HII ni zaidi ya ukatili! Jiji la Tanga bado linazizima kufuatia
mauaji ya kutisha yanayodaiwa kufanywa na mwanaume aitwaye Khalfan
Hamad (46), dhidi ya mkewe, Mary Lucas (20) kwa kumchinja na panga kisa
kikidaiwa ni wivu wa mapenzi, Uwazi lina mkasa mzima.
Enzi za uhai wake, Mary Lucas (20) anaedaiwa kuchinjwa na mumewe.
Tukio hilo lililoacha simulizi ya kushangaza miongoni mwa wanandoa na
wanaotarajia kuingia, lilijiri Aprili 18, mwaka huu nyumbani kwa
mwanaume huyo, Mtaa wa Mapinduzi ‘A’ Kata ya Duga jijini hapa.
WANACHOKIJUA POLISI WA TANGA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Zuberi Mwombeki alitangaza kwa
waandishi wa habari kwamba, mauaji hayo yalitokea saa nne na nusu
asubuhi ya Aprili 18 mwaka huu.
Alisema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kati ya wawili
hao ambapo marehemu alimuomba mumewe pesa kiasi cha shilingi elfu kumi
aende saluni kutengeneza nywele lakini mwanaume akasema hana.
“Mwanaume hakumpa pesa marehemu lakini baadaye alimkuta amesuka na
ndipo ugomvi ulipoanzia hapo hadi kutokea mauaji hayo,” alieleza kamanda
huyo.
UWAZI LAANZA NA MAJIRANI
Mengi yamesemwa kufuatia mauaji hayo, lakini kama kawaida ya Gazeti
la Uwazi ni kufuatilia kwa kina ili kujua chanzo cha kila habari
inayotakiwa kuandikwa gazetini.
Ili kujua nini kilitokea kabla na baada ya mauaji hayo, Uwazi
lilizungumza na baadhi ya majirani wa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ambaye
kwa sasa anashikiliwa na polisi chini ya ulinzi mkali.
“Jamani sisi wenyewe tumeshtuka sana kwa kifo cha Mary, mimi
nimeongea naye akiwa anakwenda saluni na hata aliporudi. Kama angejua
ndiyo siku yake ya kufa naamini asingekwenda. Inauma sana!
“Mary alitoka saluni akiwa amependeza maana alitengenezwa nywele
vizuri sana. Mimi mwenyewe nilimsifia. Kufika nyumbani kwake, mzozo
ukaanza.
“Mumewe alitaka kujua alikotoa shilingi elfu kumi ya kuendea saluni
maana yeye hakumpa. Mzozo ulikwenda hadi mwanaume akachukua panga na
kumchinja. Naamini ni wivu,” alisema jirani mmoja.
KUMBE WALIKUWA NA HISTORIA YA UGOMVI
Jirani mwingine, Shaban Juma yeye alisema: “Hawa watu wameishi katika
hali ya kutoelewana na walikuwa wakigombana kila wakati, lakini
hatukujua kama litatokea hili kwani mara zote katika kugombana kwao,
mwanaume ndiye aliyekuwa akipigwa jambo ambalo liliwafanya watu wa
karibu yake kumshauri kuvunja uhusiano wao kulikoni aibu ya kupigwa na
mke.”
Jennifer Charles yeye pia ni jirani, alisema: “Siku ya tukio Mary
alimwomba mumewe hela ya kwenda kutengeneza nywele saluni lakini mume
hakuwa na pesa siku hiyo lakini baada ya kuondoka nyumbani, marehemu
naye alikwenda saluni.
“Baadaye mume aliporudi nyumbani hakumkuta Mary lakini mara alirudi
akiwa ametengenezwa nywele jambo lililomfanya bwana kuhisi kuwa fedha
hizo amehongwa na mwanaume mwingine tofauti na yeye na hivyo kuzuka
ugomvi huo.”
MUME ALITOKA NJE AKITAMBA KUUA
Baada ya Jennifer kumaliza kusimulia hayo, Juma Ally, naye ni
jirani, akaendeleza: “Hatukujua kilichoendelea katika mzozo wao, lakini
baadaye ukimya ulitawala. Muda mfupi mbele mume alitoka nje na kutuambia
kwamba ameshaua huko ndani kwani amechoka kupigwa na sasa amejibu
mapigo.
“Kwanza tulijua anatutania lakini tulivyoona kimya kimezidi tukaamua kuingia ndipo
tulipomkuta marehemu akiwa chini, akitoka damu nyingi. Tuliogopa kwa
kweli. Mary mrembo tunayemjua sisi, amelala chini na damu chapachapa.
“Alikuwa ana majeraha makubwa sehemu ya shingo na kichwani
yaliyotokana na kupigwa na panga. Ilionekana panga lilikuwa kali sana na
panga lenyewe lilikuwa pembeni yake. Ndipo tulipoamua kumkimbiza
Hospitali ya Mkoa, Bombo ambapo alipoteza maisha wakati madaktari
wakihangaika kuokoa uhai wake.”
ASINGEKUFA MKE
Naye, Fatuma Ramadhani alisema kutokana na ugomvi wa mara kwa mara
kati ya wawili hao na mwanaume kupigwa kila wakati, majirani waliamini
siku moja mume huyo ndiye angekuja kupata madhara hata kufa kutokana na
alivyokuwa akipigwa.
MTUHUMIWA KUPANDA MAHAKAMANI WAKATI WOWOTE
Kamanda Mwombeki alisema upelelezi unaendelea ili kuweza kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
Marehemu Mary alizikwa katika eneo la Mwakizaro jijini Tanga, siku ya pili baada ya tukio hilo la kuhuzunisha.
إرسال تعليق