Urusi imezionya nchi za magharibi na za kiarabu kuacha kuwapa silaha waasi wa Syria. Akizungumza wakati wa ziara nchini Azerbaijan, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema kuunga mkono makundi yanayopigana na serikali ya Rais Bashar al Assad, kutasababisha miaka mingi ya umwagaji damu, lakini hakutayawezesha makundi hayo kuiangusha serikali. Urusi inaamini kuwa juhudi za mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Kofi Annan, ndio njia pekee kuilekea kwenye amani. Baada ya mkutano wa kile kinachojulikana kama ''Marafiki wa Syria'' uliofanyika mjini Istanbul, Uturuki, nchi za magharibi na za kiarabu zilisema zinaweza kutafakari uwezekano wa kuchukuwa hatua zaidi, kwa makusudi ya kuwalinda watu wa Syria. Urusi imejitenga mbali na nchi hizo.  Hayo yakiarifiwa, wanaharakati wamesema kuwa kwa uchache watu 80 wameuawa tangu Jumanne.  Tume ya maafisa wa Umoja wa Mataifa inaelekea mjini Damascus kujadili upelekwaji wa wachunguzi kulingana na mpango wa amani wa Kofi Annan.

Post a Comment

أحدث أقدم