HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWA WANANCHI, TAREHE 01 Juni, 2012
Ndugu Wananchi,
Kama
ilivyo ada, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia
uhai na kutuwezesha kumaliza mwezi Mei salama. Kwa kutumia utaratibu
wetu wa kuzungumza kwa njia hii kila mwisho wa mwezi, leo nitazungumzia
mambo matatu.
Mkutano wa G-8
Jambo
la kwanza, ni suala la usalama wa chakula na lishe. Duniani,
inakadiriwa kuwa kuna watu milioni 925 wanaokabiliwa na njaa na lishe
duni. Kati ya hao Afrika ina watu milioni 239 ambao ni karibu theluthi
moja ya watu wote wenye tatizo la njaa na lishe duni kote duniani.
Nchi za Afrika zenye tatizo la njaa kiasi cha kuhitaji msaada wa
chakula kutoka nje ni 27. Kati ya hizo 11 zina matatizo makubwa zaidi.
Tanzania siyo miongoni mwa nchi hizo, hata hivyo bado hatujafikia
kiwango cha kujitosheleza kabisa. Hivi sasa tumefikia asilimia 95 na
kila mwaka yapo maeneo nchini yanayopata msaada wa chakula kutoka
Serikalini.
Mwaka
2009, katika mkutano wao wa L’Aquila, Italia, viongozi wa nchi nane
tajiri kuliko zote duniani waliamua kuchukua hatua ya kuzisaidia nchi
zinazoendelea duniani kukabiliana na tatizo la njaa na lishe duni.
Katika mkutano ule waliahidi kutoa dola za Marekani bilioni 22 kwa
ajili hiyo. Tanzania tunategemea kupata dola milioni 22.9.
Katika
mkutano wa nchi hizo maarufu kwa jina la G-8 uliofanyika Camp David,
Marekani tarehe 19 Mei, 2012, pamoja na mambo mengine walizungumzia
suala la usalama wa chakula na lishe barani Afrika. Nia yao ni
kuchangia katika juhudi zinazofanywa na mataifa ya Afrika zenye shabaha
ya kutokomeza matatizo hayo. Tofauti na walivyofanya L’Aquila, safari
hii waliamua kuchangia katika utekelezaji wa mipango na progamu za
kuendeleza kilimo katika nchi za Afrika hasa zile zinazolenga kujenga
usalama wa chakula na lishe.
Aidha,
waliamua kuwa wataanza na nchi tatu na kuendelea kuziongeza kila baada
ya muda fulani, badala ya kuanza na nchi zote mara moja. Hoja yao
kubwa ni kwamba, wanataka kukusanya nguvu zao kwa nchi hizo chache ili
kufanya kazi ambayo itakuwa na matokeo yanayoonekana katika kutokomeza
njaa na kuboresha lishe. Hawakupenda kusambaza nguvu zao kwa nchi
nyingi na kuishia kutokufanya kazi ya maana.
Ndugu wananchi;
Bahati
nzuri katika programu na mipango ya nchi iliyokubaliwa kwa awamu ya
kwanza ni Tanzania, Ethiopia na Ghana. Na, jambo la kufurahisha zaidi
ni kwamba mpango wetu wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa Kusini mwa
Tanzania ulichukuliwa kuwa ni wa mfano. Maoni hayo ya nchi za G-8 ndiyo
maoni ya WEF, Sekretariat ya NEPAD na Umoja wa Afrika, wote wameona
kuwa mpango wetu unafaa kuenezwa barani Afrika kama mkakati sahihi wa
kuendeleza kilimo, kujitosheleza kwa chakula na kupunguza umaskini.
Katika
Bara la Afrika mkakati huo sasa unaitwa Grow Africa Partnership na
tayari nchi saba zimeshajiunga nao. Nchi hizo ni Tanzania, Msumbiji,
Kenya, Rwanda, Ethiopia, Ghana na Burkina Faso.
Katika
mkutano wa Camp David, nchi za Marekani, Japani, Uingereza, Ujerumani,
Ufaransa na Urusi zimeahidi kuchangia nchi yetu katika juhudi zetu za
kuendeleza kilimo na hasa zile zenye lengo la kujitosheleza kwa chakula
na kuboresha lishe nchini. Ukichanganya na ahadi iliyotolewa na Umoja
wa Ulaya katika mkutano huo, kiasi cha dola za Marekani milioni 897
zimeahidiwa kutolewa kwa nchi yetu kati ya sasa na mwaka 2015.
Ndugu Wananchi;
Mwaka
2006 tulizindua Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo nchini maarufu
kwa kifupi kama ASDP. Kwa kirefu kwa lugha ya Kiingereza ni the
Agricultural Sector Development Programme. Programu hii ndiyo mwanzo wa
safari yetu ya uhakika ya kuleta mapinduzi ya kilimo nchini Tanzania.
Jambo la kwanza lililofanyika katika utayarishaji wa Programu hii ni
kutambua vikwazo vinavyozuia maendeleo ya kilimo nchini na kupendekeza
hatua za kuchukua za kuondosha vikwazo hivyo.
Mwaka
2008, katika tathmini iliyofanywa kwa ushirikiano wa Serikali na Sekta
Binafsi kwa uamuzi wa Baraza la Biashara Tanzania, ilidhihirika kwamba
sekta binafsi ambayo ni wadau muhimu, haijahusishwa vya kutosha katika
mikakati, mipango na programu za kuendeleza kilimo nchini. Kwa pamoja
ilikubaliwa kuwa kasoro hiyo iondolewe ili wadau wote washirikishwe,
yaani Serikali, wakulima wadogo, wakulima wakubwa na sekta binafsi.
Vilevile, sote tulikubaliana kutoa kipaumbele cha juu kwa maendeleo ya
kilimo. Kwa pamoja tuliafikiana kuwa mambo mengine yanaweza kusubiri
isipokuwa kilimo. Matokeo ya maelewano hayo ndiyo yaliyozaa mkakati na
kauli mbiu ya “Kilimo Kwanza”.
Ndugu Wananchi;
Tangu
wakati huo, sekta binafsi nchini imekuwa inahusishwa na kushirikishwa
kwa karibu katika utekelezajiwa ASDP na kuendeleza kilimo kwa jumla.
Kwa upande mmoja sekta binafsi imekuwa inahusishwa katika upatikanaji wa
zana na pembejeo za kisasa za kilimo kwa wakulima. Kwa ajili hiyo,
wenzetu wa sekta binafsi wamekuwa wanategemewa kuleta na kuuza
matrekta, mitambo na vifaa mbalimbali vya kilimo pamoja na mbegu,
mbolea, dawa za kuua wadudu waharibifu wa mazao na za kukinga na kutibu
maradhi ya mimea na mifugo. Hali kadhalika, wamekuwa wanajihusisha na
ununuzi na usindikaji wa mazao ya mkulima na kuongeza thamani.
Tunataka tuachane na kuendelea kuuza nje mazao ya kilimo kama malighafi
na kununua bidhaa zilizotengenezwa na mazao hayo.
Upande
mwingine tuliwategemea wenzetu wa sekta binafsi washiriki kulima
mashamba makubwa. Wasiache kazi ya kilimo kufanywa na wakulima wadogo
peke yao ambao uwezo wao si mkubwa wa kukabili matatizo ya kuongeza
tija. Nafurahi kwamba wito wangu huo waliupokea vizuri na baadhi yao
wameshaanza kufanya hivyo.
Ndugu Wananchi;
Swali
kubwa walilouliza ndugu zetu hao siku ile ya tarehe 2 – 3 Juni, 2009
pale Kunduchi Beach Hotel ni kuhusu upatikanaji wa ardhi. Niliwaeleza
kuwa upo utaratibu mzuri wa kuwapatia wakulima wakubwa ardhi ya kilimo
na ufugaji. Utaratibu wenyewe ni kwamba kila wilaya imetakiwa kutenga
ardhi kwa ajili ya wakulima wakubwa. Hilo likishafanyika, taarifa
hutolewa kwa Kituo cha Uwekezaji na kuingizwa katika kitu kinachoitwa
Benki ya Ardhi. Mwekezaji anapojitokeza, kulingana na aina ya kilimo
anachotaka kujihusisha nacho, hugawiwa ardhi hiyo. Ardhi hiyo ni ile
ambayo siyo inayotumiwa na wakulima wadogo. Katu hawanyang’anywi ardhi
wakulima wadogo ili kuwapa wakulima wakubwa. Hiyo siyo sera wala
madhumuni na malengo ya ASDP au Kilimo Kwanza.
Nalifafanua
hili kuondoa hofu iliyokuwepo na upotoshaji uliokuwa unafanywa
makusudi wa kuhusisha wakulima wakubwa na uporaji wa ardhi. Siyo
makusudio yake hata kidogo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka
2010 tukapanua wigo wa ushiriki wa sekta binafsi kwa kuihusisha sekta
binafsi ya kutoka nje ya nchi. Mwaka huo pia, tukaamua kuipa sekta
binafsi lengo maalum la kutekeleza nalo ni kushiriki katika kilimo cha
kuhakikisha kuwa nchi yetu inajitosheleza kwa chakula na kupata ziada
kubwa ya kuuza nje, kwa majirani zetu na kwingineko. Shabaha yetu hasa
ilikuwa ni kujitosheleza kwa vyakula vikuu vya mahindi, mchele na
sukari.
Aidha,
tuliamua pia kuwa, kwa kuanzia tuelekeze nguvu zetu kwenye mikoa ya
Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa na Morogoro kwa vile mikoa hiyo ndiyo
ghala la chakula la nchi yetu. Kwa vile mikoa hiyo ipo ukanda wa kusini
ndio maana ikaja kuitwa Southern Agriculture Growth Corridor of
Tanzania au SAGCOT. Tumeamua tukusanye nguvu za Serikali, wakulima,
sekta binafsi na washirika wetu wa maendeleo kuwekeza katika kuendeleza
kilimo katika mikoa hiyo.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji
wa mpango wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa SAGCOT una shabaha kuu
mbili: Kwanza kabisa mpango unalenga kuboresha kilimo cha wakulima
wadogo ili kitoke kuwa duni na cha kujikimu na kuwa cha kisasa na
kibiashara. Chini ya mpango huu wakulima wadogo watasaidiwa na
kuwezeshwa kupata na kutumia zana na pembejeo za kisasa za kilimo. Pia
watawezeshwa kupata mikopo kwa ajili ya kilimo na masoko ya uhakika na
yenye bei nzuri kwa mazao yao. Vile vile, huduma muhimu
zitaimarishwa. Hapa tunazungumzia maafisa ugani na miundombinu ya
umwagiliaji, barabara, umeme, maji safi na teknolojia ya habari na
mawasiliano.
Pili,
kwa pale inapowezekana kwa maana ya upatikanaji wa ardhi na aina ya
mazao, kuihusisha sekta binafsi katika kilimo. Tayari utekelezaji wa
mpango wa SAGCOT umeanza. Kamati ya Utendaji imeshaundwa na
Sekretariati yake imeshateuliwa. Aidha, Mfuko wa Kuchochea Uwekezaji
umeshaanzishwa na unaendelea kuchangiwa fedha.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji
wa malengo ya SAGCOT kwa kilimo cha mpunga na kuongeza uzalishaji wa
sukari yameanza kutekelezwa. Matayarisho yanaendelea kwa kilimo cha
mahindi na mazao mengine.
Mpango
huu utakapofanikiwa utakuwa na manufaa makubwa. Nchi yetu
itajitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada kubwa ya kuuza nje.
Inakadiriwa kuwa mapato yatokanayo na kilimo katika ukanda huu yatafikia
dola bilioni 1.2 kwa mwaka, watu 420,000 watapata ajira na watu
2,000,000 wataondokana na umaskini uliokithiri.
Uwekezaji
wake ni mkubwa na kwamba kiasi cha dola bilioni 3.4 kinahitajika kwa
kipindi cha miaka 20. Kwa ushirikiano uliopo baina ya Serikali, sekta
binafsi na wabia wetu wa maendeleo wakiwemo wa nchi za G-8, hayo yote
yanawezekana.
Ndugu Wananchi;
Tukijitosheleza
kwa chakula na kwa maana pana ya chakula chenye lishe bora tutakuwa
tumefanikiwa kupata ufumbuzi wa tatizo kubwa la ukosefu wa lishe bora
miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Wanaoathirika sana na tatizo hili ni
kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Ukosefu wa lishe bora huchangia asilimia 20 ya vifo vya kinamama
wajawazito nchini na theluthi moja ya watoto wa umri wa chini ya miaka
mitano. Aidha, asilimia 42 ya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano
wamedumaa na asilimia 16 wana uzito mdogo kulingana na umri wao na
asilimia 59 wana upungufu wa damu. Kwa kina mama wajawazito asilimia 41
wana matatizo ya upungufu wa damu. Hali hii sio nzuri hata kidogo
lazima tuibadili na tunaweza kufanya hivyo. Tunao mkakati wa kitaifa wa
kuboresha lishe ambao kwa sehemu kubwa utanufaika sana na kufanikiwa
kwa mkakati wa kujitosheleza kwa chakula.
Mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika
Ndugu Wananchi;
Jana
tarehe 31 Mei, 2012 nilishiriki katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano
wa 47 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Mkutano wa
38 wa Mfuko wa Maendeleo wa Afrika. Hii ni mara ya kwanza katika
historia ya Benki hii tangu ianzishwe mwaka 1964 kwa nchi yetu kuwa
mwenyeji wa mikutano hii inayofanyika kila mwaka. Ni heshima kubwa sana
kwa nchi yetu, nami kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote,
nimemshukuru sana Rais wa Benki hiyo, Dkt. Donald Kaberuka kwa ihsani
kubwa aliyoifanyia nchi yetu.
Kuwa
mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huu ni jambo lenye manufaa mengi
kwetu. Kwanza husaidia kuitangaza nchi yetu Barani Afrika na kwingineko
duniani. Pili, ni fursa nzuri ya kuzungumza na viongozi wa Benki
kuhusu mipango na miradi yetu ya maendeleo tunayohitaji msaada kutoka
Benki hiyo.
Na,
tatu, ni fursa nzuri ya watu wetu kufanya biashara. Mkutano huu
umeshirikisha watu 2,500 ambao wametoka nje ya Tanzania na wanajitegemea
kwa kila kitu. Wenye hoteli, migahawa, vyombo vya usafiri, huduma ya
simu, internet na nyinginezo watakuwa wamefanya biashara nzuri katika
wiki nzima kabla ya tarehe 28 Mei mkutano ulipoanza hadi 2 Juni, mkutano
utakapofungwa. Ni kutokana na manufaa kama haya, ndio maana huwa
tunahangaika kuvutia mikutano mikubwa kuja kufanyikia hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu zetu wa
Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu hao.
Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote. Naomba kuwepo
kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu. Miaka
miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la
kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha. Isitoshe
hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna
hiyo. Lakini sasa imewezekana. Naomba kila mmoja wetu aweke azimio
moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena. Nyota ya
Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele tugange
yajayo.
Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni
tena niwashukuru wenzetu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa mchango
mkubwa waliotoa na wanaoendelea kutoa kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
Kwa miaka mingi Benki hii imekuwa inatupatia mikopo na misaada muhimu
kwa maendeleo ya sekta mbalimbali nchini pamoja na zile za elimu, afya,
maji na miundombinu ya barabara, reli, umeme n.k.
Kwa
msaada wa Benki hii tunajenga barabara ya Namanga – Arusha, Minjingu –
Singida, Namtumbo – Tunduru, Iringa – Dodoma, Mayamaya – Babati, na
Tunduru – Mangaka – Mtambaswala. Miaka ya nyuma pia walituwezesha
kujenga barabara ya Mutukula – Muhutwe. Aidha, hivi sasa wanagharamia
upembuzi yakinifu na usanifu wa reli mpya tunayotaka kuijenga kutoka Dar
es Salaam hadi Rwanda na Burundi.
Matukio ya Uvunjifu wa Amani Zanzibar
Ndugu Wananchi;
Jambo
la tatu ninalotaka kuzungumza nanyi leo ni matukio ya wiki iliyopita
huko kwenye Jiji la Zanzibar katika mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Kama tujuavyo sote kulitokea ghasia zilizochochewa na viongozi wa
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu maarufu kwa jina la Uamsho.
Taasisi hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kidini, lakini hivi sasa
viongozi wake wameamua kuyaacha madhumuni hayo na kubeba ajenda za
siasa.
Siku
za nyuma, ndugu zetu hawa walikuwa wakitumia muda mwingi kuilaumu
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya kuundwa kwa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa lawama hizo sasa hazisikiki. Lakini, mara
tulipoanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, mihadhara yao imeelekezwa kupinga Muungano na kuwakashifu
viongozi waasisi wa Muungano na hata waliopo sasa. Isitoshe wamekuwa
wakipandikiza chuki dhidi ya ndugu zao wa kutoka Tanzania Bara na wale
wafuasi wa dini ya Kikristo.
Baya
zaidi, katika uchochezi huo majengo na mali za Makanisa mawili
zilichomwa moto, maduka ya watu kuvunjwa na mali zao kuibiwa. Kwa kweli
vitendo hivi ni uhalifu ambao haukubaliki na wala hauvumiliki.
Naungana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kauli yake aliyoitoa jana katika
mkutano wake na waandishi wa habari ya kukemea vikali na kulaani uhalifu
huo.
Ndugu Wananchi;
Ni
jambo la kusikitisha na kushangaza kwamba, wenzetu hawa wamefanya
uhalifu huo kwa hoja ya kupinga Muungano. Haiwezekani mtu anayepinga
Muungano, akaitetea hoja yake kwa kuchoma moto makanisa au kuvunja
maduka ya watu na kupora mali zao. Ukristo haukuingizwa Zanzibar na
Muungano, bali ulikuwepo karne kadhaa kabla ya Muungano na wala
haukutokea Tanzania Bara. Na kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais Ali
Mohamed Shein jana, ukweli ni kwamba, dini ya Kikristo kama ilivyo ya
Kiislamu imeenezwa Bara kutokea Zanzibar. Kanisa kuu la Anglikan
Zanzibar lilijengwa kuanzia mwaka 1873 na lile la Katoliki kuanzia 1893
ni miongoni mwa Makanisa makongwe kuliko mengi kama siyo yote kwa
upande wa Zanzibar na Bara.
Katika
hotuba yake ya jana, Mheshimiwa Rais, Dkt. Ali Mohamed Shein,pamoja na
kueleza kwa ufasaha ukweli huu, pia alisisitiza suala la haki na
uhuru wa Kikatiba wa mtu kuchagua au kubadilisha dini au imani yake.
Katika kutumia uhuru huo, mtu hastahili kuingiliwa au kulazimishwa na
mtu yo yote. Hayo pia ndiyo matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Kwa kweli yanayofanywa na ndugu zetu wa Uamsho ya kuchoma
moto makanisa siyo sawa hata kidogo. Na, wanapoyafanya kwa kisingizio
cha Muungano ni jambo lisiloeleweka kabisa na wala halina mantiki.
Labda wenzetu wana lao jambo.
Ndugu Wananchi;
Jambo
lingine la kushangaza zaidi ni kule kutokea vurugu na ghasia hizi
dhidi ya Muungano wakati ambapo Serikali imetoa fursa sasa kwa watu
kutoa maoni yao kwenye mjadala wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kama
tujuavyo sote, Tume ya Katiba imekwishaundwa na
inajiandaa kupita kote nchini kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba
mpya waitakayo. Kama mtu ana maoni yake kuhusu Muungano, hiyo ndiyo
fursa ya kufanya hivyo. Utaratibu mzuri umewekwa kwa ajili yetu sote,
vurugu za nini?
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Mimi
sioni sababu ya msingi ya kusababisha kuvurugika kwa amani kwa jambo
ambalo limewekewa utaratibu muafaka wa kulishughulikia. Nawaomba
tutumie utaratibu mzuri uliowekwa badala ya kufanya mambo yanayoleta
mifarakano katika jamii na yanayosababisha uvunjifu wa amani na
yanaharibu sifa na sura ya Wazanzibari na Watanzania isivyostahili.
Ndugu zangu,
Haipendezi
wala haifurahishi kwa Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya raia
wake. Lakini, kama hapana budi, Serikali lazima ifanye na haitasita
kufanya hivyo. Narudia kuwasihi viongozi na wafuasi wa Jumuiya ya
Uamsho kurejea kwenye madhumuni ya msingi ya jumuiya yao. Wajiepushe
na ajenda za kisiasa na kupandikiza chuki zitakazosababisha mifarakano
baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano na baina ya Wakristo
na Waislamu. Watanzania ni ndugu na wamekuwa wanaishi pamoja kwa upendo
na furaha licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini na maeneo
watokako. Kimeharibika kipi hata leo yatokee haya? Aidha nawaomba wenye
maoni kuhusu Muungano wetu, muundo wake na uendeshaji wake watumie
fursa ya mjadala wa Katiba kutoa maoni yao. Huhitaji kufanya ghasia
kutoa maoni yako!
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia fursa hii pia kuwapa pole wale wote walioathirika na vurugu
zilizotokea. Nawaomba wawe wastahamilivu, hiyo ndiyo mitihani ya
maisha. Serikali zetu mbili zitafanya kila lililo kwenye mamlaka yake
kuwahakikishia wananchi wote usalama wa maisha yao na wa mali zao.
Nawapongeza
vijana wetu wa Jeshi la Polisi kwa juhudi kubwa waliyoifanya ya
kudhibiti hali ambayo mwelekeo wake haukuwa mwema. Nawaomba waendelee
kuwa macho ili watu wasioitakia mema nchi yetu na watu wake wasipate
nafasi ya kutuvurugia amani na utulivu wetu. Naamini tukidumisha
utamaduni wetu wa kuheshimiana, kuvumiliana na kuzungumza pale
tunapotofautiana hakuna litakaloharibika. Haya shime tufanye hayo.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.
Post a Comment