Mtikila kufungua kesi ya kudai Tanganyika
MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher
Mtikila, anakusudia kufungua kesi mpya katika Mahakama ya Haki za
Binadamu ya Afrika iliyoko Arusha, kudai serikali ya Tanganyika.
Mchungaji Mtikila aliyasema hayo jana mjini hapa, mara baada ya
kuahirishwa kwa kesi aliyoifungua katika mahakama hiyo kudai uwepo wa
mgombea binafsi.
Mtikila alisema kuwa kutokana na imani kubwa aliyonayo kwa mahakama
hiyo, ana imani haki aliyokua akiitafuta kwa muda mrefu sasa iko mbioni
kupatikana.
Alifafanua kuwa katika kufungua kesi hiyo ya kudai Tanganyika, kuna
wanasheria kutoka Nigeria wako tayari kuja kusimamia katika kesi hiyo
ambayo alidai itakuwa ni ukombozi kwa Watanganyika wote.
Aidha alisema kuwa wakati yeye anakusudia kufungua kesi hiyo tayari
ana taarifa za kuwepo kwa baadhi ya Wazanzibari wanakusudia kufungua
kesi katika mahakama hiyo kupinga muungano.
Awali katika mahakama hiyo, kesi iliyoanza kusikilizwa juzi na
mahakama hiyo juu ya hoja ya mgombea binafsi iliyofunguliwa na Mtikila
pamoja na kituo cha msaada wa sheria na haki za binadamu mara baada ya
kusikilizwa hoja za pande zote mbili iliahishwa.
Kesi hiyo inayosikilizwa na majaji tisa kati ya 10 wa mahakama hiyo
iliahirishwa hadi baada ya siku 90 ambapo itakuja kutolewa hukumu
kutokana na pande zote mbili kukamilisha ushahidi wao.
Katika kuwasilisha maelezo ya mwisho na kujibu maswali yaliyotolewa na
majaji wa mahakama hiyo, upande wa Mtikila uliiomba mahakama hiyo
itamke kuwa na haki kuwepo na mgombea binafsi katika chaguzi zote za
kisiasa hapa nchini.
Aidha kupitia kwa wanasheria James Jesse, Clement Mashamba, Donald
Deye na Profesa Lajovi waliiomba mahakama hiyo pia iiamuru serikali ya
Tanzania kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Jaji Elsien Thompson alimuuliza Mtikila ni kwa nini anataka
kuwepo kwa mgombea binafsi wakati yeye tayari ana chama chake
kinachomuwezesha kupata fursa ya kugombea.
Kupitia mawakili wake, Mtikila alijibu kuwa kutokana na kuwepo na
taratibu ngumu za uidhinishwaji wa vyama kuruhusiwa kusimamisha
wagombea, imepelekea mteja wao kushindwa kupata haki hiyo.
Chanzo:- Tanzania Daima
إرسال تعليق