
Kiongozi wa Jumuiya ya kikundi cha UAMSHO, Sheikh Farid Hadi Ahmed
---
SIKU
moja tu baada ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein, kuzungumza
na Waandishi wa Habari Ikulu mjini Zanzibar kuhusiana na Vurugu
zilizotokea wiki iliyopita, leo Kiongozi wa kundi la Uamsho Sheikh Farid
Hadi Ahmed, amezungumza na Waandishi wa Habari na kusema kuwa
wataendelea na harakati zao ya kupinga Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar mpaka kieleweke.
Sheikhe
Farid ambaye amelaani vikali vitendo vya uharibifu wa mali ukiwemo wa
uchomwaji moto magari na baadhi ya makanisa mjini Zanzibar, amesema
pamoja na wao kulisaidia Jeshi la Polisi katika kukusanya taarifa za
kuwabaini wale wote waliohusika na uharibifu huo, lakini pia
wataendeleza harakati za kudai kura ya maoni ya kupinga Muungano wa
Jamhuri ya Tanzania.
Ingawa
alikataa wafuasi wake kushiriki katika vurugu, lakini amesema leo
wanakesha msikitini kuwaombea heri vija wote waliokamatwa kufuatia
vurugu hizo ili waachiliwe bila ya masharti.
Sheikhe
Farid pia amewalaumu baadhi ya vijana wakiwemo wa chama kimoja cha
siasa kuwa wao ni miongoni mwa wanzilishi wa vurugu hizo.
Amesema
kwa hatua hiyo anajenga imani kuwa miongoni mwa watu waliochoma
makanisa siku ya tukio hilo, walikuwa ni mmoja miongoni mwa vijana hao
na wanakamilisha taarifa zao ili kuwapatia Polisi kwa hatua zao.
Amesema
mbali ya kuwa Serikali imepiga marufuku mikutano na maandamano, lakini
Jumuiya yao ya Uamsho itafanya Mhadhara mkubwa Jumapili Juni 3, mwaka
huu kwenye Viwanja vya Lumbumba mjini Zanzibar mhadhara ambao
utafuatiwa na maandamamo yatakayofanyika Juni 26, mwaka huu.
Wakati
wa mkutano huo, Sheikhe Farid pia amevilaumu baadhi ya Vyombo vya
Habari hapa nchini na kusema wameandika habari zenye chumvi nyingi na
kuupotosha umma kwa kuongeza hofu miongoni mwa wananchi wa ndani na nje
ya Zanzibar.
Hata
hivyo Shehe huyo ameshindwa kufafanua baadhi ya hoja alizoulizwa na
waandishi wa habari kwa mfano kuzibwa kwa barabara kwa mawe na magogo ya
minazi ama kuchomwa matairi na makanisa kuwa inauhusiano gani na madai
ya kuwepo kwa muungano.
Post a Comment