Mwanamke anayepambana na ukatili wa kijinsia

Ukiumwa na nyoka ukiona unyasi unashtuka ,ndivyo ilivyokuwa kwa Rhobi Pristiana Samwel (42)mratibu wa nyumba salama iliyo chini ya Kanisa la Anglikana Mugumu Serengeti Dayosisi ya Mara.
Mwanamke anayepambana kuhakikisha watoto wa kike wanasikilizwa na kuendelezwa kama ilivyokuwa kwa watoto wa kiume, ikiwa ni pamoja na kuwanusuru na ukatili wa kukeketwa na ndoa za utotoni ili wazee waweze kupata ng’ombe bila kuangalia wapi wanaenda, maisha yao yatakuwaje.
Mwanamke ambaye anasema mateso aliyoyapata akiwa mdogo bila kusikilizwa na wazazi wake, ndiyo yanamsukuma kupambana usiku na mchana ili yasiwakute watoto wa kike kwa kuwa madhara yake ni makubwa.
Nini msukumo wake
Anasema yeye alikeketwa kwa nguvu na wazazi wake na alipata madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuvuja damu nyingi, akapoteza fahamu kwa zaidi ya saa tatu. “Sherehe iligeuka majonzi kwa kuwa watu walianza kulia…pamoja na kutumia dawa za jadi hazikusaidia, ”anasema kwa uchungu.
Anasema tukio hilo likitanguliwa na mwanafunzi mwenzake aliyekeketwa awamu ya kwanza akafariki dunia na kisha maiti yake kutupwa ni vitu vinavyogusa moyo wake  na aliapa kuhakikisha anasimama imara kutetea watoto wakike ili kuwaepusha na madhara hayo.
Rhobi mtoto wa kwanza kati ya watoto 12 waliozaliwa kwa mama mmoja anasema kutokana na tukio hilo wazazi wake hawakuthubutu kukeketa wadogo zake 6 wa kike, hata majirani waliutumia mfano huo kupinga ukeketaji. Hali hiyo ilimsukuma kusoma kwa bidii ili aitumie elimu yake kusaidia wasichana waliokatika hatari ya kufanyiwa ukatili.
Aliwekewa vikwazo kusoma
Anabainisha kuwa pamoja na kufaulu kujiunga na shule ya sekondari akiwa msichana pekee kutoka Kijiji cha Matongo, Buhemba Wilaya ya Butiama, ndugu akiwemo babu yake walimtaka baba yake asimsomeshe ili apate ng’ombe wakitumia mfano wa  msichana pekee katika kijiji hicho alipata ujauzito akiwa kidato cha nne na kuonekana wasichana hawana faida.
“Nilisoma kwa bidii nikafaulu kujiunga na kidato cha tano,hata hivyo baba alikataa nikaenda ualimu, kisha nikajiunga na JKT… Niliporudi nyumbani nikakuta baba amepokea ng’ombe za mtu bila kunishirikisha, kwa kweli inauma kwa kuwa yanayoendelea sasa kuhusu ndoa za lazima na za utotoni nami yalinikuta,” anasisitiza.
Anasema pamoja na kukataa kuingia kwenye ndoa hiyo alitishiwa kutengwa na ndugu,mwisho akakubali kuolewa kwa sharti la kutokufanya sherehe na mme ambaye mpaka sasa wanaishi naye, hali hiyo ilimzidishia machungu kutafuta elimu zaidi ili aweze kufikia malengo ya  kuwasaidia watoto wa kike wanaofanyiwa ukatili.
“Pamoja na kuwa tulikuwa kijijini na mume wangu akifundisha, nilimshawishi tuhamishie biashara yetu mjini ili nipate fursa ya kusoma…alikubali bila kujua dhamira yangu,nikiwa nafanya biashara nikaanza kusoma chuo kikuu huria,nilipata msaada kutoka Woman Grant, nikahitimu shahada yangu ya biashara na utawala lakini sikuridhika nikaendelea kusoma shahada ya maendeleo ya jamii,” anasema
- Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم