Simba, APR kumchangia Mafisango Dar

Simba, APR kumchangia Mafisango Dar 

MABIN
GWA wa soka Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam, wako katika maandalizi kwa ajili ya mechi ya hisani dhidi ya APR ya Rwanda, maalumu kuichangia familia ya aliyekuwa mchezo wao, marehemu Patrick Mutesa Mafisango.
Mafisango alifariki usiku wa kuamkia Mei 17 kwa ajali ya gari maeneo ya Veta Chang’ombe jijini Dar es Salaam na kuzikwa nyumbani kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC) ambapo ameacha wake na watoto watatu.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Simba, ‘Wekundu wa Msimbazi’, Evodius Mtawala, alisema wao kama walezi wa mchezaji huyo ambaye alifariki akiwa katika timu yao, wameandaa pambano hilo litakalopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, wiki moja kabla ya kuanza kwa michuano ya Kagame Cup.
Mtawala alisema watacheza pambano hilo na fedha zote zitakazopatikana wataipa familia ya mchezaji huyo, ikiwa ni kwa ajili ya kuwalea watoto watatu wa mchezaji huyo.
“Tumepanga hiyo mechi ichezwe wiki moja kabla ya michuano ya CECAFA ili tumchangie aliyekuwa mchezaji wetu, kwa kuwa yeye alitoa mchango wake mkubwa kwetu hadi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu bara pamoja na kufika hatua ya 16 bora ya michuano ya kimataifa licha ya kutolewa, hivyo tunawaomba wanachama na wapenzi wa Simba na mashabiki kwa ujumla kutuunga mkono,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic, anatarajia kurejea nchini siku 10 zijazo tayari kwa kuanza kukinoa kikosi chake kwa ajili ya michuano ya Kagame na mchezo huo wa Hisani.
Milovan aliiambia Tanzania Daima jana kwa njia ya mtandao kuwa kwa sasa yuko nyumbani kwao Serbia kwa mapumziko mafupi, mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu na kuwa atakaporejea ataanza kazi moja kwa moja.

Post a Comment

Previous Post Next Post