CCM Yatoa Ufafanuzi Hotuba Ya Zitto Marekani

CCM Yatoa Ufafanuzi Hotuba Ya Zitto Marekani



KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA

Katika hotuba yake anadai kwamba mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea
hivi sasa unatokana na shinikizo la CHADEMA, Asasi za kiraia na
viongozi wa dini.

UFAFANUZI
Huo ni upotoshaji mkubwa na wa wazi kabisa unaolenga kufuta historia
sahihi ya mchakato wa uandikaji au upatikanaji wa Katiba Mpya
unaoendelea hivi sasa.

Ni jambo lililo dhahiri kabisa kwamba mchakato wa Katiba Mpya ni
utekelezaji wa hotuba ya Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) aliyoitoa katika salamu za kuaga mwaka 2010 kukaribisha mwaka
2011 na baadaye katika sherehe za Chama Cha Mapinduzi kutimiza miaka
34 Mjini Dodoma. Hili ndilo chimbuko halisi la hoja ya Katiba Mpya.

Akitoa maamuzi hayo alisema Katiba iliyopo sasa ni nzuri, imetuvusha
salama miaka hamsini iliyopita, tukiwa wamoja, imetujengea umoja wa
Kitaifa. Lakini katika kipindi hicho hicho kumetokea mabadiliko mengi
duniani na hapa nchini ya kisayansi, kiteknolojia, kitamaduni, kisiasa
n.k. Hakuna shaka kwamba sasa tunahitaji Katiba Mpya itakayotuvusha
miaka mingine 50 ijayo. Jambo hili Zitto Kabwe kalinukuu kwenye hotuba
yake anaposema kuwa:-

“Tanzania tunayoitaka kwa miaka mingine hamsini ….” Mantiki hii ya
miaka mingine 50 inatokana na hotuba ya Mhe. Dr. Jakaya M. Kikwete sio
yeye.


KUHUSU UBADHIRIFU SERIKALINI


Katika hotuba yake amedai kuwa CHADEMA ndio viongozi waliobeba dhamana
ya mpito huu, kutoka Serikali ya kibadhirifu isiyojali watu mpaka
Taifa lenye demokrasia iliyokomaa na lenye maendeleo na ustawi wa watu
wake. (Developmental Democratic State).

UFAFANUZI
Kwanza CHADEMA haina “dhamana” ya uongozi wa nchi, mwenye dhamana ya
uongozi wa nchi ni Chama Cha Mapinduzi ambacho kina Rais ambaye ni
Mkuu wa nchi, Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. CHADEMA
wanachokitafuta ni Mob leadership ambayo ni fujo “Anarchy or law
lessness” kitu ambacho huwezi kukidhibiti hata ukishika madaraka
(mfano ni Libya, Mali, Algeria n.k.).

Mob leadership ni fujo kwa sababu ina watu ambao hawana sera ya pamoja
hawana wajibu wa kisheria, hawana maslahi ya kijamii na kidini,
wanadai haki bila wajibu.

Dhamana ya kuwafikisha watu katika Serikali ya kidemokrasia imo
mikononi mwa Serikali iliyopo madarakani. Matamshi yanayotolewa na
baadhi ya viongozi wa CHADEMA yanaonyesha dhahiri kuwa hawathamini
demokrasia ya nchi, umoja wa kitaifa wala amani na utulivu.




Mfano:-

Tamko la Mhe. Joshua Nassari la kumzuia Rais, Mkuu wa Nchi,
asikanyage Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania.




Tamko la Mhe. Kabwe la kudai kuwa Wazanzibar wameporwa mafuta na gesi.
Hata kwenye uchaguzi mdogo wa Mbeya vijijini mwaka 2009 CHADEMA
ilitamka kwamba Mhe. Ali Hassan Mwinyi Rais Mstaafu asikanyage Mbeya.

Tamko la Mhe. Wenje kuwa Mwanza inajitosheleza kuwa nchi kwa
rasilimali zake na hivyo kupendekeza serikali za majimbo ili Mwanza
ijiendeshe yenyewe.

Matamko haya hayawezi kutamkwa na kiongozi mmoja wa CHADEMA bila
ridhaa ya Chama ama sivyo wangekuwa wanachukuliwa hatua na Chama chao.

Kwa kuwa matamshi haya ni uhaini, uchochezi na ufashisti (ANARCHY).
Kauli hizi zinaweza kupelekea machafuko katika nchi, mgawanyiko,
ubaguzi, fujo na umwagaji damu, mambo ambayo yatamwathiri kila raia wa
Tanzania bila kujali Chama chake cha kisiasa.

Kwa hiyo, Chama Cha Mapinduzi ambacho kina dhamana ya uongozi wa nchi
hii kinalaani matamshi hayo na kinawataka viongozi wa vyama vya siasa
waache kutoa matamshi ya hovyo na hatari kwa mstakabali wa Taifa letu.
Chama Cha Mapinduzi kinaitaka Serikali kufuatilia matamshi haya kwa
kina na itoe taarifa kwa wananchi.

KUHUSU WATANZANIA KUTAKA UONGOZI MPYA
Katika utangulizi wa hotuba yake amedai kuwa “watanzania kuliko wakati
mwingine wowote katika historia ya nchi yetu wameamka na kutaka
mabadiliko ya kisiasa na hasa kutaka kabisa uongozi mpya wa nchi
kutoka Chama kingine tofauti na Chama kinachoongoza hivi sasa.”

UFAFANUZI
Chama kinachoongoza hivi sasa ni Chama Cha Mapinduzi “CCM”
unapozungumza kauli kama hii lazima uangalie na hali halisi ya Chama
chenyewe kama Taasisi.

Kwanza, Chama Cha Mapinduzi kina wanachama hai wengi ambao ni
watanzania kuliko CHADEMA.

Pili, Chama Cha Mapinduzi kina mashabiki na wapenzi wastaarabu ambao
ni watanzania wengi kuliko CHADEMA.

Tatu, Chama Cha Mapinduzi katika mfumo wake hakijapata ombwe la
uongozi, kina uongozi katika ngazi za Shina, Tawi, Kata, Jimbo,
Wilaya, Mkoa na Taifa na hao wote ni watanzania. Na kama kuna Chama
chenye heshima ya kuwasemea watanzania wote kila kona ni CCM sio Chama
kingine chochote.

Nne, katika uchaguzi wa ndani ya Chama wa mwaka 2012, watanzania
wameendelea kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi ndani ya
CCM. Mpaka sasa Mashina yamekwishafanya uchaguzi kwa asilimia 97.56.
Hao walioshiriki uchaguzi huo wa mashina ni watanzania.

Tano, katika chaguzi ndogo za Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji CCM
imeendelea kuongoza na wanaopiga kura nao ni wantanzania.

Sita, Chama Cha Mapinduzi tangu 2007 kimefanikiwa kufungua matawi yake
nje ya nchi maeneo mbalimbali mfano India, Uingereza na Marekani. Hao
ni watanzania waishio katika ulimwengu wa kwanza na wanaamini kuwa CCM
bado ni imara na hata Mhe. Rais alipoalikwa juzi kuhudhuria mkutano wa
G8 alikutana na wanachama wa CCM Tawi la Marekani. Kitendo cha Mhe.
Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kualikwa G8 ni heshima kubwa
kwa Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa kuwa kigezo cha kumwalika
kilikuwa ni demokrasia, utawala bora, amani na utulivu nchini vigezo
ambavyo vinavutia wawekezaji kutoka nje.

Kwa hiyo, hoja ya Mhe. Zitto ni Batili (futile) kwa sababu anatazama
kwa macho ya ubinafsi kwa lengo la kugombea Urais mwaka 2015.

Uongozi mpya kabisa wa nchi ni upi? Kwa kuwa uongozi wa nchi yoyote
huru na ya kidemokrasia unapatikana kwa utaratibu wa uchaguzi wa
kawaida unaozingatia Katiba na Sheria za nchi katika mazingira ya
uhuru na uwazi na vyama vyote vinashiriki. Afafanue maana ya uongozi
mpya kabisa na namna utakavyopatikana huku akijua kabisa kwamba vyama
vyote vya siasa vitakuwa na haki ya kushiriki uchaguzi. Lazima utapata
uongozi mchanganyiko kama ilivyo hivi sasa katika mfumo huu wa vyama
vingi.

KUHUSU SERA YA MADINI YA 2009 NA SHERIA YA MADINI YA 2010

Katika hotuba yake amedai kuwa Tanzania haina sera ya Gesi asili na
kwamba, sheria ya madini ya mwaka 2010 imetokana na shinikizo la
CHADEMA na Asasi za kiraia.

UFAFANUZI
Chama Cha Mapinduzi katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo
inapatikana katika website ya CCM www.ccm.or.tz katika ibara ya 55 ya
ilani imeeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini kwa
kipindi cha 2005/2010, ambayo ni pamoja na kukamilika kwa sera ya
madini ya 2009 na kupitishwa kwa sheria ya madini ya mwaka 2010.

Mhe. Kabwe mwaka 2009 alikuwa wapi kutoa mchango wake?

Hoja hii ni ya CCM yeye na Chama chake wameidandia kwa malengo ya
kibinafsi na sio maslahi ya nchi.


SUALA LA URAIA WA NCHI MBILI (DUAL CITIZENSHIP)

Mhe. Zitto anadai kwamba suala la uraia wa nchi mbili ni sera ya
CHADEMA.

UFAFANUZI
Suala la uraia wa nchi mbili limekuwa ni sera ya Chama Cha Mapinduzi
na limesimamiwa na Serikali yake, hususan Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe.

Katika hotuba ya bajeti ya 2011/2012 iliyotolewa na Mhe. Bernard Membe
Bungeni katika Bunge la Nne kikao cha 31 cha tarehe 22 Julai, 2011
alisema:-

“Ni dhamira ya Wizara yangu kuona suala la uraia wa nchi mbili
linazinduliwa sanjari na Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.”

Watanzania mnapaswa kujua jinsi Zitto Kabwe anavyoiba hoja kwa manufaa
binafsi alipowadanganya watanzania waishio nchini Marekani na dunia
kwa ujumla akisema:-
“CHADEMA inataka suala hili lifikie mwisho kwenye mjadala wa Katiba.”

Huo ni uwongo mkubwa na uzushi, kwa kuwa dhamira hiyo ni ya Serikali
ya CCM na ilishawasilishwa na Waziri mwenye dhamana Bungeni na yeye
akiwepo.

6. HALI YA UCHUMI WA NCHI
Amedai kuwa uchumi unaokuwa hivi sasa sio uchumi wa watanzania bali ni
uchumi wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano
na ujenzi; hivyo kupelekea watanzania wengi zaidi ya 15m kuishi chini
ya Tshs. 500 kwa siku, kutokuwa na uhakika wa kula na kukabiliwa na
mfumuko wa bei.

UFAFANUZI
Kwanza, takwimu zake sio za kitafiti kwani hazionyeshi chanzo. Pili
hazina ulinganisho wa hali ya maisha ya wananchi wa nchi
zinazotuzunguka ili uchungu alionao moyoni uonekane waziwazi kama ni
kweli au ni uzushi.

Mhe. Kabwe amepotosha kwa makusudi ya kulinda maslahi binafsi ya Urais
wa 2015 kwa kuwa haiingii akilini kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama
takwimu hizo yeye hajazisoma.

Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2010
kilichotolewa na Wizara ya Fedha kukuwa kwa sekta ya kilimo
kumeongezeka kwa 4.2% mwaka 2010 tofauti na asilimia 3.2% mwaka 2009.
Lakini katika taarifa yake anadai kuwa uchumi wa vijijini ambako ndiko
kwenye kilimo umekuwa kwa asilimia moja tu (flat lining).

Katika uchambuzi wake wa hali ngumu ya uchumi na mfumuko wa bei kama
angelinganisha na nchi jirani angegundua kuwa mfumuko wa bei kwa
Tanzania upo chini zaidi kwa asilimia 19 ukilinganisha na nchi
zinazotuzunguka ambao mfumuko ni mkubwa zaidi mfano Ethiopia ni 30%.

Katika hali halisi ya maisha ya watanzania wa vijijini chakula chao
hakitokani na pesa, wanakula vitu vingi ambavyo haviingii kwenye
takwimu za uchumi mfano, kuku, mayai, maziwa, mihogo, viazi vitamu,
nyama n.k. Hivyo vinaliwa bila kuingia kwenye mzunguko wa soko ndio
maana hakuna mtanzania anayekufa njaa. Lakini nchi jirani wanakufa
njaa na wanakimbia nchi zao kwa njaa. Mfumuko wa bei ni tatizo la
Dunia nzima sio Tanzania peke yake.

Huyu ni mgombea Urais wa aina gani ambaye si mkweli kwa nchi yake,
hasomi takwimu na anaropoka mambo ya ndani ya nchi hovyo hovyo
duniani.

7. SUALA LA FURSA YA ELIMU
Katika hotuba yake ameeleza kuwa “leo mtoto wa maskini Tanzania hapati
elimu anayopata mtoto wa mwenye uwezo.” Na kwamba Tanzania ijiandae
kupokea bomu litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na elimu
wala ujuzi.”

UFAFANUZI
Huo ni uwongo na uzushi unaolenga kutetea maslahi binafsi. Kwa kuwa
katika uchambuzi wake amejikita kwenye shule binafsi na sio shule za
serikali ambazo zipo katika vijiji vyote Tanzania, vinatoa elimu huru,
sawa na bila ubaguzi.

Serikali ya Tanzania imetoa fursa ya Elimu kwa kila mtoto wa Tanzania
tangu awali. Mpaka imefikia wakati hata mabinti wa kazi za ndani
(house girls) hawapatikani wote wapo mashuleni.

Kuthibitisha hilo mnamo tarehe 20/9/2010 Tanzania ilipata tuzo ya
utekelezaji mzuri wa miradi ya Elimu katika ngazi za awali, elimu ya
msingi na sekondari kutoka umoja wa mataifa. Waziri Mkuu Mizengo Pinda
alipokea Tuzo hizo Mjini New York.

Hivi huyu Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA anakuwa wapi asiyaone haya
mpaka kwenda kuwadanganya watanzania waishio Marekani huko huko
ilikotolewa Tuzo?

Serikali ya CCM imejenga Vyuo vya kutosha vinavyozalisha wasomi wa
kutosha na hata bomu tunalojiandaa kulikabili ni la vijana wasomi
ambao hawana ajira na sio vijana wasio na elimu kama anavyodai yeye.

IMETOLEWA NA TAWI LA CCM MAKAO MAKUU
DODOMA
28/05/2012

Post a Comment

Previous Post Next Post