Kilimanjaro. Waganga wa jadi wanaotumia viungo
vya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) ikiwa ni sehemu ya tiba,
wametakiwa kutofanya hivyo kwa kuwa huo ni ukatili dhidi ya binadamu.
Mwenyekiti wa Chama cha Waganga na Wakunga wa Tiba
Asili Kilimanjaro (Chawatiata), Hasani Kabelo alisema hayo kwenye
mkutano wa mwaka wa chama hicho.
Kabelo alisema wanasiasa na wananchi wanatakiwa
kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria wanaojihusisha na matukio ya
kikatili kwa albino.
Kabelo alisema ili kukomesha unyanyasaji dhidi ya
albino, ni lazima jamii ielimishwe kurejea katika imani za dini
zinazosisitiza kuthaminiana bila kujali hali na tofauti za kimaumbile.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi
Mkuu, albino wanawindwa, hivyo ni jukumu la kila mmoja makini ili
kuepuka mauaji dhidi yao.
Katibu wa chama hicho, Fadhila Mohamed aliwataka
waganga na wakunga wa tiba asili kujisajili kwenye chama hicho
kinachotambulika.
Alisema kuna baadhi ya waganga wapo kwa masilahi yao binafsi kwa kupiga ramli na kuwadanganya watu.
Alisema hao ndiyo wanaosababisha waganga waonekane
wabaya mbele ya jamii Pia, alisema kuwa kuna waganga wanaotoka mikoa ya
jirani wanafikia nyumba za wageni na kufanya kazi za uganga kinyemela
kisha wanaondoka.
Aliishauri Serikali kuwakamata waganga hao kwa kuwa wengi wao ni matapeli.
Jumla ya waganga na wakunga wapatao 50 walihudhuria mkutano huo.
إرسال تعليق