JINSI YA KUTUMIA TWITTER ILI KUKUZA/KUTANGAZA BIASHARA YAKO
Makampuni mengi siku hizi yanatumia mtandao jamii wa Twitter kwa
minajili ya kutangaza biashara zao na hivyo kuongeza kiwango cha mauzo
yao kwa kupata au kuvutia wateja wengi zaidi. Ukikuta kampuni au
biashara haiutumii mtandao wa Twitter kwa kuwasiliana na wateja waliopo
na wa mbeleni,basi tambua kwamba kampuni hiyo haiendi na wakati. Yaweza
kuwa kwa makusudi au kwa kutokutambua tu faida zilizopo katika matumizi ya Twitter na hata mitandao mingine ya kijamii(Social Networks).
Pamoja na kuzidisha matumizi ya Twitter, yapo makampuni, makubwa kwa
madogo, ambayo bado wanashangaa kwamba inakuwaje watu
wanaowafuata(Followers) hawajaweza bado kubadilika na kuwa zaidi ya
wafuatiliaji tu na badala yake kuwa wanunuzi wa bidhaa au huduma.
Kwanini?
Ni wazi na ukweli kwamba Twitter ni sehemu nzuri ya kutangazia
biashara, matukio, kampeni za kusaidiana(kuchangishana fedha na mambo
kama hayo) achilia mbali sehemu nzuri ya kupashana habari,kuelimika na
kuburudisha kama ambavyo niliwahi kuandika katika post hii hapa.
Lakini kuandika tu (Tweets) haitoshi kukusaidia kukuza biashara kwa
maana ya kuongeza wateja na kipato. Unahitaji uelewa wa ndani zaidi juu
ya hadhira yako(audience), uwe na mpango thabiti wa mitandao jamii na
uwe na njia mahususi ya kupima mafanikio yako kupitia Twitter. Muhimu
zaidi unahitaji kujua jinsi gani na kwa namna gani utatumia Twitter
kabla hujaanza. Haya hapa ni mambo machache unayoweza kuzingatia;
Fanya Utafiti: Utafiti kuhusu soko lako(Market
Research) ni kitu cha lazima endapo unataka kuongeza nafasi za mafanikio
yako. Kuuliza maswali muhimu na yanayoeleweka kwa jamii ya Twitter ni
njia nzuri na rahisi ya kuelewa kwa undani kuhusu yaliyo muhimu kwa
wateja wako.Wanataka nini? Ni kitu gani wanakitazamia kutoka kwako au
kwa biashara yako.Ni aina gani za huduma ambazo wanazipendelea zaidi
kutoka katika biashara yako? Ni kitu au vitu gani vinavyochangia maamuzi
yao ya kutumia au kuchagua huduma au bidhaa kutoka kwako? Wanasemaje au
wana maoni gani kuhusu washindani wako wa biashara.
Ukitenga muda maalumu wa ku-tweet kwa minajili ya kupata undani wa
soko, bila shaka wateja wako, wa sasa na hata wa baadae, watakuchukulia
kama mtu ambaye unaingilika, unasikiliza na wanaweza wakajisikia huru
zaidi kutumia huduma au bidhaa kutoka kwako.Unakuwa karibu zaidi nao na
unawajali.
Kuwa na Mpango/Mbinu Maalumu: Biashara za aina zote,
zinahitaji kuwa na mpango maalumu wa kuwapata wateja, kubakia nao na
kujenga msingi imara wa wateja hao kitu ambacho ni muhimu sana kwa
maendeleo ya kweli ya biashara. Pamoja na njia zote za matangazo bado
neno la kuambiwa kutoka kinywani kwa mtu mwingine(word of mouth) lina
maana zaidi.Huo ni msingi.
Kwa hiyo kabla ya kuanza ku-tweet, jaribu kwanza kufanya utafiti
kuhusiana na jamii yako ya mtandaoni(online community) na jinsi gani
ujiingize au ushiriki katika jamii hiyo ukiwa miongoni mwao. Weka mpango
madhubuti wa jinsi utakavyokuwa ukituma au ku-post tweet zako, mara
ngapi utakuwa unafanya hivyo bila kusahau kuzingatia utakachokuwa
una-post.
Muhimu zaidi hapa ni kuzingatia je hiki ninacho-post kitaamsha hisia
za mtu kubofya(kama umeweka link kwa mfano), na je hii Tweet yangu
itaongeza uelewa kwa wateja wangu,wa sasa na wa baadae, juu ya aina au
huduma tunazotoa? Je, tweet hii itapelekea kuongezeka kwa masoko? Kwa
tweet hii,wateja zaidi watashawishika kutumia bidhaa au huduma
zinazotolewa na biashara yangu? Hayo ni baadhi ya maswali muhimu ya
kujiuliza
Hakikisha wateja wanaelewa undani wa Bidhaa/Huduma zako:
Kabla biashara yako haijaanza kutengeneza pesa, inahitaji kujenga kitu
kinachoitwa social media magnetism. Hii tunaweza kusema ni sumaku
ya/ndani ya mitandao jamii. Cha kwanza kufanya hapa ni kutumia watu
unaojuana nao au ambao wanajua kuhusu biashara yako(watu wako wa karibu
na watu unaokutana nao ana kwa ana wanafaa sana hapa) kwa ajili ya
kuitambulisha biashara yako na kuwashawishi wengine watue kwenye ukurasa
wako wa Twitter na hivyo wafuate brand yako.
Hapa ndipo panapokuwa na umuhimu wa kutumia jina linakubalika au
kutambulika kirahisi.Kuwa na logo na kuitumia hiyo logo katika kila kitu
kinachohusiana na biashara yako.Hakikisha kwamba ukurasa wako wa
Twitter,unatambulika hivyo kwanza.
Kisha wafuate(Follow) wataalamu au wazoefu wengine katika aina ya
biashara unayofanya. Yafuate makampuni mengine, wafuate washindani wako
wa kibiashara. Changia mawazo hususani kuhusu utaalamu ulionao ili
kuongeza heshima yako katika sekta. Kwa kufanya hivyo pia utakuwa
unaongeza imani miongoni mwa wateja wako.Watakukubali zaidi. Chagua aina
mahususi ya kushiriki katika mijadala mbalimbali kuhusiana na sekta au
aina yako ya biashara.Chagua “sauti” ambayo itakuwa ni rahisi kwa watu
kutambua.Ninaposema sauti ninamaanisha aina ya ujibuji maswali au
uchangiaji.
Shirikisha Wateja Wako: Miongoni mwa makosa makubwa
ambayo wamiliki wa biashara wanayoyafanya ni kutokuwa karibu na wateja
wao. Ninapoongelea kuwashirikisha wateja wako ninamaanisha kuwa karibu
nao.Kuwasikiliza kwa makini juu ya malalamiko,matarajio yao nk. Mitandao
jamii ni sehemu nzuri ya mazungumzo au mijadala. Kwa maana hiyo,
usiache kuwajibu wateja wako hususani katika zile Tweets ambazo
zinaitaja au kuhitaji majibu kutoka kwako. Anzisha mazungumzo na pia
shiriki mazungumzo. Katika mazungumzo hayo kuwa mkweli,muaminifu na utoe
habari au taarifa ambazo zimefanyiwa utafiti.Usikurupuke.
Wajali wafuasi wako: Kadiri wateja wanavyozidi kuwa
wengi,(hususani kwa makampuni au biashara ndogo ndogo) uwepo wako
mtandaoni unaweza kupungua kwa kisingizio cha kuwa “busy”.Usifanye hilo
kosa. Hakikisha kwamba unaendelea kuwepo mtandaoni.Hakikisha kwamba
unaendelea kufanya yote niliyoyataja hapo juu ikiwemo kushiriki
mijadala, kuuliza maswali ili kupata undani wa soko, kushughulikia
malalamiko nk. Biashara nyingi zimekuwa zikitumia Twitter kama chombo
cha kuhakikisha kwamba wateja wanaendelea kutumia bidhaa au huduma zao.
Tumia pia fursa hii kuwajulisha wateja wako kuhusiana na kile
kinachoendelea katika sehemu yako ya biashara. Kama utakuwa umefunga kwa
sababu moja au nyingine, waambie.Kama una punguzo la bei kwa bidhaa au
huduma,waambie. Washirikishe kwa kila namna.Kwa kufanya hivyo kwanza
hawatokusahau na pia wataona ni jinsi gani unavyowajali. Kila la kheri
katika biashara yako.
Jeff Msangi ni Mhariri Mkuu wa www.bongocelebrity.com. Unaweza kuwasiliana naye kupitia jeffmsangi at gmail.com au jeffmsangi at bongocelebrity.com

Post a Comment