Membe aikoroga CCM
Kauli yake ya kuitabiria ushindi CHADEMA yaibua hofu
KAULI ya hivi karibuni iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe ya kuitabiria ushindi na kukitaka
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kijiandae kushika dola
mwaka 2015, imewaduza vigogo na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Membe ambaye ni mmoja wa makada wa CCM wanaotajwa kuutaka urais mwaka
2015, alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akiukaribisha msafara wa
CHADEMA nyumbani kwake kijijini Rondo na kushiriki nao chakula cha
pamoja.
Duru za siasa kutoka ndani ya CCM, zilisema kuwa kauli ya Waziri Membe
si tu kwamba imewashangaza vigogo wa CCM, bali pia imetafsiriwa kama ni
mmoja wa mawaziri wanaotajwa kutaka kujiunga na CHADEMA hasa baada ya
jina lake kutajwa na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
kama mmoja wa mawaziri wanaotarajiwa kujiunga na chama hicho kikuu cha
upinzani nchini.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara hivi karibuni uliofanyika mjini
Sengerema, Lema aliwataja mawaziri wengine wanaotarajiwa kujiunga na
CHADEMA kuwa ni pamoja na Edward Lowassa (Monduli) na Samuel Sitta
(Urambo Mashariki). Lowassa na Sitta kwa nyakati tofauti walikanusha
madai hayo, lakini Waziri Membe hajawahi kukanusha.
Mwenyekiti wa Wazazi (CCM) Wilaya ya Nyamagana, Emmanuel Nzungu
aliliambia gazeti hili jana kuwa kauli ya Waziri Membe ina utata mkubwa.
“Tumezungumza kwenye vikao vyetu hapa ofisini, tumeona kuna haja ya
kuleta hoja hii kwenye vikao vya juu vya chama. Hii si kauli ya utani
bali ni kauli iliyopangwa na hatujui kwa sababu gani,” alisema Nzungu.
Alisema kibaya zaidi kauli hii imetolewa na Waziri Membe siku chache
baada ya Lema kumtaja kuwa mmoja wa mawaziri wanaotajwa kutaka kuhamia
CHADEMA.
“Ningesoma kwenye magazeti, ningesema amewekewa maneno mdomoni, lakini
nilimwona kwa macho yangu kwenye kituo cha televisheni ya ITV
aikimwagia sifa CHADEMA na kuitabiria ushindi. Hii inashangaza sana na
lazima kauli yake ijadiliwe kwenye vikao vya chama,” alisema Nzungu.
Kada mwingine ambaye ni mjumbe wa NEC aliyeomba jina lake lihifadhiwe,
alisema kuwa anashangazwa na ukimya wa viongozi wa juu wa CCM kwani
hakuna aliyetoa kauli ya kumwonya Waziri Membe.
“Kuna makada wa CCM waliowahi kutoa kauli ndogo tu, lakini chama
kilitumia nguvu kuzijibu na kuzitolea ufafanuzi. Hii kauli ya Waziri
Membe ya kuitabiria kifo CCM na kuitabiria ushindi CHADEMA si ya
kupuuzwa,” alisema mjumbe huyo wa NEC toka mkoani Shinyanga.
Hivi karibuni Waziri Membe aliwakaribisha na kufanya mazungumzo na viongozi wa CHADEMA waliotembelea kijijini kwake.
Katika mazungumzo yake na viongozi hao mbele ya waandishi wa habari,
Waziri Membe alikitabiria chama hicho kushika dola mwaka 2015 kwa vile
kina mvuto kwa Watanzania.
Viongozi waliokaribishwa nyumbani kwa Membe ni pamoja na Lema, James
Millya ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM Mkoa wa Arusha
na viongozi wengine wa kata za Chiponda na Mnara.
Membe ambaye pia ni Mbunge wa Mtama na mjumbe wa NEC,
aliwatahadharisha wabunge wenzake wa CCM kwamba wako hatarini kung’olewa
katika majimbo yao na CHADEMA kwani chama hicho kwa sasa kimeimarika na
kukubalika kwa wananchi wengi.
“CHADEMA sasa imegundua udhaifu wao uliokuwa ukisababisha isishinde,
zamani mlikuwa mkifanya kampeni mikoani, lakini kitendo cha kufika kata
hadi kijiji, hii sasa ndio siasa safi.
“Wapo wengi wanaodhani kuja huku ni kama mmekuja kuwavamia la hasha,
siasa ni nguvu ya hoja, haina maana mmekuja kumshughulikia mtu, binafsi
najua nguvu ya hoja ndiyo inayoleta maendeleo.
“Pia nguvu ya hoja inasaidia kuleta maendeleo, yaani nguvu ya hoja
unaweza kuita ni mgongano au msuguano wa kimawazo ambao unakumbusha
uwajibikaji wa chama na serikali.
“Mimi najua maana ya siasa, nimeishi miaka 10 nje ya nchi zenye
demokrasia safi, ikiwamo Marekani, pia nimesoma miaka miwili, hivyo kuja
kwenu hapa kunaweza kuchukuliwa na wabunge au Watanzania wengine
mmekuja kuwaingilia, hapana.
“Mimi naipenda siasa ya demokrasia na nailewa zaidi na ndiyo maana
niliposikia mko huko nimesitisha ziara zangu jimboni na natarajia kurudi
Dar es Salaam na kusafiri kwenda nje ya nchi,” alisema.
Membe alisema katika dunia hii ya tatu, vitu vyote vinabadilika
yakiwamo mabadilko ya siasa na kuongeza kwamba, hali ilivyo Tanzania
lazima kutakuwapo na mabadiliko ya vyama vya upinzani kushika dola.
“Kuna nchi nyingi zilikuwa na vyama zaidi ya 500 ikiwamo Angola,
lakini hadi sasa vimepungua na kufikia 310, sasa tahadhari yangu kwenu
CHADEMA hivi sasa mko ‘strong’ na mnashika nafasi ya pili, muanze
kujiandaa kuunda serikali ingawa bado kuna vita vikali mbele.
“Mnaweza mkajiamini mnaweza kushinda, lakini mwishowe upepo ukageuka,
unajua binadamu na mnyama ni vitu vya ajabu sana, vyama vingine vinaweza
kutumia rungu hilo hilo kukumaliza,” alisema.
Adha, Membe aliwaonywa viongozi kuchukua tahadhari kubwa juu ya
serikali ya umoja, huku akitolea mfano nchi za Kenya na Ethiopia.
“Hakuna serikali yoyote ya mseto au ya umoja itakayoleta maendeleo kwa
wananchi na sote ni mashahidi wa nchi hizo, mfano Keneth Kaunda chama
chake kilikuwa na wafuasi wengi kikashinda na watu wakashangilia, lakini
wiki tatu za kwanza walikuwa katika vita vya kuunda serikali.
“Serikali ya mseto ina madeni makubwa, maana kila chama, taasisi mtu
ana watu wake wa kutaka kupewa madaraka, mwishowe mnajikuta matatizoni,
epukeni misaada ya wafadhili maana waliokusaidia watakugharimu baadaye.
“Hapa kwetu kule Zanzibar wamenusurika kwa kitu kimoja tu, CCM na CUF
wameunda Serikali ya Umoja, lakini Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ndicho kilichowasaidia.
“Ile serikali ipo chini ya chama mama, chama chenye nguvu na fedha, kina miongozo, kanuni za CCM zinazotekelezeka,” alisema.
Alimweleza Lema kwamba alisikitishwa na maamuzi yaliyotolewa na mahakama ya kumnyang’anya ubunge.
“Lema, sikuamini baada ya maamuzi kutolewa na mahakama, lakini kama
umekata rufaa nafikiri huku kutatendeka haki zaidi, bila shaka utarudi
bungeni,” alisema.
Chanzo:- Tanzania Daima
Post a Comment