BARAZA la Wadhamini la Chama Cha Mapinduzi (CCM) limeazimia
kutumia vitega uchumi vya chama hicho kujiongezea mapato ili kuachana na
utegemezi wa ruzuku na kupokea fedha chafu kutoka kwa wahisani na
marafiki zao.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za chama hicho
jijini Dar es Salaam, jana, Mwenyekiti wa baraza hilo, Peter Kisumo
alisema lengo ni kuongeza mapato ya CCM katika kukabiliana na vuguvugu
la mabadiliko ya kisiasa nchini.
“Siasa bila pesa mapambano hayawezekani… tumezoea kuona misaada ya
wazi kama kwa akina Sabodo na wanapeleka CHADEMA waziwazi, na wengine
wanaleta kwetu kwa siri, lakini ndani yake kuna pesa chafu,” alisema
kada huyo mkongwe wa CCM.
Alisema utegemezi wa ruzuku unayumbisha chama hicho na kubainisha
kwamba, wana dhamira ya kuingia ubia na kuanzisha makampuni huru
yatakayoongeza mapato ya chama hicho.
“Huu ni mpango mpya tumeiga kutoka kwa wenzetu Msumbiji, Afrika Kusini
na Namibia, tumeona vyama vyao vimefanikiwa kwa kuingia ubia na
makampuni kupitia vitega uchumi vyao.
“…Tutakuwa na kampuni huru zilizopo kisheria, tutaingia nao ubia,
lakini chama ‘eyes on, hands off’ tunahitaji fedha safi, hii maana yake
si kila fedha zinazokuja kutoka kwa marafiki na wahisani wetu ni chafu.
“Tunasema fedha chafu iwapo nyuma yake kuna shinikizo au sharti la
kumfanyia upendeleo kwenye jambo fulani, hizo ni fedha chafu… tuliwahi
kushindwa wakati ule, lakini sasa tumejipanga kushinda kwenye mfumo huu,
ninalosisitiza hapa ni fedha safi kutoka vyanzo huru,” alisisitiza.
Alisema baraza limeagizwa na Halmashauri Kuu (NEC) kuweka utaratibu
mpya wa kuimarisha mali za chama zenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 57
zinazohitaji usimamizi bora ili kuongeza mapato.
Aliwataja wajumbe wengine pamoja naye wanaounda baraza hilo kuwa, ni
Dogo Ali Mabruki, Edward Lowassa, Balozi George Lusinde, Balozi Sir
George Kahama, Anna Abdallah, Hadija Jabir Mohamed na Makame Mzee
Selemani.
Kuhusu madai ya kumuita Katibu Mkuu wa CCM, Willson Mukama kwamba ni
mzigo ndani ya chama, Kisumo alikanusha tuhuma hizo na kusema ni kauli
za kichonganishi.
“This is… this is… huu ni uongo utamfanya huyo katibu mkuu asifanye
kazi vizuri kwa sababu atajiona mzigo. Mimi sikusema wala sifikirii kama
nimesema hivyo, wala kuifikirisha akili yangu kumwona Mukama ni mzigo.
“Zamani kila mjumbe wa NEC alikuwa anatoka kwenye kikao na muafaka wa
yaliyozungumzwa kwenye kikao hicho, lakini siku hizi siri za vikao
zinavuja sasa sijui ni uhodari wa magazeti au kikulacho!.
“…Tunakutana kwa lengo la kuboresha yanayotekelezwa na Mukama kutokana
na kauli ya mwenyekiti wetu wa taifa, Rais Kikwete ile ya kujivua
gamba, nikasema kasi ya mageuzi haikuniridhisha na sio Mukama mzigo.
“Huyo aliyeyaleta kwenu sijui alikuwa na maana gani, kwa sababu ‘it
was closed door meeting’ (kilikuwa kikao cha ndani), nilitegemea kwenye
chama wajumbe tutoke na azimio sio kilichosemwa na mtu mmoja mmoja,”
alisema Kisumo.
Chanzo:- Tanzania daima
إرسال تعليق