Chadema: Tatizo si mawaziri tu, bali mfumo
Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekosoa kusudio la kusuka upya
Baraza la Mawaziri unaotarajiwa kufanywa na Rais Jakaya Kikwete muda
wowote kuanzia sasa na kusema tatizo linalokabili nchi sasa ni mfumo
uliooza kwa maana hiyo mabadiliko hayo hayataleta tija. Kutokana na hali hiyo, wamesema uteuzi huo ni sawa na kubadili mtindo wa kusuka huku msusi akitumia nywele zile zile za zamani. Kauli
hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa wa Habari na
Uenezi wa Chadema, John Mnyika, wakati akisoma maazimio 16 ya Baraza Kuu
la Chama hicho lililokutana juzi.
Mnyika
alisema mwaka 2008, Rais Kikwete alivunja Baraza lake la Mawaziri na
kuteua watu wengine ambao hata hivyo, hawakuleta mabadiliko huku
waliokuwa wanatuhumiwa kwa ufisadi ambao waliachwa wakati huo mpaka sasa
hawajachukuliwa hatua hatua zozote za kisheria. Rais
Kikwete alilivunja baraza hilo baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward
Lowassa, kujiuzulu baada ya kuguswa na kashfa ya zabuni ya kufua umeme
wa dharura iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond ya Marekani, ambayo
baadaye iligundulikwa kuwa ilikuwa kampuni hewa. Sambamba
na Lowassa, mawaziri wengine waliojiuzulu Nazir Karamagi (Nishati na
Madini) na Dk. Ibrahim Msabaha (Ushirikiano wa Afrika Mashariki). “Aina
ya kusuka inaweza kubadilika, lakini nywele zitakazotumika zikawa
zilezile kama mnakumbuka mwaka 2008, Watanzania walitarajia mawaziri
waliokuwa wanatuhumiwa wangefikishwa katika vyombo vya sheria na
kushtakiwa, lakini mpaka leo bado tunawaona wanatesa mitaani,” alisema
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo.
Alifafanua
kuwa uozo ndani ya serikali haupo kwenye Baraza la Mawaziri pekee bali
ni mfumo mzima na kwamba unatakiwa kubadilishwa wote ili kuondoa vitendo
vya wizi wa mali za umma. Alisema
hata kama Rais Kikwete atateua Baraza la Mawaziri hakutakuwa na jipya
kwa kuwa atateua wabunge hao hao wa CCM ambayo wengi wao walipatikana
kwa njia za kifisadi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Mnyika
alisema kuna orodha ndefu ya mafisadi iliyowahi kutolewa hadharani na
Chadema mwaka 2007, lakini mpaka leo hakuna hatua zozote zilichukuliwa
dhidi yao. Aidha,
Mnyika alisema Baraza Kuu la Chadema limesema kitendo cha Kamati Kuu
(CC) ya CCM, kubariki kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri bila keleza hatua
za kuwachukuliwa mawaziri wanaotuhumiwa ni sawa kuendelea kulinda wezi
wa mali za umma.
HALI MBAYA YA UCHUMI
Kuhusu
hali ya uchumi nchini, Mnyika alisema Baraza Kuu la chama hicho
limesikitishwa na kuendelea kupanda kwa gharama za maisha miongoni mwa
wananchi sambamba na kuongezeka kiwango cha mfumko wa bei. Alisema
hatua hiyo imesababishwa na uongozi dhaifu wa serikali ya CCM, ambayo
imeshindwa kudhibiti matumizi ya mabaya ya fedha za serikali na idara
zake.
Mnyika
alisema Baraza Kuu la Chadema, lilisitiza kuwa hali ngumu ya uchumi
inayoikabili nchi ni kutokana na ukaidi wa serikali ya CCM wa kukataa
ushauri na mawazo mbadala ya katika kuongoza nchi. Alitoa
mfano kuwa mapato ya serikali kwa mwaka ni tilioni 13.4 wakati
makusanyo ya serikali ni Sh. tilioni 7.5 hatua ambayo inawafanya
wananchi kuwa na matumaini ya maisha bora wakati bajeti waliosomewa
bungeni haitekelezeki.
“Hali
hii ya maisha inaweza kuwa mbaya kutokana na utawala huu mbaya wa CCM
kwa kuwa chama hiki kimeshindwa kubuni na kusimamia sera sahihi katika
kulinda rasilimali za taifa yakiwemo madini, gesi asilia, mafuta,
misitu, bahari na ardhi,” alisema Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa
Wizara ya Nishati na Madini.
Alisema
Baraza Kuu la chama hicho, limewaagiza wabunge wa Chadema kuwahimiza
wananchi ili kuishinikiza serikali ya CCM ili kutimiza wajibu wake na
kwamba kikwazo kikubwa cha maendeleo ya Tanzania ni CCM ambayo
inaendesha serikali kwa mfumo wa rushwa na ufisadi.
Alisema
Baraza Kuu la Chadema, limewaagiza wabunge wake wote wa kuendelea
kuiwajibisha serikali na kuhakikisha katika bajeti ya serikali ijayo
wanapambana ili iwe ya kuwakwamua wananchi kiuchumi.
MAUAJI YA MAKADA WAKE
Katika
hatua nyingine, Chadema kimesema kinapanga kufungua mashitaka binasfi
dhidi ya serikali kwa kushindwa kuwalinda raia wake kufuatia vitendo vya
mauaji ya makada wa chama chao katika maeneo ya Arusha, Mbeya, Mwanza,
Mtwara na maeneo mengine ya nchi.
Chadema
kimesema kinataka kundwa chombo huru kwa ajili ya kuchunguza mauaji
hayo badala ya utaratibu wa sasa ambapo Jeshi la Polisi linahusika na
vitendo halafu linaunda kamati kwa ajili ya kuchunguza.
KATIBA MPYA
Mnyika
alisema Baraza Kuu la chama limewaagiza wabunge wake, kuzunguka nchi
nzima kufanya operesheni ya kuwaunganisha wananchi kuhusu masuala ya
Katiba mpya na uwajibikaji wa serikali.
UCHAGUZI NDANI YA CHAMA
Wakati
huo huo, Chadema kimesema mwaka huu kitafanya uchaguzi ndani ya chama
kuanzia ngazi ya chini mwaka huu hadi Oktoba mwakani kwa kuchagua
viongozi wa kitaifa. Mnyika
alisema chama kimeandaa kanuni maalum ili kudhibiti vitendo vya rushwa
katika uchaguzi huo kwa kuwa Chadema kinapinga vitendo hivyo na lazima
kiwe mstari wa mbele kuvipinga.
MISHAHARA KWA WAFANYAKAZI
Kuhusu
nyongeza za mishahara kwa wafanyakazi, Chadema kinaitaka serikali
kuangalia suala hilo ili kuhakikisha watumishi wake wanalipwa vizuri
kulingana na hali ya halisi ya maisha ilivyo kwa sasa. Baadhi
ya wabunge hivi karibuni walitia saini azimio la kuwasilisha hoja
bungeni ili ijadiliwe kwa lengo la kutaka kumung’oa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, ikiwa serikali ingeshindwa kuwawajibisha mawaziri wanane
waliotajwa kuhusika na vitendo vya ufisadi kupitia ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na ripoti za kamati za
kudumu za Bunge za Mashirika ya umma (POAC), Hesabu za Serikali (PAC) na
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).Hatua
ya kutaka kumwajibisha Pinda ilitokana na ripoti hizo kuwagusa baadhi
ya mawaziri na wabunge kuwataka wajiuzulu, lakini wakakataa.
Miongoni
mwa mawaziri waliotajwa katika ripoti hizo ni pamoja na Waziri wa
Fedha, Mustafa Mkulo, ambaye anadaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa
Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC). Alitajwa kuwa amepotea uaminifu na uadilifu kiasi cha kusema uongo bungeni ili kuficha maslahi binafsi katika ofisi za umma. Pia
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, alitajwa kuhusika
katika kumkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango la Taifa
(TBS), Charles Ekelege, kutokana na kusema uongo katika kazi ya ukaguzi
wa magari nje ya nchi.
Ekelege
anadaiwa kusema uongo kuwa kuna kampuni zimepewa kazi ya kukagua magari
yanayokuja nchini nje ya nchi, ambayo yanalipwa mamilioni ya fedha,
lakini kamati ya wabunge iliyokwenda nchi za Singapore na Hong Kong,
hawakukuta kampuni hizo. Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, naye anadaiwa kushindwa
kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kiasi cha kuruhusu nyumba yake
kukarabatiwa kwa mamilioni ya fedha.
Wengine
ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), George Mkuchika,
ambaye anadaiwa kushindwa kusimamia fedha katika halmashauri mbalimbali
nchini ambako ufisadi wa kuwango kikubwa umegundulika. Yupo
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, anayetuhumiwa kwa
kushindwa kusimamia sekta ya madini na umeme na kuweko kwa manunuzi
makubwa ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ambayo yameongezwa bei.
Pia
yumo Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ambaye atauhumiwa
kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika
katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa
wanyama hai nje ya nchi. Waziri
wa Uchukuzi, Omar Nundu, anatuhumiwa kuingilia mchakato wa kumpata
mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam;
Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
anadaiwa kushindwa kudhibiti ununuzi wa pembejeo na ulipaji wa fedha za
mdororo wa uchumi.
NA RICHARD MAKORE
CHANZO: NIPASHE
إرسال تعليق