Mkurugenzi TBS alikoroga Bunge
• Akiri kusafiri na menejimenti ya TBS
MKURUGENZI wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege
aliyesimamishwa kazi, anaelekea kulivuruga Bunge na kusababisha
mgongano wa kimamlaka.
Kuibuka kwa mvurugano huo kunatokana na hatua ya Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Viwanda na Biashara, Mahmoud Mgimwa kusafiri kwenda nje ya
nchi na menejimenti ya TBS pasipo kupata baraka au kibali cha Spika wa
Bunge.
Mbali ya hilo, Mgimwa ambaye hivi karibuni alituhumiwa kuandaa ripoti
ya kumsafisha mkurugenzi huyo wa TBS baada ya ziara hiyo, ameibuka na
kukana kupata kufanya hivyo.
Sambamba na hayo, hali ya mkorogano ndani ya Bunge imeongezwa na hatua
ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuibuka na kueleza kutojua chochote
kuhusu ziara hiyo wala ripoti iliyokuwa na mwelekeo wa kumsafisha
Ekelege ambaye hivi karibuni aliibua mjadala mkali bungeni.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Spika Makinda alisema alikuwa
hana taarifa zozote kuhusu suala hilo wala safari ya Mgimwa kwenda Japan
na China akiwa ameongozana na menejimenti ya TBS.
“Mgimwa alisafiri kama Mgimwa. Mimi Spika sina taarifa na wala ofisi
yangu haijampa kibali, na sitambui wala sijui ameendajeendaje huko,
labda akwambie yeye, maana sisi tuna utaratibu wetu,” alisema Makinda.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Mgimwa alikiri kusafiri na
timu hiyo ya watu 14 kutoka TBS katika kipindi cha kati ya Mei 6 na 14
mwaka huu, lakini akasema yeye alienda huko kwa ajili ya kujifunza na si
kufanya uchunguzi kama ilivyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Kuhusu kutopata ridhaa ya Spika au kibali chake, Mgimwa ambaye ni
mbunge wa Mufindi Kaskazini, alisema ziara hiyo aliyoiita ya kujifunza,
ilikuwa haina uhusiano wowote na shughuli za Kamati ya Bunge Viwanda na
Biashara.
Mbali ya hilo, Mgimwa alikana kuandaa ripoti yoyote kwa niaba ya
kamati yake ambayo pamoja na mambo mengine, ilikuwa ikimsafisha Ekelege,
na akasema iwapo kulikuwa na taarifa yoyote basi ilitolewa na TBS
wenyewe ambao ndio waliomwalika katika ziara hiyo.
“Mwandishi labda nikueleweshe hiyo isije kuleta matatizo. Mimi
nilienda kama mimi kujifunza na wala kuhusu ripoti mimi sijui kwa kuwa
sikuiandika. Waulizeni TBS ambao ndio waliandika na kamati yangu
haihusiki kwa lolote na wala yenyewe haikufanya ziara.
“Ni kweli nilienda Japan na menejimenti hiyo na nilialikwa kama mtu
binafsi na kwamba hakuna ripoti yoyote niliyoandika, pengine kama
imeandikwa na TBS wenyewe, hivyo waulizwe hiyo ripoti wao. Sikwenda
kumsafisha mtu mimi,” alisema Mgimwa.
Hata hivyo, ripoti iliyotolewa na TBS yenye mwelekeo wa kumsafisha
Ekelege na taasisi yake, ambayo Tanzania Daima Jumapili iliiona nakala
yake, inaeleza kuridhishwa na namna mawakala wa shirika hilo
wanavyofanya kazi nzuri katika nchi za China na Japan.
Akifafanua zaidi, Mgimwa kutokana na uzoefu alioupata, anaamini kuna
haja kwa wajumbe wa kamati yake kwenda katika nchi zenye ofisi za TBS
kwa ajili ya kujifunza, na kwamba alikuwa akitarajia kutuma maombi kwa
Spika ili awape ruhusa waende wakaangalie sheria mbalimbali kama zinafaa
au la.
Habari kutoka ndani ya duru za kamati za Bunge zinaeleza kwamba, hatua
hiyo ya Mgimwa inaonekana kuchukua mwelekeo tofauti na unaokinzana na
ule uliochukuliwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
(POAC), ambayo katika ripoti yake kwenye mkutano uliopita wa Bunge,
iliibua shutuma nzito dhidi ya TBS na mkurugenzi wake, Ekelege.
Taarifa hiyo ya POAC ambayo ilimbana pia aliyekuwa Waziri wa Viwanda
na Biashara, Cyril Chami kwa tuhuma za kumlinda Ekelege, iliibua kile
kilichoonekana kuwa ni uoza ndani ya TBS, ambayo ilibainika kuwa na
ofisi hewa katika baadhi ya mataifa ambako ilikuwa ikidai kukagua ubora
wa bidhaa zinazoingizwa nchini.
Ripoti hiyo ya POAC ambayo ilimlaumu Chami kwa kushindwa kumsimamisha
kazi au kumwajibisha Ekelege, ilitokana na ziara walizofanya baadhi ya
wajumbe wake waliotembelea Hong Kong na Singapore na kubaini kasoro
hizo.
Siku chache tu baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Dk. Abdallah
Kigoda kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, waziri huyo alitangaza
kumsimamisha kazi Ekelege na kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma
zilizokuwa zikielekezwa kwake.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
إرسال تعليق