Waziri Nagu azitaka benki kupunguza riba


 Waziri Nagu azitaka benki kupunguza riba


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji, Dk Mary Nagu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu, amezitaka benki nchini kurahisisha masharti ya mikopo kwa wateja wake sambamba na kupunguza viwango vya riba kwa wakopaji.

 Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua huduma ya Akiba Commercial Bank Mobile katika tawi la Kijitonyama inayotolewa na Akiba Commercial Bank (ACB).

 Dk. Nagu alitoa wito kwa uongozi wa ACB kuhakikisha kuwa utoaji wa huduma ya Akiba Commercial Bank Mobile unakidhi matarajio ya watanzania kwa ujumla.

 “Mteja anaponunua umeme (Luku) kupitia ACB Mobile, apate umeme kwa wakati alioutarajia na sio usumbufu wa kuambiwa kuwa hawezi kupata huduma hiyo kwa muda huo kutokana na visingizio mbalimbali, kama hitilafu ya mitambo,” alisema.
ACB Kijitonyama branch

 Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank, John Lwande, alisema kupitia huduma hiyo ya simu ya mkononi, mteja wa ACB atapata huduma ya kujua taarifa za akaunti yake, kulipia DSTV, maombi ya hundi na marejesho ya mikopo.

 Huduma nyingine ni kulipia ankara za maji (Dawasco), kujua taarifa ya akaunti yake, kuongeza muda wa maongezi wa simu yake ya mkononi, uhamishaji wa fedha kutoka akaunti moja kwenda nyingine,kupata taarifa mbalimbali za kibenki.

 Alisema ACB tangu ianzishwe 1997  kama benki ya kibiashara ikiwa na dhumuni la kumuwezesha mwananchi wa kipato cha chini kupata huduma za kibenki, mpaka sasa inawateja 23,000 na akaunti 190,000 za wateja.

 Lwande alisema ACB kwa sasa ina matawi 15 nchi nzima, matawi 13 Dar es Salaam, tawi moja Moshi na lingine Arusha, na hivi sasa wanatarajia kufungua tawi la 16 jijini Mwanza.

 Chanzo: Nipashe

Post a Comment

أحدث أقدم