KLABU ya Yanga imeanza mkakati wa kuwasajili wachezaji kadhaa
kutoka kwa watani wao Simba, wakiwamo mabeki Juma Jabu, Juma Nyoso na
kiungo Uhuru Suleiman.
Kwa mujibu wa habari zilizoifikia Tanzania Daima na kuthibitishwa na
mmoja wa viongozi wa klabu hiyo anayehusika na usajili, wameamua
kuwafukuzia nyota hao kutokana na mikataba yao Simba kukaribia mwishoni.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa, kwa sasa wapo kwenye mazungumzo ya awali
na nyota hao, ingawa bado hawajafikia hatua ya mwisho kwa ajili ya
kusaini fomu za usajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu.
Yanga imekuwa na mkakati wa kusuka kikosi cha ushindi baada ya
kushindwa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu iliyofikia tamati Mei 6,
ikimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam FC.
“Kama unavyojua, Yanga imekuwa mbovu katika siku za hivi karibuni na
matokeo yake tulipoteza ubingwa wa Ligi Kuu Bara na nafasi ya kucheza
michuano ya kimataifa msimu ujao, sasa hatutaki kurudia makosa, tunataka
kufanya usajili mzuri kurejesha heshima yetu,” alisema kiongozi huyo.
Aliongeza, mbali ya hao, pia wana mpango wa kuimarisha safu ya
ushambuliaji kwa kusajili wawili kutoka nchini Rwanda ambao ni Meddie
Kegere na Olivier Karekezi, waliong’ara kwenye michuano ya Kombe la
Chalenji, lililofanyika Desemba, 2011, jijini Dar es Salaam.
Chini ya ufadhili wa Yusuf Manji aliyerejea kuokoa jahazi, Yanga
wamepania kusajili nyota mahiri na kuajiri kocha bora atakayeziba nafasi
ya Mserbia, Kostadin Papic, aliyemaliza mkataba wake mapema mwezi huu.
Post a Comment