadre watawa wana thamani, wana heshima na hawana sababu ya kujiona wanyonge na wa ziada, kazi yao itadumu mpaka Kristo atakaporudi,” alisema Kardinali Pengo
Aliongeza: “Wana jukumu la kujisikia wana jimbo kuliko hata mashirika yao, wao ni sehemu muhimu kwa kanisa na kanisa au jimbo ambalo haliwatambui hilo siyo Kanisa Katoliki.”
Kardinali Pengo alisema: “Kazi ya watawa wanawake inaonekana zaidi kuliko watawa wanaume, watawa wanaume inawawia vigumu kuonyesha utawa wao kutokana na muda, hatupendi iwe sababu ya muda na kila mmoja atimize wajibu wake.”
Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Padilla alisema: “Tutumie mwaka huu kutafakari maisha yetu ya utawa, je, tunaishi kwa ajili ya jamii, tunaishi kwa ajili ya nani, lakini pia tuziombee familia na nchi ya Tanzania ili iendelee kuwa na amani.”
Mwenyekiti wa Watawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Sista Honoratha Tesha alisema: “Baada ya kuwapo kwa mwaka wa imani, Mwaka wa Familia na leo hii Mwaka wa Watawa unazinduliwa, ni jambo jema ambalo ni fursa kwetu kutafakari maisha yetu.”

Post a Comment

Previous Post Next Post