Kamati ya Zitto yawatimua TBS

KAMATI ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), imelazimika kuwarudisha wajumbe wa bodi ya Shirika la Viwango Nchini (TBS) kutokana na maswali ya ukaguzi 13 kushindwa kupatiwa ufumbuzi.
Licha ya hayo pia wameitaka bodi hiyo kuja na majibu na mapendekezo yao juu ya ukaguzi maalumu uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na uchunguzi uliofanywa na kamati ndogo ulioongozwa na Deo Filikunjombe kuhusu mawakala wa ukaguzi wa magari wa Hongkong na Singapore.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe (Chadema), alisema kuwa kutokana na kupitia taarifa hiyo wamebaini upungufu hivyo kamati yake imeagiza bodi hiyo ikajipange upya na kuja na taarifa sahihi.
Akitolea mfano alisema kuna suala la wakala wa ukaguzi wa magari yanayoingia nchini ambapo wamekuwa wakifanya kazi bila kuwa na leseni hatua ambayo inaiwia vigumu serikali kupata fedha inazodai kutoka kwa mawakala hao kiasi cha dola milioni 253.
Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini alisema pamoja na shirika hilo kutakiwa kufanya ukaguzi wa bidhaa mbalimbali lakini wameshindwa kufanya kazi hiyo na matokeo yake kumekuwepo na bidhaa zisizo na ubora kuingia nchini.
“Kuna bidhaa ambazo taarifa ya CAG imezigundua kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu kama vile omo, mafuta ya magari, matairi, mbolea lakini zimekuwa zikiingizwa kwa kibali cha Mkurugenzi Mkuu wa TBS Charles Ekelege,” alisema.
Zitto alisema bidhaa nyingi ambazo ni bandia zilioneshwa kukaguliwa na kugundulika ubovu wake, lakini zimeendelea kutumika kutokana na wenye kampuni hizo kufanya mawasiliano na Ekelege naye kutoa kibali cha kuingizwa kwa bidhaa hizo.
Zitto alisema kuwa bodi hiyo inapaswa kuja na mapendekezo mapya Juni 30, mwaka huu, huku wakitakiwa kufanya kazi zao kwa umakini kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuteketeza bidhaa bandia.

Post a Comment

أحدث أقدم