Kim alia na washambuliaji Kili Taifa Stars

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Soka Tanzania, ‘Kilimanjaro Taifa Stars’ Mdenish Kim Poulsen, amesema licha ya kuwa ni mara yake ya kwanza kukinoa kikosi hicho ugonjwa unaokisumbua ni umaliziaji.
Akizungumza mara baada ya pambano la kirafiki kati ya Stars na Malawi ‘The Flames’ juzi Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lililomalizika kwa sare ya bila kufungana, Poulsen alisema, umaliziaji ndilo tatizo linalowakabili vijana wake.
Poulsen alisema endapo tatizo hilo litakwisha, ana imani kikosi chake kitafanya vema licha ya kuwa ni mara ya kwanza kukabidhiwa mzigo mkubwa kama huo na kuwa kwa sasa analifanyia kazi tatizo hilo kubwa.
“Nimetazama na nilikuwa makini sana, lakini tatizo ni umaliziaji, ukiangalia utafutaji kwa maana ya kiungo walijitahidi kufanya kazi yao kwa umakini zaidi, tatizo lilikuwa katika kumalizia na hasa hapo wapinzani wetu ndipo walipokuwa wakichukulia mpira,” alisema Poulsen.
Aidha Poulsen aliwapongeza vijana wake kwa jinsi ambavyo walijituma na kusema kuwa mapungufu ni sehemu ya mchezo na ndio sababu ya kuwa na mchezo wa kujipima nguvu kabla ya kuvaana na Ivory Coast kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayofanyika ugenini Juni 2 mwaka huu.
Naye Kocha wa The Flames, Kinnah Phiri, amelipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kuona umuhimu na kuwaomba kuja hapa nchini kucheza mchezo huo wa kirafiki na kuwa ni kipimo kizuri kwa timu yake.
Aliongeza kwa kuwapongeza wachezaji wa Stars, kwa uwezo wao na kusema kuwa hata kama kuna upungufu ni kidogo, kwa kuwa ni moja ya makosa katika soka kwani hata timu yake ina upungufu iliyouonyesha.
Katika hatua nyingine, pambano hilo kati ya Stars na The Flames, limeingiza sh 40,980,000, kutokana na mashabiki 10,767 waliokata tiketi kushuhudia.
Kili Taifa Stars imedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania kupitia bia yake ya Kilimanjaro kwa kiasi cha sh bil. 23.

Post a Comment

أحدث أقدم