BASATA YAWATAKA WASANII KUONGEZA THAMANI KATIKA KAZI ZAO
Na
Mwandishi Wetu
Huku kukiwa na juhudi za
kutambuliwa na kuthaminiwa kazi za wasanii ndani na nje ya nchi, Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kuongeza thamani kwenye kazi zao ili
kuzipa ubora zaidi.
Wito huo umetolewa mapema
wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari wa BASATA Godfrey
Lebejo wakati akihitimisha programu maalum iliyohusu Ubunifu, Utengenezaji na
Uongezaji thamani katika Kazi za Sanaa kupitia Jukwaa la Sanaa.
Alisema kuwa, ubora katika
Sanaa unapatikana pia kwa Wasanii kuangalia wenzao wanafanya nini na wao kupata
ubunifu mpya kwa kuongeza vionjo, uthamani na ubunifu binafsi katika kuifanya
kazi ya Sanaa kwanza kupendwa na baadaye kupewa thamani kubwa sokoni.
“Ni wazi Wasanii wetu
wanapaswa kuzingatia uongezaji uthamani kwenye kazi wanazozifanya. Kubuni kazi
ni suala moja lakini kuongeza uthamani katika kazi yako ili ivutie wengi na
kuuzika kwa thamani kubwa ni suala lingine la kuzingatia” alisistiza Lebejo.
Aliongeza kuwa, kwa sasa
kuna taarifa za Wakenya kununua kazi za Wasanii wetu kwa bei ya chini na
baadaye kuziongezea ubunifu, thamani na kuziuza nje kwa bei kubwa. Katika hili anasema, inatokana na
wasanii wetu kutokuzingatia falsafa hiyo ya ubunifu na uongezaji thamani wa
kazi zao.
“Tuna bahati ya kuwa na
malighafi nyingi sana, baadhi zimeoneshwa hapa lakini suala hapa ni sisi
kutumia ipasavyo malighafi hizo katika kubuni kazi zenye ubora na kuhakikisha
tunazipa thamani stahiki tunapozisafirisha nje” alizidi kusisitiza.
Awali akiendesha darasa
hilo maalum ambalo wiki hii lilikuwa mahsusi kwa ajili ya wasanii na
wajasiriamali wa Sanaa za mikono (Handcrafts), Haroun Sabili kutoka asasi ya
Musoma Handcraft alisema kuwa, Sanaa hizo zinahitaji ubunifu na umakini mkubwa
kwani kinyume chake ni kutokuvutia na kupoteza uthamani.
Alitoa wito kwa Wasanii
kujiunga katika vikundi na kuwa rasmi ili kuhakikisha kwanza,wanajenga
mazingira ya kuwezeshwa lakini pia kupata mafunzo mbalimbali ambayo yatawafanya
wazalishe kazi za Sanaa zenye ubora na thamani kubwa.
“Ni ngumu sana kuhudumia
msanii mmoja-mmoja lakini mkiwa kwenye umoja ni rahisi sana kupata fursa za
uwezeshaji hususan mafunzo katika kuongeza ubunifu na uthamani wa kazi zenu”
alishauri Haroun.
Katika programu hiyo
iliyohudhuriwa na wadau 72, elimu kuhusu ubunifu na uongezaji thamani kwenye
kazi za Sanaa ilitolewa sambamba na malighafi mbalimbali na jinsi zinavyoweza
kutumika kuzalisha kazi za mikono kuoneshwa.
Chanzo:- Full Shangwe

Post a Comment