KAULI
mbili zinazotofautiana zilizotolewa na mawaziri wa Wizara ya Viwanda na
Biashara juu ya tuhuma zinazomkabili bosi wa Shirika la Viwango (TBS),
Charles Ekerege, zimewakera wabunge ambao wameitaka Serikali itoe tamko
ni kauli ya waziri upi ni ya kweli.
Hatua hiyo ilijitokeza jana
baada ya Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugora, kuomba Mwongozo wa Spika
kutokana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami na Naibu
wake, Lazaro Nyalandu kutofautiana juu ya uchunguzi dhidi ya bosi wa
TBS.
Wakati Nyalandu anajibu swali
juzi alisema uchunguzi wa CAG umekamilika na ameshawasilisha ripoti
serikalini, bosi wake, Dk. Chami alisema jana uchunguzi huo
haujakamilika na unaendelea kufanywa na CAG.
Ekerege anatuhumiwa na Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) na ile ya Hesabu za
Serikali (PAC) kuweka kampuni hewa za kukagua magari nje ya nchi na
hivyo kuingizia hasara ya Sh bilioni 30 ambazo zimeainishwa katika
ripoti ya CAG.
Baada ya Lugora kumaliza kuomba
mwongozo, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi aliyesema ni kweli majibu ya mawaziri hayo
hayafanani na Serikali imeliona hilo, na Ofisi ya Waziri Mkuu itakusanya
ushahidi wote juu ya jambo hilo na itatoa taarifa bungeni.
Lakini Mbunge wa Kigoma Mjini,
Peter Serukamba (CCM) alihoji kwa nini Serikali inashindwa kutoa majibu
ya uhakika juu ya suala hilo wakati wabunge wanachotaka kufahamu ni
kauli ipi yenye ukweli.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Kabwe Zitto (Chadema) alisema kamati yake anayoiongoza ya Mashirika ya
Umma iliunda kamati ndogo kushughulikia tuhuma zinazomkabili Ekerege na
tayari wameshawasilisha taarifa kwa spika ambaye anatakiwa aipeleke
Ofisi ya Waziri Mkuu ili walete taarifa ya utekelezaji bungeni.
Kwa upande wake, Naibu Spika Job
Ndugai alikiri kuwa jambo hilo ni la muda mrefu umefika wakati liishie
kwa kupatiwa ufumbuzi kwani linawapaka matope wabunge bila sababu za
msingi.
Chanzo - Habari Leo
|
إرسال تعليق