Mahakama ya kadhi kuanzishwa wakati wowote -Pinda

Serikali imesema uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi itakayoshughulikia migogoro na masuala mbalimbali ya usatawi wa Waislamu nchini umefikia katika hatua nzuri.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema jana wakati akijibu hoja za wabunge zilizojadili kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na  Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Alisema itaanzishwa wakati wowote baada ya maandalizi kukamilika na kwamba utekelezaji wake uko katika hatua nzuri baada ya kamati ndogo iliyoteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria yenye wawakilishi wa Waislamu na Serikali imetoa taarifa yake ya mwanzo ya  namna ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.

Waziri Mkuu alisema mambo yatakayoshughulikiwa na mahakama  hiyo ni pamoja na ndoa na talaka, mirathi, wosia, hiba/zawadi na wakifu vilevile itahusika na mashauri ya jinai.

Alisema “upo umuhimu na dhamira ya kweli ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara aidha, mahakama hiyo itagharamiwa na kuendeshwa na Waumini wa Dini ya Kiislamu wenyewe.” Alisema.

Alisema wataalamu wa kuanzisha mahakama hiyo watakwenda  nchini Kenya, India, Uingereza  na Zanzibar kujifunza jinsi ya kuanzisha chombo hicho na kwamba ziara hiyo itagharamiwa na serikali.

BILIONI 300 ZILIZOHIFADHIWA KWENYE BENKI ZA USWISI

Waziri Mkuu alisema taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na ile ya  upelelezi wa fedha (Financial Intelligency Unit (FIU) zimemeanza kufanya uchunguzi wa taarifa za wizi wa Sh. bilioni 300 za rushwa kutoka kwenye miradi ya gesi na petroli zilizohifadhiwa na Watanzania sita katika Benki ya Uswizi.

Alisema uchunguzi huo utakapokamilika matokeo yake yatatangazwa kwa umma.

MATUMIZI YA FEDHA ZA CHENJI YA RADA

Waziri Mkuu akizungumzia kuhusu matumizi ya fedha za  rada zilizolengwa kununua madawati na  vitabu kwa ajili ya shule za  misngi  hayatabatilishwa.

Katika michango yao wabunge walishauri fedha hizo zinunulie madawati na kujenga nyumba za walimu badala ya kununua vitabu na madawati na pia walitaka Zanzibar nayo ipate mgawo wake.

Pinda alisema kwa mujibu wa hati ya makubaliano baina ya  Serikali ya Tanzania  - Wizara ya Fedha  na Serikali ya Uingereza kupitia shirika DFID na kampuni ya vifaa vya  mawasiliano na usalama ( BAE Systems)  na taasisi ya kuuchunguza rushwa kubwa (SFO)  iliyosainiwa Machi, mwaka huu, ilikubaliwa kuwa matumizi ya fedha za fidia ya rada yawe kwenye kuimarisha elimu ya msingi.

Alisema ilikubalika kuwa asilimia 75 ya fedha zitumike kununua vitabu vya kiada, viongozi vya walimu na  mihtasari ya ya walimu  na asilimia 25 iliyobakia itumike  kununua madawati.

Alisema maamuzi hayo yalifanywa kufuatia ukweli kuwa  kitabu kimoja hutumiwa na wanafunzi 10 na  kwa wastani wanafunzi wengi hawapati fursa ya kutumia vitabu katika maisha yao yote  ya shule.

Ilibainika kuwa  kukosekana  mihtasari na vitabu vinavyowaongoza kufundisha kunasababisha wanafunzi wengi kuhitimu elimu ya msingi bila kupata stadi za kutosha za  kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) na hivyo kutofanya vizuri kwenye mitihani yao ya darasa la nne na saba.

Alisema vitabu vikinunuliwa kutakuwa na uwiano mzuri wa kwa masomo ya msingi yaani Hisabati, Kiswahili, Sayansi, Kiingereza na Jiografia na kwamba kitabu kimoja, kitatumiwa na wanafunzi wawili hadi watatu.

Kwa upande wa walimu alisema watakuwa na uhakika wa kupata muhtasari, miongozo ya masomo na viongozi vya mwalimu kwa masomo yote.

Alisema makampuni za Kitanzania 13 yakiwemo Ben Company, Best Deal Publisher,  E & D Vision, Education Books Publisher, Jadida, LongHorn,  Longman, Macmillan, Mkuki na Nyota, Mture, Oxford, Taasisi ya Elimu (TIE), Ujuzi Book yatanunua vitabu hivyo.

Kwenye madawati alisema  eneo hili lilichaguliwa kutokana na upungufu mkubwa wa madawati kitaifa na takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa karibu nusu ya wanafunzi wote nchini ambao ni milioni  nane (8,000,000) hawana sehemu nzuri za kukalia.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa upungufu wa madawati uliopo ni kati ya milioni 1.5 na milioni mbili.

Alisema iwapo madawati yatanunuliwa kwa bei nafuu Sh bilioni 18.1 zilizotengwa zitanunua madawati yasiyopungua karibu 4000,000na kuwezesha watoto 1,200,000 kunufaika.

Lakini alisema iwapo zitajenga nyumba za walimu si busara kwani kwa vile  wastani wa Sh milioni 12 zinahitajika kujenga  nyumba moja ya mwalimu fedha zote zitajenga  nyumba 6,000 hivyo kwa shule 16,000 zilizopo nchini kote hazitaweza kupata nyumba za walimu na uhaba utabakia pale pale.

Alisema kwa msingi huo fedha hizo zitatumika kununua vitabu na madawati na pia hazitapelekwa Zanzibar kwa vile ununuzi wa rada ulifanywa na Sekta ya Mawasiliano ya Wizara ya Miundombinu ambayo siyo ya Muungano na siyo Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambayo ni miongoni za Wizara za Muungano.

PENSHENI YA WAZEE
Kuhusu pensheni ya wazee alisema serikali imeanza kufanya utafiti wa jinsi ya kuwalipa wazee na mchakato unafanywa kikanda  ambapo imechaguliwa mikoa saba  inayowakilisha kanda mbalimbali ili kufanyika utafiti wa awali.

Aliitaja kuwa ni Rukwa, Mtwara, Dodoma, Manyara, Kagera, Pwani na Dar-es-Salaam.

Alisema dodoso zimesambazwa kwa wilaya zote ili kuanza kukusanya taarifa zote muhimu na kazi hiyo imeanza katika mikoa ya Pwani na Dar-es-Salaam.

Pinda alisema serikali inatarajia mara baada ya kukamilisha utaratibu wa kuandaa utaratibu wa malipo ya pensheni hiyo serikali itatoa taarifa kamili inayoelekeza utekelezaji wa Pensheni kwa Wazee Wote.

Wabunge walipitisha bajeti hiyo.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post