Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed amesema wananchi hawana
imani tena na Jeshi la Polisi kwa kuwa vitendo vya uhalifu vinafanyika,
lakini hakuna wanaotiwa mbaroni.
Waziri Aboud alitoa kauli hiyo wakati wa kufunga
mkutano wa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi uliokuwa ukifanyika mjini
hapa, huku chombo hicho cha dola kikizidi kurushiwa lawama kutokana na
ongezeko la uhalifu ambao umefikia hatua ya vituo vya polisi kuvamiwa na
askari kuuawa na kuporwa silaha.
Jeshi hilo pia linalaumiwa kutokana na jinsi
linavyoshindwa kushughulikia vurugu kwa weledi na hivyo kujikuta
ikitumia nguvu nyingi zinazosababisha wananchi kuuawa na kujeruhiwa.
Waziri Aboud alibainisha kuwa wananchi wengi kwa
sasa hawana imani tena na polisi kwa kuwa vitendo vya uhalifu
vinafanyika lakini hakuna watuhumiwa wanaokamatwa na kutiwa mbaroni.
“Tabu inakuja pale uhalifu unapotokea na polisi
kushindwa kuwapata wahalifu… wananchi wanapenda wahalifu wote watiwe
mbaroni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Aboud pia aliitaka polisi kujiimarisha katika
kusimamia mchakato wa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa
utakaohitimishwa Aprili 30 na Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba.
“Katika uchaguzi kama huu, kutokea vurugu na
kupotea kwa amani, nina imani polisi kuwa wana uwezo mkubwa wa kuzuia
hali mbaya isitokee katika uchaguzi,” alisema.
Waziri Aboud pia alilitaka Jeshi la Polisi kubadilika na kuimarisha kikosi chake cha Intelijensia.
Alisema ikiwa kitengo hicho kitaimarika, itasaidia
kuzuia uhalifu usitokee au hata kama uhalifu utatokea, itakuwa rahisi
kuwapata wahusika. Aboud alisema ili polisi iende na wakati katika
kukabiliana na vitendo vya uhalifu nchini, ni lazima imarishe kitengo
chake cha intelijensia ili kuzuia uhalifu ambavyo vinapangwa kufanyika
katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ikiwa polisi itaimarisha kikosi chake cha
intelijensia, itakuwa imefaulu katika kukabiliana na uhalifu kwa kuwa
itakuwa inafahamu mahali uhalifu unapopangwa kutokea na hata kuuzuia.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu
amesema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Rais,
Wabunge na Madiwani na Kura ya Maoni vinafanyika bila kuwapo na lepe la
vurugu.
IGP Mangu alisema: “Polisi imeshajipanga
kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi chote cha Kura ya Maoni na
Uchaguzi Mkuu ili kuwawezesha wananchi kufanya uchaguzi katika hali ya
usalama, utulivu na amani.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment