Kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani
Arusha,Kim Fute
---
Joto la ubunge katika jimbo la Arusha
mjini limezidi kupanda mara baada ya Kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani
Arusha,Kim Fute kutangaza rasmi kuwania ubunge katika jimbo hilo endapo akipewa
ridhaa na chama chake kugombea.
---
Mwandishi wetu Moses Mashalla, Anaandika kutoka Arusha.
Kim,amejitokeza kutangaza azma hiyo
ikiwa ni siku chache baada ya makada wengine wa CCM ambao ni Phillemon
Mollel,Victor Njau,Thomas Munisi,Deo Mtui,Godfrey Mwalusamba kutangaza nia
ya kuwania jimbo hilo linashikiliwa na mbunge wake,Godbless Lema ambaye tayari ametangaza kugombea tena.
Akizungumza na gazeti hili jijini
hapa,Fute alisema kuwa amesukumwa na dhamira ya kuwania ubunge katika jimbo
hilo mara baada ya kutathmini na kubaini ya kwamba jimbo hilo linakabiliwa na tatizo la ombwe la
uongozi.
Alisema kwamba amejipima vya kutosha
na kubaini ya kwamba ana sifa za kutosha za kuwawakilishi wakazi wa
jimbo la Arusha mjini ambao alidai kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa viongozi
bora wa kuwawakilisha.
Kada huyo alisisitiza kwamba miongoni
mwa mambo ambayo atakwenda kuyafanyia kazi pindi akifanikiwa kuwa mwakilishi wa
jimbo hilo ni pamoja na kushughulikia suala la usalama wa mji wa Arusha ambalo
alidai tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 mji huo umeandamwa na matukio
mbalimbali kama maandamano,vurugu na mambomu.
Alisema
kuwa mji wa Arusha ni mji wa
kimataifa na pia una fursa nyingi kama kitovu cha utalii hapa nchini na
duniani hivyo
atajikita kuhakikisha anasimamia hali ya kurejea kwa usalama ili
biashara hiyo iweze kufanyika kwa uwepesi kwa kuwa inachangia pato
kubwa la taifa.
“Arusha ni mji wa kimataifa na una
fursa nyingi kama biashara ya utalii ambayo inachangia pato kubwa la taifa lakini
usalama ni hafifu na unaharibu kwa kiasi kikubwa hivyo nitajikita kuhakikisha hali ya usalama inarejea”alisema
Kim
Hatahivyo,alibainisha kwamba mbali na
usalama pia atahakikisha anakutana na makundi mbalimbali ya viongozi wa dini
zote,waandishi wa habari pamoja na wadau wa maendeleo jijini hapa ili kuangalia
namna ya kuuweka mji wa Arusha katika hali ya utulivu.
“Tunahitaji mtu sahihi wa kuunganisha
siasa na uchumi mzuri, endapo nikifanikiwa kuwa mwakilishi nitahakikisha
ninakutana na makundi mbalimbali ili kujadili kwa kina changamoto zetu na
kubadili fikra na mtazamo kwa wakazi wa Arusha”alisisitiza Fute
إرسال تعليق