Video Yatumika Kutoa Ushahidi katika Kesi ya Sheikh Ponda

UPANDE wa Mashikata kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda umewasilisha ushahidi muhimu wa mkanda wa video unaodaiwa kuonesha uhalisia wa tukio zima la kesi yake inayomkabili ya kutoa maneno ya uchochezi.
 
Mkanda huo wa video uliletwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo na kuoneshwa na shahidi wa tano wa kesi hiyo ambaye ni askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi kitengo maalumu cha uchunguzi wa picha, Aristides alieleza vigezo alivyovitumia kuitambua uhalisia wa video hiyo iliyochukuliwa Agosti 10 mwaka 2013.
 
Shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola alieleza mahakamani hapo kuwa video aliichunguza na kugundua kuwa ilichukuliwa katika eneo la tukio kupitia kamera ndogo aina ya JVC na kwamba baada ya kuichunguza aliandika hati na taarifa iliyoeleza vigezo alivyovitumia katika uchunguzi huo na yale aliyoyaona na kuyasikia katika video hiyo ambayo aliitoa mahakamani kama kielelezo.
 
Pamoja na ushahidi wake, lakini pia aliionesha video hiyo mahakamani hapo ambapo ilionesha tukio zima pamoja na maneno aliyoyatoa Shehe Ponda ambayo yanadaiwa kuwa yalikuwa ya uchochezi na yaliyoumiza imani ya dini nyingine.
 
Shahidi huyo pia alitoa kamera, DVD, hati na taarifa ya uchunguzi wa video hiyo kama kielelezo na kupokewa na mahakama hiyo.
 
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna msaidizi wa Polisi, Faustine Shilogile alikuwa shahidi wa nne katika kesi hiyo ambaye alieleza kuwa baada ya kupata taarifa za kutafutwa kwa Shehe Ponda kufuatia tuhuma mbalimbali zilizomkabili yeye kama kiongozi wa jeshi la polisi mkoa aliandaa askari kwa ajili ya kumkamata baada ya kufika mkoani Morogoro.
 
Shahidi huyo alidai kuwa taarifa hizo za kiintelijensia zilimhusisha Ponda na tuhuma za kumwagia tindikali wasichana wawili raia wa Uingereza huko Zanzibar na tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi jijini Dar es Salaam na kwamba tuhuma hizo alizipata wakati akiwa kwenye adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja ambapo pia alitakiwa kutofanya kosa lolote katika kipindi hicho cha mwaka mmoja.
 
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Juma Nasoro ulimuuliza maswali shahidi huyo, hata hivyo baadhi ya watu waliokuwepo mahakamani hapo walishindwa kuzuia vicheko vyao kutokana na aina ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa pamoja na majibu yaliyokuwa yakitolewa.
 
Wakili wa utetezi: “Je wewe ulijuaje kama Shehe Ponda alitoa maneno ya uchochezi?”
Shahidi: “Niliambiwa na OCD wangu kupitia radio call (simu ya upepo) kwani alikuwepo eneo la tukio.”
 
Wakili: “Je, unayajua mashitaka yanayomkabili Shehe Ponda?”
Shahidi: ”Siyafahamu kwa kuwa mimi sio muandaaji wa hati ya mashitaka.”
 
Wakili: “Ni askari wangapi uliwaandaa kumkamata Shehe Ponda?”
Shahidi: “Sikumbuki”
 
Wakili: “Je, hukuandaa askari 25 hadi 30 kwa ajili ya kumkamata Shehe Ponda? “
Shahidi: “Wewe ndio utakuwa umeeleza hiyo idadi”
 
Wakili: ”Je, askari wako walikuwa na silaha na kama walikuwa nazo tunaweza kuamini kuwa wao ndio waliomjeruhi Shehe Ponda?”
 Shahidi: “Ndiyo baadhi ya askari wangu walikuwa na silaha lakini siwezi kufahamu Shehe Ponda alijeruhiwa na nini.”
 
Wakili: “Je, unajua kama Msemaji wa Polisi, Advera Senso alitoa taarifa kuwa kuna askari alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi?” 
Shahidi: “Sina taarifa na kama alitoa taarifa hizo basi ni yeye na sio mimi.”
 
Wakili: “Je, kibali cha kufanya kongamano kilitolewa na nani na je uliambiwa kama Shehe Ponda ni mzungumzaji katika kongamano hilo?”
 
Shahidi: “Kibali kilitolewa kwa OCD na sikuwa na taarifa kama Shehe Ponda atakuwa mzungumzaji.”
 
Awali, upande wa mashtaka ulipanga kusikiliza mashahidi watano hata hivyo mahakama ilishindwa kuendelea kusikiliza mashahidi wengine watatu kutokana na muda kuwa umekwisha hivyo mashahidi hao watatu wataendelea kusikilizwa leo Februari 10 katika mahakama hiyo.
 
Hata hivyo, kesi imeendelea kuvuta hisia za wakazi wengi wa mkoa wa Morogoro na maeneo mengine huku hali ya ulinzi katika viwanja vya mahakama hiyo ikiwa imaimarishwa na kufikia hatua ya kuweka vifaa maalumu vya kuwakagua watu wanaoingia katika mahakama hiyo.

Post a Comment

أحدث أقدم