Rais wa Msumbiji ataka wabunge waungane dhidi ya ufisadi, ugaidi

Dodoma. Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi amewataka wabunge kuwa kitu kimoja katika viti dhidi ya ufisadi na ugaidi na nchi yake itakuwa mstari wa mbele kushirikiana na Tanzania kupambana na maovu hayo.
Akizungumza wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano jana mjini Dodoma, Rais huyo aliyechaguliwa Januari 15, alitumia dakika 15 kuzungumzia masuala mbalimbali muhimu, alisisitiza zaidi kuhusu ufisadi na rushwa.
Kutokana na ujio huo, ratiba za shughuli za Bunge jana zilisitishwa kwa muda ili kumpa nafasi ya kuhutubia, huku muda wa mawaziri kuwasilisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka 2015/16 ukipunguzwa kutoka saa moja, hadi dakika 40 huku hotuba za kamati za Bunge na kambi ya upinzani zikiwasilishwa kwa dakika 20 badala ya 30.
“Tumekuja kujifunza demokrasia na namna ya kuendesha shughuli za Bunge katika masuala mbalimbali kama bajeti na kupinga ufisadi. Sasa hivi tumeweza kushiriki chaguzi za kidemokrasia na ujumbe wangu hapa unawakilisha makundi ya watu mbalimbali kisiasa,” alisema.
Aliongeza, “Serikali ya Msumbiji inafanya kazi pamoja na Bunge katika kupinga ufisadi. Tumeona tuje kujifunza kwa Bunge la Tanzania.”
Alisema wabunge wapo kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi,  hivyo jukumu kubwa walilonalo mbali na siasa, ni kufanya kazi ya kuendeleza uchumi, elimu, utalii na shughuli nyingine.
Huku akiishukuru Tanzania kwa kusaidia vita ya ukombozi kusini mwa Afrika na juhudi za ushiriki wake wa kuzuia vita barani Afrika, Rais Nyusi alisema Serikali yake itaendeleza uhusiano wa karibu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili.
“Tanzania ni nchi inayoendeshwa kizalendo na demokrasia, tumekuja kuona jinsi mnavyofanya kazi kwa uzalendo na mnavyoendesha nchi yenu kidemokrasia,” alisema.
Alisema katika kuimarisha uhusiano uliopo katika ya nchi mbili hizo, Serikali yake imefungua milango kwa Watanzania kwenda Msumbiji kufanya biashara.
Akitoa neno la shukrani, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimpongeza Rais Nyusi kwa kuweka historia ya kuwa mkuu wa kwanza wa nchi hiyo kulihutubia Bunge la Tanzania.
Kabla ya kulihutubia Bunge, Rais Nyusi akiwa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete  alitembelea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Post a Comment

أحدث أقدم