
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimekataa kuthibitisha kama miongoni mwa mambo
yatakayojadiliwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec)
mwishoni mwa wiki, ni utekelezaji wa azimio la kikao kilichopita la
kuvuana magamba.
Alipoulizwa
kama suala hilo la utekelezaji wa kujivua gamba litakuwa moja ya ajenda
katika kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili kitakavyofanyika Jumamosi
wiki hii na kufuatiwa na vikao vya Kamati Kuu (CC) na Nec, Katibu wa
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alikataa kuthibitisha.
“Nyie (waandishi wa habari) mmeniuliza pale (kwenye mkutano wa
waandishi) kuhusu ajenda ambazo zitajadiliwa katika vikao nikawatajia,
sasa hayo mnayoyatafuta ni ya kwenu,” alisema Nape juzi akionyesha
kutofurahishwa na swali hilo.
Akizungumzia kuhusiana na maazimio yaliyofikiwa baada ya kumalizika kwa
vikao vya CC na Nec Novemba mwaka jana, Katibu Mkuu wa chama hicho,
Wilson Mukama, alisema Nec iliagiza CC na kamati za siasa za ngazi zote
za chama hicho kuanza mara moja mchakato huo.
“Halmashauri Kuu ya Taifa imeiagiza Kamati Kuu, pamoja na kamati za
siasa za ngazi zote za chama chetu kupitia kamati ya usalama na maadili
za ngazi zao zianze mara moja mchakato wa kutekeleza azimio hilo la
kufanya mageuzi ndani ya chama,” alisema Mukama.
Akisoma maazimio hayo yaliyopewa kichwa cha habari cha utekelezaji wa
maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu viongozi wanaotuhumiwa,
Mukama alisema, Nec imezitaka ngazi hizo za uongozi kutekeleza azimio
hilo kwa mujibu wa kanuni, taratibu zinazohusika za chama hicho.
“Vile vile zoezi hilo lifanyike bila kuchelewa. Baada ya kukamilika kwa
kazi hiyo, taarifa zipelekwe kwenye vikao vya kikatiba vya maamuzi vya
ngazi zinazohusika kwa hatua za utekelezaji,” alisema Mukama
aliyeongozana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Pius Msekwa na
Nnauye.
Kuhusu mwitikio, Mukama, alisema hadi sasa takribani miezi saba baada ya
azimio hilo kupitishwa, bado halijapata mwitikio wa kuridhisha kutoka
kwa viongozi wa ngazi yoyote ya CCM ambao ni walengwa wa azimio hilo.
Alisema bila shaka wakati sasa umefika kwa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika.
“Lakini utekelezaji wake utafanyika vipi ili haki ionekane kuwa
imetendeka? Jibu ni kwamba utekelezaji huo hauna budi ufanyike kwa
kufuata utaratibu uliowekwa na kanuni za CCM za Uongozi na Maadili,”
alisema.
Alisema kanuni hizo zinaelekeza hatua zinazopaswa kufuatwa katika
kudhibiti viongozi na wanachama wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kuwapatia wahusika nafasi ya kutoa utetezi wao.
Katika kikao cha Nec kilichofanyika Aprili mwaka jana, kiliazimia jumla
ya mazimio 27 ambayo yalilenga katika kukiimarisha chama hicho kwa
kukipa sura mpya itakayokuwa na mvuto zaidi kwa wanachama na pia kwa
wananchi kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mukama, Sektarieti ya Nec imekwisha kutengeneza mpango wa
utekelezaji wa maamuzi hayo yaliyopewa jina la kujivua gamba na mpango
huo umekwisha kuidhinishwa na Nec.
Katika kikao hicho cha Aprili mwaka jana, Nec iliazimia viongozi wote wa
CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime wenyewe na kuchukua
hatua wenyewe kwa maslahi ya chama na wasipofanya hivyo chama
kiwawajibishe bila kuchelewa.
Miongoni mwa waliokuwa walengwa wa ajenda hiyo ni Waziri Mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa. Lowassa aliguswa na kashfa ya kuipa
mkataba kwa njia ya upendeleo kampuni hewa ya Richmond ya Marekani ya
kufua umeme wa dharura.
Wengine ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
Chenge ambaye pia ni mjumbe wa Nec alikuwa anatuhumiwa kwa kashfa ya
ununuzi wa rada ya kijeshi kwa gharama ya juu ambayo Tanzania iliuziwa
na Uingereza wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Rostam Azizi ambaye pia alikuwa mjumbe wa Nec, alikuwa akituhumiwa
kutumia kampuni hewa ya Kagoda Agriculture Limited kuchota Sh. bilioni
40 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) pamoja na mahusiano yake na kampuni ya kufua umeme wa
dharura ya Dowans Tanzania Limited.
Hata hivyo, hadi sasa ni Rostam Aziz aliyetekeleza azimio hilo baada ya
kutangaza kujiuzuku nyadhifa zake zote Julai 13, mwaka 2011, akidai kuwa
amechoshwa na siasa uchwara ndani ya CCM pamoja na fitina.
Chenge amekwisha kusema mara kadhaa kwamba yeye si gamba, na kwamba hana
lolote baya alilofanya katika ununuzi wa rada na hata fedha zake
zilizokutwa katika akaunti visiwa vya Jersey hazina uhusiano wowote na
rada hiyo.
Alijitetea kuwa fedha hizo ni akiba ya familia yake inayotokana na kazi zake za uwakili.
Lowassa alizungumza katika Nec iliyopita akilaumu kuchafuliwa na
viongozi wa CCM kwa kutumia fedha za chama ilhali ikijulikana wazi kuwa
maamuzi yote ya mkataba wa Richmond mwenyekiti wa chama hicho, Rais
Kikwete alikuwa anajua.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment