Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki
Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo
amelitahadhalisha kanisa hilo kwamba ni hatari endapo mapadri watawa
watashindwa kutekeleza wajibu wao kwa kigezo kwamba wenzao wa jimbo
wanajitosheleza.
Kardinali Pengo akizungumza jana katika ibada ya
kuzindua Mwaka wa Utawa katika Kituo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam
iliyoongozwa na Askofu msaidizi wa Jimbo hilo, Titus Mdoe alisema
mapadre watawa hawatakiwi kujiona wanyonge na watimize wajibu wao
ipasavyo.
“Ni jambo ambalo kwa kipindi cha miaka 24 ya
uaskofu wangu nimeona ni moja ya hatari kubwa...Mapadre watawa wana
thamani, wana heshima na hawana sababu ya kujiona wanyonge na wa ziada,
kazi yao itadumu mpaka Kristo atakaporudi,” alisema Kardinali Pengo
Aliongeza: “Wana jukumu la kujisikia wana jimbo
kuliko hata mashirika yao, wao ni sehemu muhimu kwa kanisa na kanisa au
jimbo ambalo haliwatambui hilo siyo Kanisa Katoliki.”
Kardinali Pengo alisema: “Kazi ya watawa wanawake
inaonekana zaidi kuliko watawa wanaume, watawa wanaume inawawia vigumu
kuonyesha utawa wao kutokana na muda, hatupendi iwe sababu ya muda na
kila mmoja atimize wajibu wake.”
Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Mkuu
Francisco Padilla alisema: “Tutumie mwaka huu kutafakari maisha yetu ya
utawa, je, tunaishi kwa ajili ya jamii, tunaishi kwa ajili ya nani,
lakini pia tuziombee familia na nchi ya Tanzania ili iendelee kuwa na
amani.”
Mwenyekiti wa Watawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Sista Honoratha Tesha alisema: “Baada ya kuwapo kwa mwaka wa imani,
Mwaka wa Familia na leo hii Mwaka wa Watawa unazinduliwa, ni jambo jema
ambalo ni fursa kwetu kutafakari maisha yetu.”
إرسال تعليق