MAHAKAMA YATENGUA UBUNGE WA MBUNGE WA SUMBAWANGA MJINI KWA TIKETI YA CCM


CHAMA cha Mapinduzi, kimepata pigo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga kutengua matokeo ya ubunge wa jimbo la Sumbawanga mjini yaliyompa ushindi mgombea wake Aeshi Hilal.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Betwell Mmila, alitengua matokeo ya mbunge huyo baada ya kubaini kuwapo kwa dosari katika ya vipengele kadhaa wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31, 2010.

Kati ya hoja 21 zilizowekewa pingamizi na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CHADEMA, Nobert Yamsebo, ni vipengele viwili pekee ambavyo mahakama hiyo imeridhia kuwa na dosari katika uchaguzi huo.

Katika hukumu hiyo ambayo ilichukua zaidi ya saa tatu kusomwa na jaji huyo, imevitaja vipengele ambavyo vilikuwa na dosari kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mazingira ya rushwa na kutokuwapo kwa mazingira huru katika kampeni kwenye baadhi ya maeneo yaliyo katika jimbo hilo.

Jaji huyo alibaini kuwa aliyekuwa mgombea wa CCM Aeshi Hilali alikwenda kwenye kikao cha ndani kilichodaiwa kuitishwa na viongozi wa CCM katika eneo la Shule ya Msingi Kantalamba Mazoezi, na kuwashawishi baadhi ya wapiga kura kwa kuwapa rushwa ya sh 15,000 watu sita walikuwa kwenye mkutano huo kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.

Eneo jingine ambalo lilitajwa kuwa na dosari ni kutokuwapo kwa mazingira huru kwa zoezi la kampeni kwenye vijiji vya Mtimbwa na Kisumba ambapo mgombea wa CHADEMA alizuiwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kufanya kampeni zake baada ya kumfanyia fujo.

Katika hoja ya msingi mlalamikaji aliiomba mahakama kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za uchaguzi.

Waliokuwa walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), msimamizi msaidizi na msimamizi mkuu wa uchaguzi ambao nao walidaiwa kukiuka sheria na kanuni za uchaguzi huo.

Katika kesi hiyo, mlalamikaji Yamsebo aliwakilishwa na kampuni ya kisheria ya Mkumbe Advocate and Company Ltd ya mkoani Mbeya ambapo kwa upande wa serikali uliwakilishwa na wanasheria wawili wa serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Shahidi.

Aiyekuwa mlalamikiwa aliwakilishwa na jopo la mawakili watatu, Juma Nassoro kutoka kampuni ya Nassoro Advocate; Abubakar Salim wa kampuni ya BLC Advocate; na Ileth Mawalla kutoka S. Mawalla, Law Consultant and Attorney ya mjini Sumbawanga.

Aidha hukumu ya mahakama hiyo imemtaka aliyekuwa mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini Aeshi Hilali kulipa gharama zote za kesi hiyo.

Pamoja na hukumu hiyo mahakama hiyo imetoa fursa kwa upande wa mlalamikiwa kukata rufaa iwapo atakuwa hajaridhika na hukumu iliyotolewa.

Hata hivyo, Wakili Nassoro aliyekuwa akimtetea Aeshi alisema kuwa wanakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo mara baada ya kutathmini mwenendo mzima wa kesi hiyo.

Kwa upande wake, aliyekuwa mlalamika wa kesi hiyo, Yamsebo alisema kilio cha wanyonge kimesikika na mahakama imetenda haki hali ambayo inawafanya wananchi kuendelea kuwa na imani na muhimili huo wa dola.

Katika uchaguzi huo uliotenguliwa, Aeish alishinda kwa kupata kura 17,328 wakati mgombea wa CHADEMA, Yamsebo, akipata kura 17,132.

Mji walipuka kwa shangwe
Mara baada ya hukumu hiyo, umati mkubwa wa watu uliofurika katika viwanja vya mahakama hiyo, wengi wao wakiaminika kuwa wanachama na mashabiki wa CHADEMA, ulilipuka kwa shangwe.

Idadi kubwa ya askari polisi waliokuwa wameletwa kwa wingi tangu asubuhi na kutanda kote mahakamani hapo, waliondoka kimyakimya mara baada ya kutolewa kwa hukumu, wakiwaacha mamia ya wananchi wakishangilia.

Shangwe hizo zilizagaa kwa kipindi kifupi na kuenea katika mji na vitongoji vingi vya mjini hapa kiasi cha kusababisha baadhi ya watu kuacha kwa muda shughuli zao na kuungana katika makundi ya watu waliokuwa wakipita mitaani wakionyesha alama ya V inayotumiwa na CHADEMA.

Mnyika apongeza
Ushindi huo umepongezwa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA John Mnyika ambaye alisema miongoni mwa kesi walizokuwa na matumamini nazo ni ya Sumbawangawa Mjini na kwamba haki imetendeka.

Alisema kuwa wanasubiri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza jimbo hilo kuwa wazi, ili wajiandae kwenda kuongeza mbunge mwingine wa chama hicho

Post a Comment

Previous Post Next Post