Shehena kubwa ya silaha imenaswa Mashariki mwa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika shamba linalomilikiwa na mbabe
wa kivita wa zamani Jenerali Bosco Ntaganda.
Kwa mujibu wa jeshi, silaha nyingine zimenaswa
katika maeneo mengine mawili katika Mkoa wa Kivu ya Kaskazini, eneo
ambalo lilikumbwa na mapigano kati ya wanajeshi na waasi. Inadaiwa
silaha hizo zilikuwa za wapiganaji watiifu kwa Jenerali muasi Bosco
Ntaganda.
Tukio hili linajiri siku moja kabla
ya kukamilika kwa muda waliopewa waasi watiifu kwa Ntaganda
kujisalimisha au wakabiliwe kijeshi.
Kanali Innocent Gahizi ambaye ni kamanda mkuu wa
operesheni katika Mkoa wa Kivu ya Kaskazini ameiambia BBC, kuwa malori
matatu yaliyosheheni bunduki za rashasha na grunedi yamenaswa na jeshi
katika maeneo ya Singi, Mushake na Kirorirwe.
Gahizi ameongeza kuwa jeshi limetwaa uthibiti wa
maeneo yote mashariki mwa Masisi na limetangaza mpango wa kusitisha
mashambulio ili kuwapa waasi hao muda wa kujisalimisha kabla usiku wa
manane.
Jenerali Ntaganda anayejulikana kama Terminata
katika jina la utani, anasakwa na mahakama ya ICC kwa tuhumu za uhalifu
wa kivita.
Anatuhumiwa kuwasajili watoto kuwa wapiganaji wa
kundi la waasi la Thomas Lubanga, ambaye alikuwa mtu wa kwanza
kuhukumiwa na mahakama hiyo ya ICC mwezi Machi mwaka huu.
Jenerali Ntaganda ambaye amehusika na
mashambulio kadhaa nchini humo kwa miaka mingi, amekanusha madai ya
kuchochea uasi ndani ya jeshi, akitumia wanachama wa zamani wa kundi la
waasi wa CNDP.
Chanzo:- BBC Swahili
إرسال تعليق