Dk Slaa: Maalim Seif msaliti
Mnyika ataka kauli ya JK kuhusu ushoga
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Wilbroad Slaa amesema Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ni msaliti wa demokrasia
nchini kwa kuwa hana dhamira ya kutetea mageuzi ya kisiasa kwa maslahi
binafsi.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Luatala, Kata
ya Sindano, Jimbo la Lulindi mkoani Mtwara jana, Dk. Slaa alisema kuwa
Maalim Seif ni kiongozi asiyeeleweka, na ameshindwa kutumia chama chake
cha CUF na nafasi aliyonayo kutatua matatizo ya wananchi wanyonge,
badala yake amekifanya kipoteze heshima na mvuto ikiwa ni pamoja na
kupoteza dhamira ya kushika dola.
“Tulimuamini Maalim na timu yake kuwa wangeweza kupambana kuisaidia
mikoa ya kusini, kwa maana wao washambulie huku na sisi maeneo mengine
na kisha tumuondoe adui. Lakini cha kusikitisha wenzetu wameungana na
hao tunaotaka kuwaondoa, na tunachoshuhudia huku sasa ni wananchi
kuaminishwa kuwa kuna vyama vya kidini vinafaya siasa,” alisema Dk.
Slaa.
Alisema kutokana na usaliti wa kiongozi huyo, hatakuwa tayari kukaa
nae meza moja kwa ajili ya kuzungumzia siasa, hata kama ataombwa na
wananchi, kwa vile haaminiki na anaweza kumsaliti.
Alidai kuwa, muungano baina ya Maalim Seif na chama chake na watawala,
umewafanya washindwe kupigia kelele uonevu unaofanywa na Serikali ya
CCM dhidi ya wakulima wa korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi, na
badala yake wabunge wa vyama hivyo (CUF na CCM) wakiungana kutetea vitu
visivyo vya msingi ikiwamo kudai posho katika vikao vya Bunge.
Dk. Slaa alisema hakuwahi kuwa na tuhuma zozote za ufisadi, ndiyo
maana Serikali ya CCM inashindwa kumdhibiti kila mara anapoamua kuweka
uozo wao hadharani, badala yake imekuwa ikifanya kila mbinu kumsingizia
mambo yasiyo ya msingi, ambayo mwishowe wananchi hubaini hayana ukweli
wowote.
Mnyika ataka kauli ya JK kuhusu ushoga
Katika hatua nyingine, CHADEMA kimemtaka Rais Jakaya Kikwete atoe
tamko na msimamo wa Tanzania kuhusu hatua ya Rais Barack Obama wa
Marekani kuidhinisha sheria ya ushoga nchini mwake.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye Kata za Mnavira
na Mchauru, Jimbo la Lulindi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA,
John Mnyika alisema ukimya wa Rais Kikwete hauleti picha nzuri katika
suala hilo linalopingwa na dini zote.
Kauli hiyo ya Mnyika ilifuatia swali aliloulizwa na Katibu wa Chama
cha Wananchi (CUF), Kijiji cha Rivango, Keneth Khamis aliyetaka kujua
ukweli kuhusu taarifa zilizowasilishwa kwao, zikieleza kuwa CHADEMA
inaunga mkono ushoga na usagaji, kutokana na kuwa na uhusiano na
ushirikiano na chama cha Conservatives cha Uingereza.
Alisema hizo ni propaganda zilizopangwa na CCM ili CHADEMA
kisikubalike katika jamii, na kusema kauli iliyowahi kutolewa na Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ikiihusisha CHADEMA na kuunga
mkono ushoga ni ya unafiki.
Alisema baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuukubali
ushoga na usagaji na kutaka iwe sehemu ya masharti kwa misaada
inayotolewa na nchi za Magharibi, CHADEMA ilipinga na kuweka wazi kwamba
haiungi mkono ‘uchafu’ huo.
Mnyika alisema kutokana na Rais Kikwete kwenda Marekani kwa lengo la
kutafuta misaada, kuna dalili ya kuwepo uwezekano wa taifa hilo
kupenyeza ajenda ya ushoga na ikakubaliwa na serikali kama ilivyotokea
kwa Malawi.
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
إرسال تعليق