Waziri asema wananchi hawana imani na polisi

Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed amesema wananchi hawana imani tena na Jeshi la Polisi kwa kuwa vitendo vya uhalifu vinafanyika, lakini hakuna wanaotiwa mbaroni.
Waziri Aboud alitoa kauli hiyo wakati wa kufunga mkutano wa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi uliokuwa ukifanyika mjini hapa, huku chombo hicho cha dola kikizidi kurushiwa lawama kutokana na ongezeko la uhalifu ambao umefikia hatua ya vituo vya polisi kuvamiwa na askari kuuawa na kuporwa silaha.
Jeshi hilo pia linalaumiwa kutokana na jinsi linavyoshindwa kushughulikia vurugu kwa weledi na hivyo kujikuta ikitumia nguvu nyingi zinazosababisha wananchi kuuawa na kujeruhiwa.
Waziri Aboud alibainisha kuwa wananchi wengi kwa sasa hawana imani tena na polisi kwa kuwa vitendo vya uhalifu vinafanyika lakini hakuna watuhumiwa wanaokamatwa na kutiwa mbaroni.
“Tabu inakuja pale uhalifu unapotokea na polisi kushindwa kuwapata wahalifu… wananchi wanapenda wahalifu wote watiwe mbaroni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Aboud pia aliitaka polisi kujiimarisha katika kusimamia mchakato wa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa utakaohitimishwa Aprili 30 na Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba.
“Katika uchaguzi kama huu, kutokea vurugu na kupotea kwa amani, nina imani polisi kuwa wana uwezo mkubwa wa kuzuia hali mbaya isitokee katika uchaguzi,” alisema.
Waziri Aboud pia alilitaka Jeshi la Polisi kubadilika na kuimarisha kikosi chake cha Intelijensia.
Alisema ikiwa kitengo hicho kitaimarika, itasaidia kuzuia uhalifu usitokee au hata kama uhalifu utatokea, itakuwa rahisi kuwapata wahusika. Aboud alisema ili polisi iende na wakati katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu nchini, ni lazima imarishe kitengo chake cha intelijensia ili kuzuia uhalifu ambavyo vinapangwa kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ikiwa polisi itaimarisha kikosi chake cha intelijensia, itakuwa imefaulu katika kukabiliana na uhalifu kwa kuwa itakuwa inafahamu mahali uhalifu unapopangwa kutokea na hata kuuzuia.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na Kura ya Maoni vinafanyika bila kuwapo na lepe la vurugu.
IGP Mangu alisema: “Polisi imeshajipanga kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote cha Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu ili kuwawezesha wananchi kufanya uchaguzi katika hali ya usalama, utulivu na amani.
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم