Simba, APR kumchangia Mafisango Dar
Mafisango alifariki usiku wa kuamkia Mei 17 kwa ajali ya gari maeneo
ya Veta Chang’ombe jijini Dar es Salaam na kuzikwa nyumbani kwao Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC) ambapo ameacha wake na watoto
watatu.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu
wa Simba, ‘Wekundu wa Msimbazi’, Evodius Mtawala, alisema wao kama
walezi wa mchezaji huyo ambaye alifariki akiwa katika timu yao,
wameandaa pambano hilo litakalopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam, wiki moja kabla ya kuanza kwa michuano ya Kagame Cup.
Mtawala alisema watacheza pambano hilo na fedha zote zitakazopatikana
wataipa familia ya mchezaji huyo, ikiwa ni kwa ajili ya kuwalea watoto
watatu wa mchezaji huyo.
“Tumepanga hiyo mechi ichezwe wiki moja kabla ya michuano ya CECAFA
ili tumchangie aliyekuwa mchezaji wetu, kwa kuwa yeye alitoa mchango
wake mkubwa kwetu hadi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu bara pamoja na kufika
hatua ya 16 bora ya michuano ya kimataifa licha ya kutolewa, hivyo
tunawaomba wanachama na wapenzi wa Simba na mashabiki kwa ujumla
kutuunga mkono,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Milovan Cirkovic,
anatarajia kurejea nchini siku 10 zijazo tayari kwa kuanza kukinoa
kikosi chake kwa ajili ya michuano ya Kagame na mchezo huo wa Hisani.
Milovan aliiambia Tanzania Daima jana kwa njia ya mtandao kuwa kwa
sasa yuko nyumbani kwao Serbia kwa mapumziko mafupi, mara baada ya
kumalizika kwa Ligi Kuu na kuwa atakaporejea ataanza kazi moja kwa moja.
إرسال تعليق