CHADEMA yailiza tena CCM Arusha
Mzito mwingine Moshi ajiandaa kutimka
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekiliza tena
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuibomoa tena ngome yake baada ya
kuwachomoa wanachama takriban 400, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana
(UVCCM) Kata ya Enduleni, Cosmas Lakani.
Lakani ambaye ni mmoja wa viongozi machachari na aliyekuwa tegemeo
kubwa la umoja huo katika Wilaya ya Ngorongoro, alihama na wanachama 394
kutoka kata za Ngorongoro na Enduleni juzi na kufanya idadi ya Wana CCM
waliojiunga na CHADEMA ndani ya miezi miwili kufikia 3,481.
Wanachama hao walihamia CHADEMA wakati wa mikutano ya hadhara
iliyoongozwa na viongozi wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, akiwamo Mwenyekiti,
Samson Mwigamba, kwenye kata hizo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kadi ya CHADEMA, Lakani alisema
kuwa amechukua hatua hiyo kwa vile serikali ya CCM imeshindwa kutatua
kero za wananchi, na kibaya zaidi kuonekana kuwa wanathamini wanyama
walioko katika mbuga kuliko watu.
Alizidi kuishambulia serikali akidai imeshindwa kuwapatia hospitali,
ambapo kwa kipindi chote wamekuwa wakitegemea ile inayomilikiwa na
Kanisa Katoliki, na kuhoji kama kanisa hilo lisingejitolea wao wangepata
wapi huduma za afya.
Alidai kuwa amekuwa akizuiwa na uongozi wa juu kusema lolote kuhusiana na kero za wananchi, huku akitakiwa kufumba mdomo wake.
Baadhi ya wanachama hao walidai mbele ya viongozi wa CHADEMA Mkoa wa
Arusha kuwa serikali imeshindwa kuwasaidia hata kupata chakula cha
kutosha familia zao kama walivyowaahidi wakati wakiwazuia kuendesha
kilimo cha kujikimu ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA).
“CCM imetunyonya mpaka mwisho, walisema tuache kilimo cha kujikimu
watatupa chakula, lakini wanatupa chakula kidogo, wanaona mnyama
anathamani kubwa kuliko sisi tunaoishi Ngorongoro. Ndiyo maana
tunawaacha na CCM yao tumekuja CHADEMA itusaidie tukadai haki yetu,”
alisema Ndaito Sabore.
Mwana CCM mwingine mpya wa CHADEMA, Shuraa Sungai, alisema kuwa CCM
iliwadanganya kuwa itatoa ajira kwa vijana lakini inasikitisha mpaka
sasa vijana wao wanahitimu kidato cha nne na wengine vyuo vikuu lakini
wanarudi kijijini hapo baada ya kukosa kazi.
Mwenyeki wa CHADEMA wa mkoa, Mwigamba, aliwaeleza wananchi hao kuwa
CCM haijawahi kuwa na sera ya kuwasaidia wafugaji, jambo alilosema
limechangia kuibuka kwa mapigano kati ya wafugaji na wakulima mara kwa
mara.
Naye mratibu wa Baraza la Wanawake Mkoa wa Arusha, Cecilian Ndossi na
Ephata Nanyaro, walisema maisha ya wananchi hao yanasikitisha kwa vile
wanaishi katika umaskini wa kupindukia wakati wilaya yao ikiliingizia
taifa mamilioni ya fedha za kigeni kupitia utalii unaofanyika ndani ya
Hifadhi ya Ngorongoro.
“Serikali ya CCM inaonesha ni kiasi gani inathamini wanyama kuliko
wananchi wake, hata ukiangalia barabara zinazotumika kwa ajili ya utalii
zimetengenezwa vizuri lakini hizi zinazokuja huku kwa wananchi ni mbovu
na zinapitika kwa shida sana,” alisema Nanyaro.
“Mimi niko kwenye sekta ya utalii, Ngorongoro inaliingizia taifa
mamilioni ya dola, Serikali ya CCM inaacha kuwaletea huduma muhimu kama
hospitali, maji safi na barabara kwa sababu inajua nyie ni wateja wao,
wakataeni mje CHADEMA tushirikiane kudai haki hiyo mpaka kieleweke,”
alisema Ndossi.
Kada mwingine apasua vichwa viongozi wake huko Moshi, viongozi wa CCM
wa Wilaya ya Moshi Vijijini, wanaumiza vichwa kujaribu kumzuia kwa kila
mbinu kada wake maarufu, Ansi Mmasi, anayetajwa kuwa katika harakati za
kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA.
Mmasi ambaye amekuwa mpinzani mkubwa wa mbunge wa sasa wa Jimbo la
Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami, anatajwa kuwa miongoni mwa vigogo wa
CCM ambao wanatazamiwa kukihama chama hicho, ili kuwania nafasi hiyo
katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Moshi Vijijini, Gabriel
Masenga, alidai kuwa hajapata taarifa rasmi kutoka kwa Mmasi kama
anataka kuhama, lakini akakiri kusikia fununu hizo kupitia vyombo vya
habari.
Mwenyekiti huyo amedai kuwa wao hawawezi kupuuza habari hizo kwa kuwa
ni nzito, lakini akadai kuwa ikiwa itathibitika, itakilazimu CCM
kupambana vilivyo kuhakikisha kuwa kinaweka mtu katika uchaguzi mkuu
ujao anayekubalika katika jimbo ili lisiangukie mikononi mwa wapinzani.
Kumekuwapo na taarifa za kada huyo kukihama chama hicho na kujiunga na
CHADEMA kwa lengo la kuwania kiti cha ubunge katika uchaguzi mkuu ujao
mwaka 2012 huku Mmasi mwenyewe akisita kuweka bayana msimamo wake.
Taarifa hizo zimewagawa wanachama wa CCM katika wilaya hiyo katika
makundi mawili makubwa, huku wengi wao wakionya kuwa kuhama kwa Mmasi
kutasababisha mpasuko mkubwa na huenda akafuatwa na kundi kubwa la
wanachama.
Baadhi ya wanachama wa CCM waliliambia Tanzania Daima jana kuwa Mmasi
ana nguvu kubwa za ushawishi wa kisiasa katika Jimbo la Moshi Vijijini
licha ya kwamba aliangushwa katika kura za maoni katika uchaguzi mkuu
mwaka 2010.
Mmasi hakukiri wala kukanusha taarifa za kuhamia CHADEMA, badala yake aliomba apewe muda wa kutafakari.
Chanzo:- Tanzania Daima
إرسال تعليق