Mukama awatibua CHADEMA
Mbowe akereka, amjibu kwa vielelezo
KATIKA kile kilichoonekana kama vijembe vya kisiasa kuutawala
msiba wa muasisi wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Bob
Makani, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, jana alijikuta katika wakati
mgumu kutokana na kauli yake kupingwa vikali na Freeman Mbowe.
Mukama wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya chama chake
katika viwanja vya Karimjee zilikofanyika shughuli za kuuaga mwili wa
marehemu, alimsifu Makani akisema alikuwa ni Katibu Mkuu wa Kwanza wa
CHADEMA kutoka nje ya kanda ya kaskazini kati ya waasisi wenzake tisa.
Mbali na sifa nyingi alizommwagia marehemu, Mukama pia alisema CHADEMA
wanatakiwa kuweka kumbukumbu hiyo kwa kuwa alikuwa ni mtu shupavu
asiyependa kuongea wala kuhubiri kwa muda mrefu na asiyekumbatia udini,
ukabila na ukanda.
Hata hivyo, wakati Mukama akieleza hayo, viongozi wengi wa CHADEMA
walionekana kushangazwa na kauli ile ambapo Mwenyekiti wa chama hicho,
Mbowe, katika salamu zake alitumia mwanya huo kumjibu kwa vielelezo.
Mbowe alisema kuwa kitendo cha kusema kuwa CHADEMA kiliasisiwa na watu
tisa kutoka eneo moja la kanda ya kaskazini ni uchafuzi wa kihistoria
ndani ya chama hicho.
Katika kuonesha kukerwa na kauli hiyo, Mbowe alilazimika kuwataja
waasisi na mikoa yao kuwa ni Edwin Mtei (Arusha), Makani (Shinyanga),
Marehemu Brown Ngwilupipi (Iringa), Edward Barongo (Kagera), Mary Kabigi
(Mbeya), Menrad Mtungi (Kagera), Costa Shinganya (Kigoma), Evalist
Maembe (Morogoro) na Steven Wassira (Mara).
“Mimi wakati huo nilikuwa mdogo na shughuli zangu zilikuwa ni kuandaa
vikao na mikakati ndani ya chama. Nashangaa sana wakati nakumbuka
historia ya chama hiki, hivyo watu wasijaribu kuipotosha,” alisema
Mbowe.
Mbowe pia aligusia suala zima la uanzishwaji wa mchakato wa Katiba
mpya akisema ni lazima kufanyike na marekebisho ya mfumo wa kisheria ili
kuwapa nafasi wenye uwezo kuingia bungeni na kutoa michango ya
maendeleo kwa jamii.
Alisema mwaka 1995, 2000 na 2005 Makani aligombea ubunge Shinyanga
Mjini akashindwa, hivyo ni vema watu kama hao wenye mchango mkubwa
wakaingizwa bungeni kwa ajili ya kuleta changamoto mbalimbali.
Rais Kikwete amlilia
Rais Jakaya Kikwete naye alielezea kuhuzunishwa kwake na msiba huo na
kusema kuwa Bob Makani alikuwa ni mtu muhimu na msaada mkubwa katika
michango yake aliyowahi kuitoa katika kukuza uchumi wa nchi.
“Nilisikia taarifa za msiba ambao ulinihuzunisha na kushtuka sana
nikajaribu kumpigia simu Mwenyekiti wa Chama, Mbowe, lakini hakupatikana
kwa kuwa alikuwa katika shughuli kubwa huko Ruangwa, nikamtumia ujumbe
mfupi na baada ya kuupokea akanipigia na mimi nilikuwa katika shughuli
sikupatikana, hivyo nikampigia tena baadaye ndipo tukazungumza,” alisema
Kikwete.
Rais Kikwete alisema kuwa ni vema kuhuzunika kwamba tumepoteza mtu
muhimu lakini pia iendane sambamba na kusherehekea na kuyaenzi mambo
yake mazuri ambayo ameyafanya wakati wa uhai wake.
Prof. Lipumba akumbusha enzi
Kwa niaba ya vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa CUF, Prof Ibrahim
Lipumba, alimwelezea Makani kuwa alikuwa mtu mzuri na kwamba CHADEMA
inatakiwa kuiga mfano wake wa kuunganisha watu.
Alisema alikuwa ni mwana mageuzi aliyeasisi harakati za mabadiliko ya
Katiba na kusema alipata suluba pamoja naye katika mapambano hayo. Pia
alikumbushia enzi zao za shule akisema Makani alikuwa na akili nyingi
darasani.
Muasisi wa CHADEMA ambaye aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu na
Mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, Erdwin Mtei, alimtaka Makani kuwa
alikuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu, na ameeleza masikitiko yake ya
kuondokewa na mwenzake.
Mtei alisema Makani kwa nafasi yake katika BoT alikuwa ni mtu
aliyejali maslahi ya nchi na pia mwepesi wa kutoa taarifa za fedha.
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa
alisema walifaidi utawala wa sheria na aina ya uongozi wa Makani
kutokana na kuwa mwanasheria.
Alisema Makani ni mfano wa kuigwa kwa kuwa alikuwa ni mtu wa watu
aliyekuwa na kipaji cha kuelewa wananchi ambapo urefu wake uliweza
kuonekana kila mahali alipoenda sambamba na ucheshi wake.
Asema kuwa Makani alizaliwa mwaka 1936 katika Hospitali ya Kolandoto,
Shinyanga na kusoma shule ya msingi Ibadakuli mkoani humo. Alifauru
sekondari na kupelekwa Chuo Kikuu cha Makerere, ambako alifuzu na kupata
Shahada ya Kwanza katika Uchumi (BA Economics).
Mwaka wa 1961 alikwenda Chuo Kikuu cha Liverpool, nchini Uingereza na
1965 akatunukiwa Shahada ya Sheria (LLB) alirudi nchini ambapo
aliajiriwa na serikali kama Mwanasheria wa Serikali kwa muda mfupi kabla
hajapandishwa cheo na kuwa Exchange Control Manager wa Benki Kuu.
Makani ni mwasisi wa CHADEMA mwenye kadi namba tatu baada ya Edwin
Mtei, na marehemu Brown Ngwilulupi. Mwaka wa 1998 akachaguliwa kuwa
mwenyekiti chama hadi 2003.
Makani pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi za wakurugenzi katika
Shirika la Ndege Tanzania, Williamson Diamond, Tanzania Breweries, Benki
ya Taifa ya Biashara na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Law
Society.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment