Kikwete ashuhudia hasira za wananchi

MSAFARA wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, jana ulisimama
kwa muda katika eneo la Namanga lililopo Tegeta wilayani Kinondoni,jijini Dar es Salaam kufuatia mapigano yaliyotokea baina ya wakazi wa eneo hilo na watu waliotumwa na mmiliki wa kituo cha mafuta cha Gapco kuvunja nyumba zao.

Licha ya msafara huo kusimama kwa dakika kadhaa wakati wakielekea mjini Bagamoyo,  askari waliokuwa katika msafara huo walilazimika kufanya kazi ya ziada ya kufyatua mabomu ya machozi kuzima mapambano yaliyokuwa yakiendelea baina ya makundi hayo ambayo yalihusisha silaha za moto na zile jadi.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela amethibisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa watu wawili wamejeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya Mwananyamala na Jeshi la polisi linamshikilia mmiliki wa kituo hicho.
Alisema pia walinzi 54 wa Nas na wabomoaji 44 wanashikiliwa na polisi kuhusiana na vurugu hizo na mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Farida Saidi alisema, sakata hilo lililosababisha eneo hilo kugeuka uwanja wa mapambano, lilitokea majira ya saa 3:45 asubuhi.
Farida alisema, muda huo lilifika kundi la watu wapatao 100 wakiwamo walinzi wenye silaha za moto wa Kampuni binafsi ya Nas na kuwataka wakazi wanaoishi  nyumba zilizokuwa katika eneo hilo kuondoa vitu vyao haraka kwa lengo la kuvunjwa kwa nyumba hizo.

 "Walipofika wakawa wanapaza sauti wakitueleze kuwa kila mtu atoke na kilicho chake kwani nyumba zinavunjwa," alisema wakiwa bado wameduwaa ndipo vijana hao walipoanza kuwashambulia kwa kuwapiga na kuwatoa nje ya nyumba zao.

Alisema licha ya kupewa vipigo na vijana hao, lakini pia waliendesha vitendo vya uporaji hali ambayo iliwafanya wakose uvumilivu na kuchukua hatua ya kukabiliana nao na ndipo walinzi hao walipopiga risasi mbili hewani ambazo zilijibiwa kwa mawe, marungu na silaha zingine toka kwa wakazi hao.

Hali hiyo ilizua sintofahamu katika eneo hilo na katikati ya ghasia hizo ndipo msafara wa Rais Jakaya Kikwete ukawa unapita na kukuta barabara imefungwa kwa mapambano hali ambayo ilizua mtafaruku mkubwa ambao uliwalazimisha walinzi wake kuingilia kati.
"Askari waliokuwa katika Land Rover walishuka na kuanza kupiga mabomu ya machozi na muda mfupi baadae msafara ukaendelea na safari", alisema shuhuda mwingine eneo hilo Shaaban Mohamed.

Kenyela  alikiri kuwa msafara wa Kikwete kukumbwa na dhahama hiyo katika kadhia hiyo na kueleza kuwa hata hivyo hakuna ambaye amejeruhiwa katika msafara huo wala gari ambalo limeharibiwa.
"Siwezi kusema msafara wa Rais umesimamishwa na ghasia hizi isipokuwa  ilitokea bahati mbaya wakati vurugu zinatokea na wao walikuwa wanapita hali ambayo ilisababisha usumbufu kidogo lakini msafara ulipita salama", alisema Kenyela.

Kamanda Kenyela alisema kutokana na hali kuwa tete eneo hilo kituo hicho cha mafuta kitakuwa chini ya ulinzi wa polisi hadi hapo itakapoelekezwa vingine kwa kuwa suala hilo wanalifanyia uchunguzi kujua kama kulikuwa na taratibu za kisheria ambazo zilifuatwa.

Wakazi wa eneo hilo walidai kuwa eneo hilo ni lao na mmiliki huyo alikuwa katika mazungumzo nao ya kutaka wamuuzie lakini maafikiano hayakufikiwa muafaka kunako Machi mwaka huu hivyo walishangaa kumuona mwakilishi wa mmiliki huyo akija na kuwataka waondoke kwani eneo hilo limeuzwa.

Kulingana na hati yenye namba 112/2012 ya Baraza la ardhi Wilaya ya Kinondoni ya Aprili 29, mwaka huu ambayo imebandikwa katika miti na kuta za nyumba za eneo hilo, inazuia kuondolewa kwa wakazi hao hadi shauri la msingi litakapomalizika katika baraza hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post