Mwakyembe alipuka tena
Aanika madudu yaliyomng’oa mkurungezi ATC
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harison Mwakyembe, ameendelea kuwasha
moto ndani ya Shirika la Ndege (ATCL) ambapo jana aliweka bayana sababu
kadhaa za kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
hilo, Paul Chizi.
Akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo katika karakana ya uwanja
wa ndege jijini Dar es Salaam, Mwakyembe alisema kamwe hawezi kufanya
kazi na watendaji wabovu na kuwataka wale walioumizwa na maamuzi yake
kuacha kazi mara moja.
Huku akionyesha kukasirika, waziri huyo aliapa kuendelea kufukuza
watendaji wengine zaidi watakaobainika kwenda kinyume na sheria.
Akitaja sababu zilizomwondoa Chizi, alisema kuwa uteuzi wake haukuzingatia tarartibu za utumishi wa umma.
“Chizi katika ripoti yake ya uzoefu wa kazi inaonekana kuwa
alishastaafu kwa mujibu wa sheria ambapo kwa wafanyakazi wa aina yake
kuna taratibu za kuwaajiri, hivyo anatakiwa azifuate ili kuajiriwa
tena,” alisema.
Mbali na hilo, sababu nyingine iliyomponza mkurugenzi huyo ni kuingia
mkataba wa kukodi ndege bila ridhaa ya serikali wala wizara husika.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe alipotakiwa aeleze kwa nini mkurugenzi huyo
alifanya hivyo, alisema anaogopa kusema kwani huenda akazidi kuibua
mjadala zaidi katika taifa.
“Inasikitisha sana kuona kuwa ilifika mahali watu wakaona shirika ni
mali yao na kufanya maamuzi vile wanavyotaka huku wakisahau kwamba
wananchi wanaliangalia shirika hilo linavyouawa,” alisema.
Alisema kuwa serikali mbali na kutoridhia pia ukodishwaji huo
haukufuata taratibu za manunuzi ya umma kwani ndege hiyo ilinunuliwa
nchini Liberia ambako bidhaa zote chakavu ‘mikweche’ kama baiskeli,
pikipiki na ndege zimekuwa zikipelekwa huko na nchi zilizoendelea.
Alieleza kukerwa na kitendo cha watendaji wa shirika hilo kujinunulia
magari ya kifahari wakati serikali ilitoa fedha ili shirika lifufuke.
“Maana inashangaza iweje idara na kampuni ndogo zinaweza kujiendesha
na kusimama zenyewe lakini ATCL imekuwa ikibebwa hadi leo pamoja na kuwa
na wafanyakazi wazuri ambao wakienda kufanya kazi katika makampuni
mengine wanafanya vizuri,” alihoji.
Alisema kuwa serikali inajua wako mawakala wa makampuni ya ndege
binafsi, wanaodhani wataiua ATCL kumbe wanajiua wenyewe, na hivyo
kuwaonya akisema kama bado wapo ni bora waondoke wenyewe kabla
hajawaondosha.
Alisema yuko tayari kufikishwa mahakamani kwa ajili ya suala hilo kwani wanaofanya hivyo ni sawa na kuchezea sebuleni kwake.
Akifafanua zaidi madudu ndani ya ATCL, Mwakyembe alisema kuwa fedha za
bima ya ndege iliyodondoka mkoani Kigoma takriban dola bilioni saba,
tatu za awali zililipwa na iliagizwa ziingizwe katika akaunti ya Shirika
Hodhi la Mashirika ya Umma(CHC) lakini watendaji wakafanya kinyume.
“Watendaji hao hawakufanya hivyo na kuamua kuziingiza katika akaunti
ya ATCL, ambapo kati ya fedha hizo tumekuta dola bilioni mbili na dola
bilioni moja zilizosalia hazijulikani zilipopelekwa,” aliongeza.
Waziri huyo aligusia pia hatua ya baadhi ya maafisa kwenda nchini
China na kukaa huko takriban siku 45 kwa ajili ya kusimamia sare za
wafanyakazi, jambo ambalo alidai ni ufujaji wa fedha za umma kwa
kugharamia sare moja dola 49,900.
Kuhusu ajira ndani ya ATCL, Dk. Mwakyembe alisema kuna waajiriwa wengi
waliokwishastaafu na pia ajira mpya zilitolewa bila kufuata tararibu
ikiwemo kutangaza nafasi zilizopo ili wenye sifa washindane.
Alisema kuwa badala yake watu wamekuwa wakipeana ajira hizo kwa
kufahamina na kuacha wale walio na sifa, jambo alilodai kuwa walikuwa
wameamua kufukuza menejimenti yote, lakini wakahisi wangekosa kumbukumbu
za urushwaji ndege.
“Baada ya kupitia baadhi ya mafaili ya watendaji hao tulikuta mwenye
afadhali ni Kaimu Mkurugenzi huyu niliyemteua, Kapteni Lusajo Lazaro,”
alisema.
Aliwaonya wanaozusha kuwa ametumia ukabila kumteua mkurugenzi huyo,
akidai kuwa amebebwa na sifa pamoja na uwezo wake kiutendaji.
Waziri huyo alisema kuwa wameunda tume ambayo anaamini itakuja na majibu mazuri yatakayoliwezesha shirika hilo kusonga mbele.
Aliwataka wafanyakazi waliobaki, kuchapa kazi ili kumrahisishia pale
anapoomba fedha serikalini aeleweke na kuongeza kwamba tayari
wameshakabidhiwa sh bilioni 4.9 kutoka hazina kwa ajili ya matengenezo
ya ndege.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo aliahidi kuyafanyia
kazi yale yote waziri huyo aliyowaagiza, na kutimiza malengo ndani ya
miezi mitatu waliyopewa.
Kwa niaba ya wanafanyakazi hao, Nelson Kalinga, alisema kusuasua kwa
ATCL kumechangiwa na serikali kutowasikiliza wafanyakazi, kwani tangu
awali walipinga kununuliwa kwa ndege hiyo ya Air Bus, ambapo
waliandamana na kuandika barua wizarani lakini hawakusikilizwa.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
إرسال تعليق