JK azuiwa kusoma ripoti

Rais Jakaya Kikwete
NI YA KUJITATHIMINI KATIKA MKUTANO WA AU,KISA MADENI

RAIS Jakaya Kikwete amezuiwa kuwasilisha taarifa ya Tanzania kuhusu utekelezaji wa mpango wa Mpango wa kujitathmini wa Umoja wa Afrika (APRM), kwa sababu ya madeni makubwa yanayotokana na kutowasilishwa kwa michango kwa ajili ya uendeshaji wa sekretarieti ya mpango huo.
Tanzania inadaiwa kiasi cha Dola za Marekani 800,000 sawa na Sh1.258 bilioni kwa kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha (exchange rate) vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambavyo ni wastani wa Sh1, 572.87 dhidi ya Dola ya Marekani.
Deni hilo ambalo ni malimbikizo ya ada ya Dola 100,000 kila mwaka kwa miaka minane mfululilizo tangu mwaka 2005 ni kashfa kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inayoongozwa na Waziri Benard Membe, ambayo mpango wa APRM unatekelezwa chini yake.
Julai 22 mwaka jana, wakati akiwasilisha makadirio ya wizara yake, Membe alisema taarifa kamili ya mchakato huo hapa nchini ilitarajiwa kuwa imekamilika na kuwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa nchi wanachama wa APRM Julai, 2012.
Ni kwa mantiki hiyo, Rais Kikwete alitarajiwa kuwasilisha ripoti ya Tanzania kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika (AU) utakaofanyika Lilongwe, Malawi Julai 10 mwaka huu, lakini habari zinasema deni hilo limekwaza mpango huo.
Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib alisema jana: “Ni kweli kwamba tunadaiwa Dola 800,000 ambazo ni kama Sh1.2 bilioni na kidogo hivi na hizo ni malimbikizo ya mwaka huu wa 2012 na miaka mingine ya nyuma kwa sababu kila mwaka tunatakiwa kulipa Dola 100,000.”
Habari zilizopatikana baadaye na kuthibitishwa na Twalib zinasema tayari APRM Tanzania imepokea waraka kutoka Sekretarieti ya APRM na AU makao makuu kwamba ripoti ya Tanzania haitaweza kuwasilishwa katika mkutano huo wa Lilongwe.
“APRM nadhani wamepokea barua kutoka makao makuu kwamba Rais wetu hataweza kuwasilisha ripoti ya Tanzania, lakini hawa jamaa ni wajanja sana hawakueleza sababu ila wameambatanisha na orodha ya madeni tunayodaiwa kama nchi,”alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kuongeza:
“Hii ni aibu kwa Tanzania, wenzetu wanatushangaa kwamba sisi tumekuwa nyuma katika mambo haya yanayohusu Utawala Bora wakati sisi ndiyo tulitarajiwa kuwa msitari wa mbele kuliko wengine.”
Twalib katika maelezo yake alikiri kwamba Rais Kikwete hatawasilisha ripoti ya Tanzania kwenye mkutano huo wa Lilongwe lakini akasema hilo halihusiani moja kwa moja na deni nchi inalodaiwa.
“Kweli walileta taarifa hiyo kwamba taarifa yetu haitawasilishwa kwenye mkutano ujao, lakini ni kwa sababu ya mchakato wenyewe kuwa mrefu, lazima ipitie kwenye ngazi mbalimbali na kwa kungalia muda uliobaki pengine waliona kuwa hautatosha kukamilisha hatua zote,” alisema Katibu Mtendaji huyo.
Sehemu ya taarifa ya APRM Tanzania iliyowasilishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (NEC- CCM), Mei 15 mwaka huu, mjini Dodoma inaeleza kuwapo kwa kusudio miongoni mwa nchi zinazoshiriki mchakato wa APRM kuziengua zile zisizolipa madeni yake.
“Tanzania imeshindwa kulipa ada zake za kila mwaka kwa Sekretarieti ya AU/APRM kwa miaka saba iliyopita. Baadhi ya nchi zimeanza wanachama wa mchakato huu zimeanza kujenga hoja kwamba nchi kama Tanzania ziondolewe kwenye mchakato huu,”inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, Twalib alisema licha ya kwamba Tanzania inapaswa kulipa madeni yake, lakini hakuna kipengele chochote kinachoipa Sekretarieti ya APRM mamlaka ya kuizuia nchi kutathminiwa katika mkutano wa wakuu wa nchi.
Alikiri kuwa deni hilo linachafua taswira ya Tanzania mbele ya nchi nyingine na kwamba lazima yalipwe kwani ilijiunga kwa hiari na kusaini makubaliano ya kutoa michango husika.

Deni la Tanzania
Rais Kikwete alipata taarifa za Tanzania kudaiwa na APRM katika kikao cha (NEC- CCM) Mei 15, mwaka huu mjini Dodoma na inaelezwa kwamba zilimsutua.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa Rais alishangazwa na taarifa hizo hivyo kuagiza mchakato wa malipo ya deni hilo uanze mara moja: “Kweli Rais alionyesha kushangazwa na deni hilo na aliagiza kwamba fedha hizo zilipwe kesho yake,” alisema mmoja wa wajumbe wa NEC.
Hata hivyo, haifahamiki iwapo agizo hilo la Rais lilitekelezwa au la kwani wiki mbili tangu atoe maelekezo hayo ndipo APRM Tanzania walipopata taarifa kutoka AU kwamba ripoti ya Tanzania haitaweza kuwasilishwa.

Taarifa iliyowasilishwa NEC ambayo Mwananchi limeiona, inaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2012/13 APRM Tanzania wameomba kuidhinishiwa kiasi cha Sh5.194 bilioni kwa ajili ya kugharamia kazi zake lakini maombi yaliyowasilishwa Hazina na wizara kwa ajili ya mango huo ni Sh1.149 bilioni tu.
“Kwa upande mwingine kama fedha tulizoomba Sh5,194, 204,304 zingeidhinishwa, tungeweza kutekeleza majukumu yetu kama yalivyopangwa kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa ikiwa ni pamoja na kulipa limbikizo la deni la Sh1.280 bilioni ambalo halijalipwa kwa miaka saba,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaonyesha kwamba kiwango kinachopendekezwa kuidhinishwa na Bunge kinaweza kutosheleza kugharamia kazi za mchakato wa APRM nchini kwa miezi mitatu na kidogo ikilinganishwa na kile kilichoidhinishwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mwaka huu ambacho ni Sh 2.04 bilioni.
Tanzania pia inatajwa kwenye taarifa ya Sekretarieti ya APRM ya mwaka 2010 kwamba ni miongoni mwa nchi ambazo zimewahi kuwasilisha michango yake mara moja tu tangu iliposaini na kuridhia kushiriki kwenye mchakato wa kutathminiwa utendaji wake.

Nchi nyingine ambayo imewahi kulipa michango yake mara moja ni Sierra Leone wakati Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Djibouti, Sudani na visiwa vya Sao Tome na Principe hazijawahi kutoa mchango wowote.

Tanzania ni nchi pekee katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati inayodaiwa fedha nyingi ililinganishwa na majirani zake ambazo zinadaiwa kiasi cha fedha kwa Dola za Marekani kwenye mabano, Rwanda (300,000), Zambia (200,000), Kenya (100,000) na Uganda (400,000).
Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ezekia Wenje katika maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni, Julai 22 mwaka jana alihoji sababu za Serikali kushindwa kulipa deni hilo ambalo alisema linalitia aibu taifa.

“Deni la nchi yetu katika Sekretarieti ya APRM ngazi ya Bara la Afrika na malimbikizo yanafikia Sh 1.07 bilioni. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuthibitisha taarifa hizi na kujieleza ni kwa nini kwa kipindi chote hicho haikulipa ada ya uanachama APRM na lini italipa fedha hizo, kwani hii ni aibu kubwa kwa Taifa,” alisema Wenje.

APRM Tanzania
Mchakato wa kujitathini wa nchi za Afrika ulibuniwa na viongozi wa Afrika mwaka 2002, taasisi hiyo ilianza rasmi mwaka 2003 baada ya idadi ya wanachama iliyotakiwa kusaini mkataba huo kutimia.
Kwa upande wa Tanzania, Kamati ilibaini Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) zinaonyesha kuwa mpango huo uliridhiwa na Bunge la Nane, Februari 1, 2005, katika kikao cha Kumi cha Mkutano wake wa 14 na kupitisha Azimio la kuridhia Mkataba wa Tanzania kujiunga na Utaratibu wa African Peer Review Mechanism.

Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika taarifa yake mwaka jana ilisema: “Kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya mchakato huo sanjari na kulipia michango na ada ya uanachama kwa wakati.”

Hivyo hatua ya Tanzania kuzuiwa kuwasilisha taarifa yake kunaifanya iendelee kuchelewa zaidi kwani tayari muda uliotarajiwa kukamilisha mchakato huo ulikwishapita.

Wenje katika hotuba ya upinzani alibainisha kwamba: “Ni dhahiri kuwa nchi yetu imechelewa sana. Ni dhahiri kuwa Serikali haikutimiza wajibu wake kuhakikisha mchakato huu wa kujitathmini unatekelezwa kwa wakati kwani takriban miaka sita imepita tangu Bunge hili lipitishe uamuzi wa kuingia kwenye mchakato wa APRM, lakini hadi leo hatujaweza kupata ripoti ya mwisho ya APRM kuhusu nchi yetu.”

“Kwa kawaida kazi ya kujitathmini inapaswa kufanyika mara moja ndani ya kila miaka mitano, lakini kwa Tanzania huu ni mwaka wa saba bila kupatikana kwa ripoti ya mwisho. Nchi nyingine kama Ghana,Uganda na Rwanda tayari zimejitathimini na kupata ripoti zao za mwisho.”

Post a Comment

Previous Post Next Post